Dar es Salaam, TANZANIA — Alysha Clark, ambaye ni mchezaji wa kulipwa wa timu ya Washington Mystics inayoshiriki Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu kwa Wanawake nchini Marekani (WNBA) yupo nchini Tanzania akiwa ni Balozi wa Michezo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Balozi huyu wa Michezo anasaidia kuimarisha uhusiano wa kitamaduni na kijamii kati ya Marekani na vijana wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na vijana wa Kimaasai wanaoishi chini ya Mlima Kilimanjaro.
Aidha, Alysha ataendesha madarasa ya mafunzo ya mpira wa kikapu na kuzungumza na wachezaji wa kike wa mchezo huo jijini Dar es Salaam na Zanzibar ikiwa ni pamoja na kliniki zitakazofanyika katika Kiwanja cha Mpira wa Kikapu cha Ocean Road siku ya Jumanne, tarehe 15 Novemba Jioni na Jumatano tarehe 16 Novemba. Balozi huyu wa Michezo ataendesha mafunzo kwa wachezaji wa kike akiangazia umuhimu wa fursa sawa kwa wote.
Toka mwaka 2003, Idara ya Elimu na Masuala ya Utamaduni ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewapeleka wanamichezo wa Kimarekani zaidi ya 330 katika zaidi ya nchi 85 kupitia program za Mabalozi wa Michezo, jambo linalosaidia kuwafikia raia wa kigeni ambao hawafikiwi na aina nyingine za mahusiano ya kidiplomasia, ili kukuza ushirikiano katika masuala ya kipaumbele katika sera za Marekani.