Alex Morgan Na Servando Carrasco Mabalozi Wa Michezo Wa Marekani Nchini Tanzania

Dar es Salaam, TANZANIA. Mshindi wa Medali ya Dhahabu na Mshindi wa Kombe la Dunia la FIFA kwa soka la Wanawake akiwa na Timu ya Taifa ya Marekani, Alex Morgan na kiungo wa kati wa timu ya Orlando City SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani Servando Carrasco wapo katika ziara nchini Tanzania kama Mabalozi wa Michezo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Katika ziara hiyo, iliyoanza tarehe 4 hadi 8 Disemba, Mabalozi hawa wa michezo wanasaidia kukuza ushirikiano wa kitamaduni na kijamii kati ya Marekani na vijana wa Kitanzania, ikiwa ni pamoja Na vijana wa Kimaasai waishio chini ya Mlima Kilimanjaro.

Hali kadhalika, Morgan and Carrasco wataendesha mafunzo ya soka na kuzungumza na wanafunzi kutoka shule mbalimbali jijini Dar es Salaam na Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kuendesha mafunzo katika viwanja vya Jakaya Mrisho Kikwete hapo siku ya Jumatano tarehe 6 Disemba kuanzia saa 10:30 jioni. Aidha, mabalozi hawa wa michezo watatembelea programu mbili za soka ya wasichana ili kuonyesha na kusisitizia umuhimu wa kutoa fursa sawa kwa wote. Katika kusaidia programu hii kampuni ya Nike imechangia mipira kwa shule na washiriki wa programu.

Programu hii ya Mabalozi wa Michezo inayowalenga zaidi wasichana na wanawake katika michezo ni muendelezo wa mradi ujulikanao kama “Equal Playing Field” ambao hapo mwezi Juni 2017 uliwawezesha wanawake 30 kutoka mabara sita, akiwemo mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Marekani Lori Lindsey,  kuchezo soka katika kilelecha Mlima Kilimanjaro na kuweka rekodi ya dunia ya mechi iliyochezwa juu zaidi kiasi cha futi 18,747 (mita 5,714) kutoka usawa wa bahari.

Toka mwaka 2003, Idara ya Elimu na Masuala ya Utamaduni ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewapeleka zaidi ya wanamichezo 250 wa Kimarekani katika nchi 85 chini ya programu ya Mabalozi wa Michezo. Programu hii inasaidia kuwafikia wale ambao kwa kawaida hawawezi kufikiwa na  programu nyingine za kidiplomasia ili kukuza ushirikiano.

Fuatilia ziara ya Alex Morgan na Servando Carrasco katika  Instagram (@alexmorgan13, @serva5, na @USEmbassyTZ) na katika Twitter (@alexmorgan13, @Serva_Carrasco, na @AmEmbTZ).

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe:  DPO@state.gov.