Balozi wa Zamani wa Marekani Nchini Tanzania Athibitishwa Kuwa Kiongozi Mpya wa Shirika la Marekiani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID)

Tarehe 3 Agosti 2017, Bunge la Seneti la Marekani lilimuidhinisha Balozi Mark Andrew Green kuwa Kiongozi Mkuu mpya wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID). Akiwa Kiongozi Mkuu wa USAID, Balozi Green atasimamia taasisi kubwa zaidi ya Serikali ya Marekani inayojihususha na misaada ya maendeleo, inayoendesha shughuli zake katika zaidi ya nchi 100 kwa lengo la kukabiliana na umasikini uliokithiri na kuzisaidia jamii imara na za kidemokrasia kupata maendeleo kwa kadri ya upeo wa uwezo wao.

Balozi Green anaingia katika wadhifa huu akiwa na hazina kubwa ya uzoefu kutokana na kuhudumu kwake kama Balozi wa Marekani nchini Tanzania. Hivi karibuni, alihudumu pia kama Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Chama cha Republican (International Republican Institute) ambayo imekuwa ikitekeleza programu kadhaa za USAID nchini Tanzania na katika nchi mbalimbali duniani.

Katika kipindi chake akiwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania kuanzia mwaka 2007 hadi 2009, Balozi Green aliwezesha kuwepo kwa ushirikiano rasmi baina ya nchi hizi mbili katika baadhi ya programu kubwa zaidi za maendeleo zilizowahi kufadhiliwa na Marekani.

Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, unampengeza Balozi Green kwa kuidhinishwa kwake kuwa Kiongozi Mkuu wa USAID na unatarajia kuona mafanikio makubwa ya shirika hili chini ya uongozi wake mahiri.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.