Flag

An official website of the United States government

Maoni ya Balozi wa Marekani Donald Wright Katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani
4 MINUTE READ
Mei 3, 2021

Kwa takriban miaka 30, tarehe 3 Mei ya kila mwaka, dunia imekuwa ikiadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani inatupa fursa ya kuenzi nafasi na wajibu muhimu wa vyombo huru vya habari katika kimarishaa na kuhifadhi jamii zilizo huru na kuangazia kazi adhimu inayofanywa na waandishi wa habari, vyombo vya habari, wahariri, wafanyakazi na wengineo katika vyumba vya habari, studio na vituo vya radio za kijamii duniani kote kuwaelimisha na kuwahabarisha raia kuhusu masuala mbalimbali ya siku hadi siku.

Aidha, Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ni fursa ya kubainisha na kukumbusha kuhusu vitisho vikubwa vinavyowakabili waandishi na taasisi hizo za habari wakati zikitekeleza kazi yao hiyo muhimu.

Ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote, kuazimia na kujitoa kwa dhati kusaidia uhuru wa vyombo vya habari.

Toka nilipowasili Tanzania mwaka jana, nimejiwekea utaratibu wa kuwatafuta waandishi wa habari na kusikiliza simulizi zao. Ninafahamu kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa sana, kutoka mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia yanayotikisa misingi ya uandishi wa habari, kuzuka kwa mitandao ya kueneza taarifa za uongo na uzushi hadi sheria kandamizi za habari. Haijawahi kutokea kuwa vigumu zaidi kuwa mwandishi wa habari nchini Tanzania kama ilivyo sasa. Isitoshe, janga la COVID-19 limeongeza maradufu kila moja ya changamoto hizi.

Lakini pamoja na vikwazo vyote hivi, nina matumaini kuwa bado kuna mustakabali mwema kwa uhuru wa tasnia ya habari nchini Tanzania.

Kuhusu hitaji la kwenda na mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia, ninatiwa moyo na vyombo kadhaa vipya vya habari vilivyokubali kupokea teknolojia mpya katika uendeshaji na ufanyaji wake biashara. Serikali ya Marekani inafadhili program kadhaa za kusaidia maendeleo ya vyombo vya habari, zinazofanya kazi na wamiliki wa vyombo vya habari katika kubuni na kuboresha mbinu mpya za kibiashara zenye ufanisi zaidi. Nina matumaini makubwa kwamba jitihada hizi zitazaa matunda.

Katika kukabiliana na ongezeko la usambaaji wa taarifa zisizo sahihi na za uzushi kupitia mitandao yaa kijamii, nimefurahishwa na jitihada kadhaa zikiibuliwa humu nchini kukabiliana na changamoto hii. Ninapongeza kazi inayofanywa na taasisi kama Nukta Africa, ambayo kwa msaada wa Serikali ya Marekani, inakabiliana na uenezaji wa taarifa za uongo kwa kuwapatia waandishi wa habari na raia vijana ujuzi wa kuthibitisha ukweli wa taarifa (fact-checking) na ujuzi wa kidijitali (digital literacy skills).

Mwisho, kuhusu masuala ya kisheria yanayokwaza utendaji wa waandishi wa habari, nimetiwa moyo sana na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan za kuondoa baadhi ya vikwazo kandamizi kwa vyombo vya habari.  Ninafahamu kuwa hivi karibuni Serikali itaunda kamati ya kupitia sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na zile zinazokwaza uhuru wa habari na vyombo vya habari. Ninapongeza hatua hizi muhimu na kuwahimiza wadau wote wa habari kuzipokea kwa nia njema na dhamira safi pamoja na kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria zilizokwaza uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania katika miaka ya hivi karibuni. Aidha, nimetiwa moyo na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Serikali ya Tanzania za kuwawajibisha wanaowatisha na kuwanyanyasa waandishi wa habari. Ni matumaini yangu kuwa hatua hizi zitapanuliwa zaidi katika siku zijazo na hivyo kwa mara nyingine tena, waandishi wa habari wa Tanzania watapata uhuru na nafasi ya kufanya kazi yao.

Kwa kumalizia, napenda kuwashukuru waandishi wa habari wa Tanzania kwa wajibu muhimu wanaoutekeleza wa kuwafikishia raia wenzao habari na taarifa mbalimbali. Katika Siku hii ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Dunia, mimi na timu nzima ya Ubalozi wa Marekani tunatarajia kuendelea kushirikiana na wadau wote – iwe wa umma, sekta binafsi na wa kiserikali – katika kusaidia kuimarisha Uhuru wa Vyombo vya Habari.