Remarks by Chargé d’Affaires Dr. Inmi Patterson, at the Ambassador’s Fund for HIV/AIDS Relief (AFHR) awards ceremony

Deputy Chief of Mission Inmi Patterson
Chargé d’Affaires Dr. Inmi Patterson

Venue: American Corner at the National Library, Dar es Salaam
Date: September 21, 2018

Karibuni, kila mmoja, kwenye hafla ya kutoa tuzo chini ya Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya VVU/UKIMWI nchini Tanzania. Hafla ya leo ni ya kipekee,  kwa kuwa tunaadhimisha miaka kumi ya Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya VVU/UKIMWI na pia maadhimisho ya miaka 15 ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI, PEPFAR, duniani.   Ndio maana, kupitia programu kama za Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya VVU/UKIMWI, sio tu tunalenga kupambana na ugonjwa bali pia kuwajengea uwezo watu wa Tanzania na jamii zao.

Kabla ya kuanzishwa kwa PEPFAR, ukipimwa na kubainika kuwa na virusi vya UKIMWI ilikuwa ni kama adhabu ya kifo.  Katika miaka ya elfu moja mia tisa na tisini (1990) na mwanzoni mwa miaka ya elfu mbili (2000) watu wachache sana walikuwa wanapimwa virusi vya UKIMWI na kati ya hao ni watu elfu moja na mia tano (1500) pekee walioweza kupata matibabu.  Kilikuwa kipindi kisicho na matumaini.  Kilikuwa kipindi cha kukata tamaa.  Ukweli ni kuwa, tangu nchi hii ipate uhuru, UKIMWI ulileta athari kubwa sana kwa afya na usalama nchini.

Lakini sasa hivi, zaidi ya watanzania milioni moja wanapata matibabu.  Kwa mara ya kwanza katika historia ya zama za sasa tumepata fursa ya kudhibiti ugonjwa bila chanjo.  Lakini, bado hatujafika tunapotaka, na ili tufike pale, itahitajika jitihada ya pamoja kutoka kwetu sote, ikiwemo PEPFAR na washirika wake, serikali ya Tanzania, asasi za kiraia na watanzania wote kwa ujumla.

Tunawategemea watu kama ninyi mnaofanya kazi bila kuchoka kusambaza habari za mafanikio  hadithi za watu wanaoishi na VVU ambao wana nguvu na afya, hadithi za watu wenye VVU waliopata tiba ya kuokoa maisha ili kuwalinda wenza wao na hadithi za watu wanaoishi na VVU, ambao wanachangia maendeleo ya nchi hii.

Kupitia Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya VVU/UKIMWI, Ubalozi wa Marekani unazisaidia jamii kutambua na kushughulika na changamoto ambazo zimetambuliwa na wao wenyewe. Misaada hii imeendelea kukua tangu ilipoanzishwa mwaka 2009, sasa tunaweza kutoa misaada zaidi; mwaka huu tumepokea maombi 254 yaliyovunja rekodi, kutoka mashirika ya asasi za kiraia nchini kote. Hivyo, wanufaika 19 mnaowaona mbele yenu leo ni miongoni mwa walio bora kati ya bora, wakifanya kazi kwa bidii kuwasaidia watu wanaoishi na VVU katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na VVU

Ninajivunia kutangaza tena kwamba, hadi kufikia Septemba 2019, Serikali ya Marekani, kupitia PEPFAR, itatoa nyongeza ya Dola Milioni 512 (Shilingi 1.17 Bilioni) ili kuboresha Uzuiaji, Upimaji na Matibabu ya Virusi vya Ukimwi Tanzania. Hii itaongeza jumla ya gharama za uwekezaji wa PEPFAR Tanzania tokea mwaka 2003, kufikia zaidi ya Dola bilioni 4.5 (sawa na Shilingi Trilioni 10.6).

Vikundi vyote vinavyopokea misaada leo vimesimama kidete dhidi ya unyanyapaa na vinafahamu jinsi ya kuwasaidia watu katika jamii zetu.  Kwa wanaopokea misaada leo, asanteni sana kwa kujali na kwa uchapaji kazi wenu. Serikali ya Marekani inashukuru kwa nafasi hii ya kutimiza ndoto za matakwa yenu kuwa kweli kwa ajili ya watu katika jamii zenu. Lakini juhudi zenu zisiishie katika programu hizi.  Endeleeni kujali,  endeleeni kusaidia, na endeleeni kuleta tofauti!

Hongereni Sana.