Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani wa Peace Corps Arubaini na Watatu Waapishwa

Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani wa Peace Corps Arubaini na Watatu Waapishwa
Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani wa Peace Corps Arubaini na Watatu Waapishwa
Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani wa Peace Corps Arubaini na Watatu Waapishwa

Dar es Salaam, TANZANIA.  Tarehe 20 Aprili 2016 Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Virginia Blaser, aliwaapisha wafanyakazi wapya wa kujitolea wa Peace Corps wapatao 43 kuhudumu nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka miwili. Wafanyakazi hawa watapangiwa kufanya kazi katika wilaya 19 nchini, ambazo ni:

Iringa, Mufindi, Kondoa, Mbinga, Masasi, Ludewa, Lushoto, Songea, Hanang na Makete. Wilaya nyingine ni Singida vijijini, Same, Njombe, Manyoni, Shinyanga, Njombe, Makambako, Wanging’ombe na Mbeya

Hafla ya kuwaapisha wafanyakazi hao ilifanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI Dk. Deo Mtasiwa, Mkurugenzi wa Peace Corps nchini Tanzania Dk. Elizabeth O’Malley,watu mbalimbali waliowahi kuwa wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps katika nchi mbalimbali na maafisa kutoka katika taasisi mbalimbali wabia.

Akitoa nasaha kwa wafanyakazi hawa wapya wa kujitolea Kaimu Balozi Blaser alisema: “Kitakacho watambulisha na kuwapambanua katika mawazo ya Watanzania mtakaoishi nao na kufanya nao kazi katika kipindi cha miaka miwili ijayo, ni dhamira yenu ya dhati ya kujenga urafiki na kuimarisha Amani inayovuka mipaka ya nchi na maslahi mengine yoyote.”

Naye Naibu Katibu Mkuu Mtasiwa alisema; “Ninatoa wito kwa jamii, maafisa wa serikali na wadau wengine wote katika maeneo ambayo wafanyakazi hawa wa kujitolea watahudumu, kuwapatia msaada wa hali na mali na ule wa kitaalamu na kuwasaidia kuzoea utamaduni mpya na katika kujifunza kwao kiswahili. Aidha aliwaasa wafanyakazi wa kujitolea “kufanya kazi kwa bidii, kutenda yaliyo mema, kuwa na ari na hamasa kubwa katika kazi zenu, kufurahia uzoefu mtakaoupata na kujitahidi kuwa mfano mwema kwa watu wa Tanzania.”

Peace Corps ni taasisi ya Serikali ya Marekani iliyoanzishwa na Rais John F. Kennedy mwaka 1961 ambayo hivi sasa inahudumia zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea zaidi ya 8,000 katika zaidi ya nchi 75 duniani wanaohudumu kutokana na maombi ya nchi hizo. Kwa miaka 55, Peace Corps imekuwa taasisi inayoendesha shughuli za mabadilishano ya kiufundi na kitamaduni zisizoegemea mrengo wowote wa kisiasa na kidini. Zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 200,000 wamehudumu katika nchi 138. Peace Corps ina dhamira ya kukuza amani na urafiki duniani kwa kutekeleza malengo matatu yafuatayo:

  • Kutoa wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani watakaochangia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi itakayohitaji wafanyakazi hao;
  • Kukuza uelewa kuhusu Wamarekani miongoni mwa watu katika jamii zinazohudumiwa na Wafanyakazi wa kujitolea;
  • Kuimarisha uelewa wa Wamarekani kuhusu dunia na watu wake.

Zaidi ya Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps wapatao 2,600 wamehudumu nchini Tanzania toka mwaka 1962. Peace Corps hutoa wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani wenye taaluma stahiki  wanao fanyakazi katika jamii katika nyanja za elimu ya sekondari (wakifundisha hisabati, sayansi na Kiingereza), afya na elimu ya mazingira.

Wafanyakazi wa kujitolea husaidia na kutoa mafunzo kuhusu utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuzuia kuharibika kwa ardhi, kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi ardhi na matumizi ya mbinu bora za kilimo na uhifadhi wa misitu (agro-forestry) wakiweka msisitizo katika kufanya kazi kwa ubia na wanawake na vijana. Pia watatoa mafunzo na kuwezesha kuanzishwa kwa kilimo hai cha bustani (bio-intensive gardens) ili kuongeza upatikanaji wa chakula, na kuboresha lishe ya kaya pamoja na shughuli nyingine za kujiongezea kipato.

Aidha, wafanyakazi hawa wa kujitolea husaidia katika kuimarisha afya ya umma kwa kufanya kazi na vituo, vikundi vya kijamii na vile vilivyomo mashuleni vinavyotoa huduma na elimu ya afya ikiwa ni pamoja na zile zinazohusu kujikinga dhidi ya VVU/UKIMWI, matibabu na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI,yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi. Wafanyakazi wa kujitolea hufanya kazi kwa karibu na kamati za afya vijiji ili kubaini na kuchambua mahitaji na vipaumbele vya jamii na kushiriki katika shughuli zinazohamasisha mabadiliko ya tabia katika maeneo ya afya ya mama na mtoto, lishe, malaria, maradhi yanayosababishwa na maji yasiyo salama, afya ya uzazi na kinga dhidi ya VVU/UKIMWI.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana kwa barua pepe na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam.