Remarks by Chargé d’Affaires, a.i. Inmi Patterson on Visit to Mnazi Mmoja Hospital, Dar es Salaam

Deputy Chief of Mission Inmi Patterson
Chargé d’Affaires, a.i. Inmi Patterson
Chargé d’Affaires, a.i. Inmi Patterson

Habari za Asubuhi.

Niwashukuru sana Naibu Waziri wa Afya, Dr. Faustine Ndugulile na Mkurugenzi wa Hospitali, Dr. Sophiani Ngonyani kwa kunikaribisha mahali hapa.

Nimefurahi sana kuona hiki kituo na huduma zinazotolewa mahali hapa na kukutana na watu wanaofaidika na upimaji wa virusi vya Ukimwi, ushauri nasaha na matibabu.

Niko hapa asubuhi ya leo kuzungumza na ninyi kuhusu msaada wa Marekani katika kuboresha Afya kwa watanzania na Mpango wa Rais wa Marekani kukubaliaba na Ukimwi, yaani kwa kiingereza ‘President’s Emergency Plan for AIDS Relief” maarufu kama “PEPFAR”.

PEPFAR ilianzishwa mwaka 2003 na rais mstaafu George Bush kama mwitikio wa dharura wa mlipuko wa ugonjwa wa ukimwi.  Toka kipindi hicho imekua sana na kuwa programu yenye ufanisi mkubwa zaidi duniani katika kupambana na virusi vya ukimwi, ikiwemo hapa Tanzania.

Kabla ya kuanzishwa kwa PEPFAR, ukipimwa na kubainika kuwa na virusi vya ukimwi ilikuwa ni kama adhabu ya kifo kwa Tanzania na maeneo ya kusini na mashariki ya Afrika. Katika miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, watu wachache sana walikuwa wanapimwa virusi vya Ukimwi na ni watu 1500 pekee walioweza kupata matibabu. Matokeo yake watu wengi walioishi na virusi vya ukimwi hawakutibiwa na baadae kuishiwa kinga mwilini na wakawa wagonjwa. Wenye virusi vya Ukimwi ambavyo havikutibiwa waliambukiza wenza wao na watoto na wengi wao walikufa. Kilikuwa ni kipindi kisicho na matumaini. Nina uhakika wengi wetu hapa tumepoteza wapendwa wetu kwasababu ya Ukimwi.

Tumetoka mbali sana ndani ya miaka hii 15. Kwa sasa, PEPFAR inasaidia matibabu ya dawa zinazo ongeza urefu wa kuishi kwa watu takribani milioni moja Tanzania. Ninajivunia kutangaza leo kwamba, hadi kufikia Septemba 2019, Serikali ya Marekani, kupitia PEPFAR, itatoa nyongeza ya Dola Milioni 512 (Shilingi 1.17 Bilioni) ili kuboresha Uzuiaji, Upimaji na Matibabu ya Virusi vya Ukimwi Tanzania. Hii itaongeza jumla ya gharama za uwekezaji wa PEPFAR Tanzania tokea mwaka 2003, kufikia zaidi ya Dola bilioni 4.5 (sawa na Shilingi Trilioni 10.6)

Kutokana na hatua kubwa tunayopiga katika kuwapatia matibabu watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, tuko karibu sana kudhibiti mlipuko wa Virusi vya Ukimwi na kuzuia usambaazaji wake, lakini bado hatujafika tunakotaka kwenda na ili tufike huko inahitaji jitihada za makusudi kutoka kwetu sote ikiwemo, Wananchi wa Tanzania, na Serikali ya Tanzania.  Hapa tunazungumzia ofya yenu, afya ya watanzania wote.

Matokeo ya mwezi Disemba kutoka Tanzania HIV Impact Survey, ambao ni Utafiti uliofanywa juu ya Madhara ya Ukimwi Tanzania, ulituonesha kwamba Tanzania imeshuka tena ukilinganisha na nchi nyingine za Ukanda huu. Nusu tu ya waathirika wa virusi vya ukimwi wamepimwa na kujua kuwa wana virusi. Majirani wa Tanzania kama vile Uganda, Malawi na Zambia, wameweza kupata matokeo mazuri Zaidi.

Tanzania lazima irudi kwenye nafasi yake na hii itahitaji wananchi kuwa na uelewa zaidi na kwenda kupima, jitihada za kuwa na sera mpya na utekelezaji wa haraka wa sera hizo.  Ili kudhibiti mlipuko wa virusi vya ukimwi, PEPFAR imedhamiria kufanya idadi ya matibabu kufikia 1.3m ambayo ni sawa na asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi Tanzania.

Tutadhamiria kufanya wote wanaoishi na VVU wapimwe na kupata matibabu ya kuokoa maisha yao ili idadi ya vifo kutokana na Ukimwi iwe Sifuri (0). Watu ambao wametibiwa na kupona kwa dawa zinazo ongeza urefu wa kuishi kwa muda mrefu, kiwango cha virusi kwenye damu yao kiko chini sana na hawawezi tena kuambukiza wengine ukimwi. Hii inamaanisha kwamba matibabu yatatusaidia pia kufikia malengo yetu ya kutokuwa na maambukizi mapya kabisa. Na ili tufanikiwe kufikia na kuwasaidia watu wenye hofu ya kupima, lazima tufikie kiwango cha kutokuwa na Unyanyapaa kabisa. Lazima tujivunie na kuwapongeza watu wanaopima. Ni wajasiri wanaojitokeza kupimwa afya zao ili kisaidia familia zao na jamii yao.

Ninapata mashaka nikiona Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali ya Tanzania yakionesha punguzo la fedha kwenye Huduma za Afya. Afya ya watanzania lazima ibaki kuwa suala la muhimu zaidi kwetu sote. Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR na Mfuko wa Dunia inatoa zaidi ya asilimia 80 ya fedha kwenye programu za Ukimwi Tanzania. Ili kujenga programu endelevu, lazima tufanye kazi kwa pamoja kuhakikisha kunakuwa na msisitizo kwenye VVU/UKIMWI na magonjwa mengine yanayoua.

Ili kufikia malengo haya mwaka huu, inatupasa watanzania hususani wanaume na vijana kufanya upimaji wa ukimwi kuwa jambo la lazima. Kupima ukimwi ni sawa na kujiondoa kitambaa kinachokuziba machoni, ni kujiondolea upofu. Haibadilishi hali ya mtu. Haibadilishi kama una VVU au hauna. Kupima kunafungua macho ya mtu na ni hatua ya kwanza ya kujikinga na kifo kisicho cha lazima na kuacha kueneza VVU kwa wengine.

Katika miaka 15 iliyopita, Serikali zetu mbili zimekuwa zikijitoa kusaidia watu wanaoishi na VVU na kazi yetu ya kuhakikisha idadi inafikia sifuri, bado inaendelea. Leo tujitoe kwa upya na kuahidi kufanya zaidi na kumzuia huyu muuaji UKIMWI.  Sisi kama serikali ya Marekani, tupo hapa nanyi.  Je, nyinyi kama serikali ya Tanzania na watanzania, mko hapa na mko tayari?

Asanteni.