Flag

An official website of the United States government

Tahadhari ya Kiafya – Ongezeko la visa vya COVID-19
6 MINUTE READ
Febuari 10, 2021

Tahadhari ya Kiafya – Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam (10 Februari,2021)

Mahali:Tanzania

Tukio:Ongezeko la visa vya COVID-19

Ubalozi wa Marekani unafahamu kuwa pamekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya visa vya COVID-19 toka mwezi Januari 2021. Aidha, hatua za kuondosha na kuzuia maambukizi ya COVID-19 bado zimeendelea kuwa za kiwango cha chini.  Serikali ya Tanzania haijatoa takwimu zozote kuhusu visa vya maambukizi au vifo vilivyotokana na COVID-19 toka mwezi April 2020. Hospitali na vituo vya afya vya Tanzania vinaweza, kwa haraka sana, kuzidiwa kutokana na ongezeko la janga hili la kiafya. Uwezo mdogo wa hospitali nchini kote Tanzania unaweza kusababisha wagonjwa walio katika hali ya dharura kuchelewa kupatiwa huduma, jambo linaloweza kuhatarisha maisha.

Tahadhari ya Usafiri iliyotolewa kwa wasafiri wanaotaka kwenda Tanzania ni  Tahadhari ya daraja la 3 (Level 3) inayowashauri wasafiri kufikiria upya kuhusu safari zao (Reconsider Travel) kutokana na janga COVID-19.  Aidha, Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi ya Marekani (CDC)  inasema kuwa wasafiri waepuke kusafiri kwenda Tanzania. Taarifa zetu za hivi punde zaidi kuhusu COVID-19 zinaweza kupatikana katika ukurasa wetu – COVID-19 Information Page.

Kuanzia tarehe 26 Januari, abiria wote wanaosafiri kwa ndege kwenda Marekani walio na umri wa kuanzia miaka miwili na kuendelea, ni lazima waonyeshe cheti kinachoonyesha kuwa hawana maambukizi ya COVID-19 kutokana na vipimo vilivyochukuliwa ndani ya siku tatu kabla hawajasafiri.  Vinginevyo, msafiri anaweza kuonyesha nyaraka kutoka kwa mhudumu wa afya mwenye leseni (aliyesajiliwa) kuonyesha kuwa amepona maradhi ya COVID-19 siku zisizopungua 90 kabla ya safari yake.  Kwa taarifa zaidi na kuona maswali yanayoulizwa mara kwa mara, tembelea tovuti ya CDC – Frequently Asked Questions.

Upimaji wa virusi COVID-19 nchini Tanzania hufanyika katika Maabara za Serikali. Maelezo ya kina kuhusu upimaji huo (ikiwa ni pamoja na aina ya kipimo na utendaji/ufanisi wake) hayajawekwa wazi au kuthibitishwa na chombo kingine huru. Wakati ambapo kwa kawaida majibu ya vipimo hutoka baada ya saa 72, si wakati wote majibu hutolewa ndani ya muda unaotakiwa na kuna taarifa kuwa kuna nyakati vipimo hutoa majibu yasiyo na uhakika hivyo kuwafanya wale wanaopimwa kutakiwa kurudia upya vipimo baada ya siku kadhaa.  Hali kadhalika, baadhi ya wasafiri kutoka Tanzania waliopimwa na kukutwa kuwa hawana maambukizi ya COVID 19 kabla ya safari zao, waligunduliwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo baada ya kupimwa tena walipowasili katika nchi za kigeni.

Ubalozi wa Marekani unatoa huduma za uhamiaji (Consular services) kwa kiwango kidogo sana.  Tafadhali tembelea tovuti yetu kwa taarifa zaidi kuhusu miadi ya Huduma zinazotolewa kwa Raia wa Marekani (American Citizen Services) na Huduma za Viza (Visa services).

Ubalozi bado unaendelea kupendekeza kuwa watu wote wachukue tahadhari katika shughuli zao za siku hadi siku. (Mathalan, kuzuia/kupunguza idadi ya wageni wanaoingia nyumbani kwako) pamoja na kuchukua hatua stahiki za kupunguza uwezekano wa kuambukizwa unapokuwa nje ya nyumbani kwako (mathalan, kuweka umbali unaotakiwa kati yako na mtu mwingine – social distancing, vaa barakoa kwa usahihi, epuka mikusanyiko/misongamano na osha mikono yako mara kwa mara).

Hatua za Kuchukua:

 

Kwa Msaada:
Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam, Tanzania
686 Old Bagamoyo Road,Msasani,
S.L.P 9123
Dar es Salaam, Tanzania
+25522229-4000

drsacs@state.gov
https://tz.usembassy.gov