Hatua Zilizochukuliwa na Serikali ya Marekani Kukabiliana na COVID-19 (3 Aprili, 2020)

Dar es Salaam: Serikali ya Marekani imejizatiti, na kila siku, kote duniani, inapiga hatua kukabiliana na changamoto ya kihistoria inayotokana na janga la COVID-19. Watu wa Marekani, kupitia taasisi za kiserikali, makampuni binafsi ya kibiashara, mashirika ya kiraia, mashirika ya misaada na vikundi vya kidini wametoa msaada mkubwa kwa waathiriwa wa virusi vya corona katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi janga hili, kuanzia Afrika hadi Asia. 

Nchini Tanzania, Marekani imetangaza kutoa msaada wa Dola za Kimarekani Milioni moja ili kusaidia jitihada za utoaji taarifa (risk communication) , miradi ya maji na usafi wa mazingira (water and sanitation), kuzuia na kudhibiti maambukizo, kutoa elimu ya afya kwa umma (public health messaging) na miradi mingine. Kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita Marekani imewekeza takriban Dola za Kimarekani bilioni 7.5 kwa maendeleo ya Tanzania na karibu Dola za Kimarekani bilioni 4.9 zilizoelekezwa kwenye sekta ya afya pekee. Hii ikijumuisha msaada wa zaidi ya shilingi 200,000 kwa kila Mtanzania ili kukabiliana na janga la VVU na UKIMWI nchini Tanzania.   

Toka mwaka 2009, Walipakodi wa Marekani wametoa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 100 kusaidia masuala ya afya na takriban Dola bilioni 70 kama misaada ya kibinaadamu duniani kote. Serikali ya Marekani inaendelea kuwa mtoaji mkubwa zaidi duniani wa misaada kusaidia sekta ya afya na misaada mingine ya kibinaadamu, huku misaada hiyo ikilenga kuwezesha maendeleo ya muda mrefu, kusaidia jitihada za kuwajengea uwezo wabia wetu na kukabiliana na majanga au dharura mbalimbali zinazojitokeza. Tunaongoza duniani katika utoaji misaada katika sekta ya afya na misaada ya kibinaadamu kukabiliana na janga la COVID-19. Kama alivyotangaza Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo hapo tarehe 26 Machi 2020, Marekani imetenga takriban Dola milioni 274 kama msaada wa dharura kwa sekta ya afya na huduma za kibinaadamu ili kukabiliana na janga la COVID-19. Pamoja na sekta binafsi nchini Marekani, watu wa Marekani wanaeandelea kuongoza katika kujitoa na kujitolea kukabiliana na janga hili 

Katika ngazi na nyanja mbalimbali, tunafanya kazi kwa makini kuhakikisha kuwa kipaumbele cha msaada wetu kinawekwa katika kusaidia jamii zile zenye uhitaji mkubwa zaidi. Hadi hivi sasa sehemu kubwa ya msaada wetu kukabiliana na janga hili unalenga utoaji wa madawa, vifaa tiba na zana nyinginezo (medical assistance and supplies). Hata hivyo, hivi karibuni jitihada hizo zitaongezewa nguvu na misaada ya ziada itakayolenga kusaidia kuimarisha mifumo ya afya ya wabia wetu na kukabili athari za kiuchumi, kijamii na kiusalama za mlipuko wa janga hili. 

To request more information, please call the U.S. Embassy Dar es Salaam Press Office at Tel: +255 22 229-4000 or email: DPO@state.gov