Remarks by Chargé d’Affaires Inmi Patterson at the Awarding of Grants from the U.S. Ambassadors Fund for HIV/AIDS Relief (AFHR)

Deputy Chief of Mission Inmi Patterson
Deputy Chief of Mission Inmi Patterson
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Inmi Patterson

Septemba 6, 2017

Tangu ulipoanzishwa mwaka 2008, mpango huu umetoa ruzuku ndogo ndogo zenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni moja kwa mashirika madogo ya huduma kwa jamii ndani ya Tanzania.

Dola milioni moja ni kiasi cha kushangaza, lakini cha kushangaza zaidi ni watu na mashirika ambayo yamepewa ruzuku hizo.  Ni mtu wa kipekee anayeweza kubaini hitaji alilonalo mtu asiyemfahamu.  Mtu huyo ni wa kipekee zaidi kama atachukua hatua za kukidhi hitaji la mtu huyo asiyemfahamu.

Ninyi ndio watu hao, na ingawa siwafahamu kwa karibu, ninahisi kuwa nyote mna tabia ambayo inapatikana kwa nadra katika dunia hii yenye misukosuko ambayo sote tunaishi.  Kwa Kiingereza, tuna neno maalum tunaloita tabia hiyo, nalo ni “empathy”.  Ni uwezo wa kuelewa na kushiriki katika hisia za mtu mwingine.  Sisi sote tunahisi “huruma,” yaani kujisikia vibaya au kuhuzunika mara nyingi katika maisha yetu kwa sababu ya mabaya yaliyomkuta mtu fulani.  Ni wachache wetu tunaoweza kutambua kwa kina matatizo ya wengine kiasi cha kukubali kujituma ili kutatua matatizo hayo, kumwinua mtu huyo, na kufanya maisha ya huyo mtu yawe na nafuu kidogo. Adui akianguka muinue.

Ruzuku 18 tunazotoa leo zinaonyesha kuwa ndani ya Tanzania kuna tabia ya kushiriki hisia za wengine na kuwa haipo kwenye eneo moja tu.  Tabia hii ipo hapa Dar es Salaam, lakini pia ipo Pwani ya Kusini. Inapatikana Arusha, lakini pia karibu na mpaka wa Burundi.  Mahitaji yanayobainiwa yanaweza kuwa rahisi kama ukosefu wa choo au mafunzo ya ufundi na umeme wa jua.

VVU/UKIMWI ulipojitokeza kwa mara ya kwanza, ulisababisha uharibifu, kama  kimbunga au tufani, nchini kote. Na ukaacha uharibifu: familia zilizofiwa, mifumo ya huduma na afya iliyolemewa, na vurugu katika uchumi wa ndani.  Lakini pia janga la ugonjwa wa VVU/UKIMWI ulionyesha wazi uzuri wa watu.  Wanasayansi na madaktari walishirikishana walichofahamu, serikali na mashirika zilichepusha rasilimali ili kutafuta tiba na matibabu sahihi, na watu kama ninyi na mashirika ya kiraia mnayowakilisha yalichukua nafasi ya kuboresha maisha katika jamii zenu zilizoathirika ili kuzipa afueni.

Hivyo, nawashukuru nyote kwa kujali.  Serikali ya Marekani inashukuru kwa kupata fursa hii ya kusaidia kutimiza matamanio yenu kwa ajili ya watu katika jamii zenu.  Lakini jitihada zenu zisiishie kwenye mipango hii tu. Endeleeni kujali, endeleeni kutoa msaada.  Na zaidi ya yote, endeleeni na tabia ya kushiriki hisia za wanadamu wenzenu.  Endeleeni kuleta mabadiliko!