Flag

An official website of the United States government

Ujumbe wa Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald Wright
6 MINUTE READ
Julai 5, 2021

Katika Maadhimisho ya Miaka 245 ya Uhuru wa Marekani
na
Miaka 60 ya Uhusiano kati ya Marekani na Tanzania

Tarehe 4 Julai, Wamarekani tutaadhimisha miaka 245 ya uhuru wetu. Harakati zetu za kudai uhuru zilichagizwa na amali na maadili kadhaa: Usawa, uhuru, haki za binadamu kwa wote, na kupigania maendeleo, ustawi na heshima kwa watu wote. Maadili haya yanaendelea kutuongoza hadi leo.

Maadili haya haya ndiyo yameweka msingi wa urafiki wa karibu kati ya Marekani na Tanzania ambao mwaka huu unatimiza miaka 60.

Miaka sitini iliyopita, mwezi kama huu, Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere alikutana kwa mara ya kwanza na Rais wa Marekani John F. Kennedy. Kutokana na mkutano huo wa kwanza, Kennedy na Watu wa Marekani walivutiwa sana na Tanzania na kuweka dhamira ya kusaidia maendeleo ya taifa hilo changa. Dhamira hiyo haijawahi kuyumba.

Kwa miongo sita, Marekani imesimama bega kwa bega na watu wa Tanzania katika kuwasaidia kufikia malengo ya kitaifa ya maendeleo.

Pale taifa huru jipya la Tanzania lilipohitaji msaada wa kupanua miundombinu yake, Marekani ilijibu, ikijenga maelfu ya kilomita za barabara, ikiwemo barabara kuu ya Tanzania-Zambia ambayo imesaidia kuiunganisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni mashuhuri kwa kilimo na masoko ya kimataifa.

Ili kusaidia kutimiza maono ya Mwalimu Nyerere ya kuongeza kiwango cha upatikanaji elimu kwa wananchi wa Tanzania, Marekani ilituma Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps kwenda kufundisha katika shule za vijijini pamoja na kusaidia kujengwa kwa taasisi kadhaa za mafunzo ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Chuo cha Afrika cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Chuo cha Uongozi na vyuo vya ualimu huko Iringa na Dar es Salaam.

Pale Rais Ali Hassan Mwinyi alipoamua kufanya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa, Marekani ilikuwa mbia madhubuti katika kufikiwa kwa lengo hilo. Programu zetu zilisaidia kupanua sekta binafsi na kuimarisha uwezo wa asasi za kiraia na vyombo huru vya habari.

Pale Rais Mkapa alipoanzisha mapambano dhidi ya janga la VVU/UKIMWI nchini Tanzania, Marekani iliungana katika mapambano hayo kwa kuzindua Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR), programu kubwa zaidi kuwahi kuanzishwa na taifa lolote katika kukabiliana na maradhi ya aina moja katika historia ya wanadamu. Toka kuanzishwa kwa PEPFAR hapo mwaka 2003, vifo vitokanavyo na UKIMWI nchini Tanzania vimepungua kwa takriban asilimia 75.

Pale Rais Kikwete alipomueleza Rais Obama kuhusu haja ya kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini na kuinua tija katika kilimo, kwa mara nyingine tena Marekani ilijibu kikamilifu. Programu ya Changamoto ya Milenia (MCC) yenye thamani ya Dola za Kimarekani million 700, iliyozinduliwa mwaka 2008 iliwezesha kujengwa kwa njia za umeme zenye urefu wa kilomita 3,000 na vituo vya kupoozea na kusambazia umeme (power sub-stations) 800. Aidha, mpango wa kuendeleza kilimo wa Feed the Future ulioanza mwaka 2021 umewanufaisha wakulima 800,000 wa Kitanzania kwa kuwezesha matumizi ya teknolojia za kuongeza uzalishaji na tija katika eneo la kilimo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta milioni 3.6.

Marekani ina fahari kwa msaada iliyoutoa kwa Tanzania katika miongo hii kadhaa, lakini pia tunashukuru kwa msaada ambao Tanzania imetupatia. Kupitia jitihada zake za kusaidia harakati za kupigania uhuru barani Afrika, kuwahifadhi wakimbizi waliokimbia machafuko katika nchi zao na kutoa askari kwa ajili ya operesheni za kulinda amani katika kanda, kwa muda mrefu, Tanzania imekuwa nguzo imara ya utulivu na amani. Dunia nzima, ikiwemo Marekani, zina deni la shukrani kwa jitihada hizi. Nitakuwa mtovu wa shukrani kama sitataja msaada ambao Tanzania iliutoa kwa Marekani kufuatia shambulizi baya la bomu katika ubalozi wetu mwaka 1998. Waokozi wa Kitanzania na maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama walitoa msaada mkubwa na kuwafariji majeruhi pamoja na kusaidia kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria. Kwa kitendo hiki cha kirafiki, mimi na watu wa Marekani, tutashukuru milele na hatutasahau.

Leo ushirikiano kati ya nchi zetu mbili ni imara na wa karibu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Marekani na Tanzania tunafanya kazi pamoja ili:

  • Kupunguza kuenea kwa maradhi ya kuambukiza kama vile UKIMWI, malaria na COVID-19
  • Kuimarisha utoaji wa huduma za afya, hususan kwa akinamama, watoto na makundi mengine yaliyo katika hatari zaidi.
  • Kuongeza kiwango cha upatikanaji wa elimu
  • Kuwajengea uwezo wanawake, vijana na watu walio katika makundi maalum
  • Kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaheshimiwa
  • Na kuongeza ukuaji wa uchumi na biashara ili kukuza ustawi kwa nchi zetu mbili.

Katika miezi ijayo Ubalozi wa Marekani utakuwa ukisherehekea miongo sita ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kupitia kampeni tunayoiita “Pamoja 60.” Ninamuhimiza kila mmoja kufuatilia mitandao yetu ya kijamii ili kufahamu zaidi kuhusu shughuli nyingi na matukio yaliyopangwa kufanyika kama sehemu ya maadhimisho hayo.

Nikiwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania, nina dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wetu, ili miaka 60 ijayo iwe yenye tija na mafanikio kama ilivyokuwa kwa miaka 60 iliyopita. Ninafahamu kuwa kwa pamoja, hakuna jambo ambalo tutashindwa kulifanikisha.

Twende Pamoja

– Donald Wright
Balozi wa Marekani nchini Tanzania