Anna Henga Mshindi Wa Tuzo Ya Kimataifa Ya Mwanamke Jasiri Ya Mwaka 2019

Washington, DC:  Anna Henga, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) amekuwa mtetezi wa haki za binadamu, hususan zile zinazowahusu wanawake na watoto katika kipindi chote cha utumishi wake. Jitihada zake zilitambuliwa hapo Machi 7 pale alipotunukiwa tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri kwa mwaka 2019 katika hafla iliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo na Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump.

Huu ukiwa mwaka wake wa 13, Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri hutolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa wanawake kutoka sehemu mbalimbali duniani walioonyesha ujasiri na uthubutu usiokuwa wa kawaida pamoja na uongozi katika kutetea na kupigania amani, haki, haki za binadamu, usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake. Toka kuanzishwa kwake hapo mwezi Machi 2007 zaidi ya wanawake 120 kutoka zaidi ya nchi 65 wamepatiwa tuzo hii.

Katika hafla ya utoaji wa tuzo hii, Waziri wa Mambo ya Nje Pompeo alisisitiza umuhimu wa kutambua na kuenzi jitihada za kijasiri za wanawake, “wanawake jasiri wapo kila mahali. Wengi wao hawatatambuliwa na kupewa heshima wanayostahili. Wanakabiliwa na changamoto kadhaa wa kadhaa, changamoto kubwa na muhimu….wanawake jasiri wapo kila mahali na wanahitajika kila mahali.”

Anna Henga anakuwa ni Mtanzania wa pili kutunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri, akifuata nyayo za Vicky Ntetema aliyepata tuzo hii mwaka 2016.