Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam
11 Aprili, 2022
Mkurugenzi Mkuu Lwoga
Wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa
Wawakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje
Walimu na wanafunzi wa Chuo cha Diplomasia
Wana habari
Wageni waalikwa
Mabibi na mabwana
Ni heshima kwangu kuwa nanyi hapa asubuhi ya leo, mwanzoni mwa wiki muhimu sana katika historia ya Tanzania, Wakati taifa likiadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa mwasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere.
Sisi, kutoka Ubalozi wa Marekani, tuna Fahari kutoa mchango wetu mdogo katika maadhimisho haya, kwa njia ya maonyesho ambayo tunayazidua leo. Maonyesho ya kihistoria yakiangazia urafiki kati ya Mwalimu Nyerere na Rais wa Marekani John F. Kennedy.
Miaka 61 iliyopita, Mwalimu Nyerere alisafiri kwenda Marekani kukutana na Rais Kennedy katika Ikulu ya White House. Kutoka mkutano huu wa kwanza, urafiki kati ya viongozi hawa wawili ukaweka msingi wa urafiki baina ya mataifa na watu wan chi hizi mbili, urafiki ambao umeweza kudumu kwa muda mrefu. Ilikuwa, kwa jina la maonyesho haya, urafiki uliojenga historia.
Viongozi hawa walipokutana kwa mara ya kwanza, Tanzania – au Tanganyika, ilivyokuwa ikijulikana Wakati huo – ilikuwa bado taifa changa sana. Ukweli ni kuwa nchi hii haikuwa imepata uhuru kamili ambao ulipatikana baadaye mwaka 1961. Hivyo, Kennedy alielewa kazi kubwa iliyokuwa ikimkabili Mwalimu Nyerere katika kujenga nchi na kuwaunganisha watu wake pamoja. Ni kwa sababu hiyo Rais Kennedy alimuelezea Mwalimu Nyerere kuwa sawa na waasisi wa Taifa la Marekani Thomas Jefferson na George Washington.
Kwa upande wake Nyerere, alikiri kufanana kwa maadili ambayo kwayo taifa la Marekani liliundwa na matumaini ya taifa lake changa. “Taifa lenu limejengwa katika maadili imara ya kiimani (idealism). Vivyo hivyo kwa mataifa tunayojaribu kuyajenga Barani Afrika,” aliandika katika mojawapo ya barua nyingi ambazo viongozi hawa wawili walitumiana.
Kennedy alivutiwa sana na maono ya Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya Tanzania kiasi kwamba aliziagiza taasisi mbili alizozianzisha, USAID na Shirika la Wafanyakazi wa Kujitolea la Peace Corps, kuifanya Tanzania nchi ya kipaumbele katika jitihada zao. Kundi la kwanza la wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps liliwasidi Tanzania mwezi Septemba 1961, ikiwa ni miezi miwili tu baada ya Kennedy na Nyerere kukutana.
Kutokana na Kennedy na Nyerere kuheshimiana na kila mmoja kuvutiwa na mwenzake, watu wa Marekani waliazimia kwa dhati kusaidia maendeleo ya Tanzania. Kwa miongo sita iliyofuata dhamira hiyo ya dhati haijayumba.
Leo hii, uhisiano kati ya mataifa yetu ni wa karibu zaidi kuliko ilivyowahi kuwa Wakati wowote ule. Marekani ndiyo mfadhili mkubwa zaidi wa kiserikali kwa Tanzania, na tunafanya kazi kwa ubi ana serikali, asasi za kiraia na sekta binafsi tukijenga amani, ustawi, furs ana uhuru zaidi kwa nchi zetu mbili.
Mabibi na mabwana,
Maonyesho haya yanaonyesha urafiki uliokuwa na matokeo makubwa sana, lakini ambao kwa majonzi makubwa, ulikatishwa mapema sana. Kennedy aliuawa mwaka 1963. Toka Wakati huo, watu vizazi kwa vizazi wamekuwa wakijiuliza ni kwa jinsi gani historia ya Marekani ingeweza kubadilika iwapo Rais Kennedy angeendelea kubaki kuwa Rais na kama pengine angeshinda muhula wa pili wa Urais.
Kwa upande wa Mwalimu Nyerere, Tanzania ilikuwa na bahati kuendelea kuwa na mtu huyu wa kipekee kama sehemu muhimu ya maisha yake ya kisiasa kwa zaidi ya miongo minne. Tunapoadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere, Naungana na Watanzania wote na watu wengine duniani kote kuenzi uongozi wa Nyerere katika kipindi chote cha maisha yake akitumikia umma: Akiwa muumini kijana wa uhuru kutoka ukoloni; akiwa baba wa taifa la Tanzania na rais wa kwanza wa nchi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili kabla ya kung’atuka kwa hiari; akiwa ni msukumo kwa nchi kuingia katika zama mpya ya demokrasia ya vyama vingi na uchumi huria; na akiwa mzee mzalendo na mtetezi wa amani na usalama katika kanda.
Zaidi ya yote, tunamkumbuka Mwalimu Nyerere kama mtetezi mahiri wa heshima na utu wa kila mwanadamu, hususan wale wanaoishi katika nchi zinazoendelea duniani ambao mara nyingi sauti zao hazisikilizwi. Wakati Mwalimu Nyerere aliposafiri duniani kore na kuzungumza katika Umoja wa Mataifa au katika vikao vingine vya kimataifa, alihakikisha kuwa sauti zao zinasikika.
Na hii ni mojawapo ya sifa zake kuu – na sifa kuu za Tanzania. Ninaamini ni kwa moyo huu huu wa Mwalimu Nyerere, ndiyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa mara nyingine amerejea katika kushiriki katika kushirikiana kimataifa (multilateralism) na anapaza sauti yake na sauti ya Tanzania katika vyombo vya kimataifa kama Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.
Tunatumaini, kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere, naye atatembelea Ikulu ya White House.
Mabibi na Mabwana,
Miaka 61 iliyopita Rais Nyerere na Rais Kennedy walipanda mbegu ya urafiki kati ya mataifa yetu. Mbegu hiyo ndogo imetunzwa kwa miongo kadhaa na leo imemea na kuwa mti mkubwa na imara kama mbuyu. Tukiwa na nguvu kubwa kama hiyo, ninaamini kwa dhati kwamba hakuna lengo litakalitushinda kulifikia na hakuna changamoto itakayotushinda kuitatua.
Tulikuwa Pamoja, tuko Pamoja, na tutakuwa Pamoja.
Asanteni Sana. Kwa haya machache, nina furaha kutamka kuwa maonyesho haya yamezinduliwa rasmi!