Hotuba ya Balozi Donald Wright katika Kongamano la Pamoja 60 Chuo Kikuu cha Dodoma
[Translation → English] |
Chuo Kikuu cha Dodoma
7 Juni, 2021
Waziri Mkenda
Katibu Mkuu Sedoyeka
Profesa Tenge
Dk. Mmari
Waheshimiwa wanajopo
Wahadhiri na wafanyakazi
Wanafunzi
Wageni waalikwa
Ni furaha kubwa kwangu kuwa nanyi leo. Ningependa kuanza kwa kumshukuru Waziri Mkenda kwa kuungana nasi asubuhi ya leo. Mheshimiwa Waziri, nafikiri uwepo wako hapa unaashiria umuhimu mkubwa ambao serikali ya Tanzania imeweka sio tu katika elimu ya juu, bali pia katika ushirikiano imara na wenye mafanikio makubwa ambao Marekani inaupata kutoka Wizara ya Elimu. Ahsante.
Ningependa pia kuwashukuru wenyeji wetu, Chuo Kikuu cha Dodoma, kwa msaada wake mkubwa kwa kongamano hili muhimu. Kipekee, napenda kumshukuru Profesa Tenge kwa ukarimu mkubwa alionipatia asubuhi ya leo na kwa kumuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Tunashukuru kwa makaribisho yenu mazuri.
Pia ningependa kumshukuru Dk. Mmari na wafanyakazi wa REPOA kwa kazi nzuri sana ya kuandaa kongamano hili na makongamano yaliyopita ya Pamoja 60.
Nitakuwa mtovu wa shukrani, nisipowashukuru wazungumzaji wetu na wanajopo wote wa kongamano letu la leo. Tunashukuru na kuthamini sana mchango wenu.
Mwisho, napenda kutambua uwepo wa wanafunzi wote waliopo hapa leo. Ninawapongeza kwa ushiriki wenu na ni matumaini yangu kuwa majadiliano yetu ya leo yatakuwa yenye manufaa makubwa kwenu.
Mabibi na Mabwana,
Kama ambavyo mnafahamu, mwaka jana tulitimiza miaka 60 ya ushirikiano rasmi wa kidemokrasia kati ya Marekani na Tanzania. Katika kuadhimisha hatua hiyo kubwa, Ubalozi wa Marekani uliungana na REPOA kuandaa mlolongo wa makongamano katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini Tanzania ili kuangalia na kuchambua sura mbalimbali za uhusiano kati ya Marekani na Tanzania katika miongo kadhaa iliyopita. Katika mlolongo huo tumefanya makongamano katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine.
Imestahili kwamba mlolongo wa makongamano haya unaishia hapa katika Chuo Kikuu cha Dodoma – Chuo Kikuu kipya zaidi cha umma Tanzania – kwa sababu leo hatuangazii siku zilizopita, bali tunaangalia mustakabali na siku zijazo.
Mada yetu ya leo ni “Mustakabali wa Mwelekeo wa Maendeleo ya Tanzania na Uhusiano na Marekani.”
Ni muhimu tukajadili na kuunganisha maoni na mawazo yetu pamoja kutafakari kuhusu siku zijazo kwa sababu bila mashaka yoyote, karne ya 21 itakuwa karne ya Afrika. Ifikapo mwaka 2050, mtu mmoja kati ya wanne duniani atakuwa ni Mwafrika. Changamoto kubwa zaidi zitakazoikabili dunia wakati huo zitakuwa katika bara hili. Na ninaamini kwamba suluhisho za changamoto hizo nazo zitapatikana hapa.
Kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Tony Blinken “Afrika ndiyo itakayojenga na kuamua mustakabali – sio tu wa watu wa Afrika bali pia wa dunia.”
Swali la leo ni kuwa, mstakabali huo utakuwaje.
Ninajua Waziri na wanajopo wetu watatoa mawazo yao kuhusu namna ambavyo Tanzania inaweza kutumia rasilimali na maliasili ilizojaaliwa kuwa nazo kuhakikisha inatumia vyema na kunufaika na fursa zinazojitokeza.
Kwa upande wangu, ningependa nizungumzie kwa undani kidogo kuhusu pale ambapo uhusiano kati ya Marekani na Tanzania unaelekea.
Nguzo kuu za uhisiano kati ya Marekani na Tanzania ni pamoja na:
- Kuwawezesha vijana kutumia na kunufaika na fursa zitakazojitokeza katika siku zijazo.
- Kuongeza biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu
- Kuimarisha amani na usalama katika kanda
- Na kuimarisha taasisi za kidemokrasia ili wananchi wote waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utawala
Kuhusu nguzo ya kwanza, tumedhamiria kwa dhati kuhakikisha kuwa vijana wa Tanzania wana afya, wanalishe nzuri, wameelimika vizuri na wana ujuzi sahihi utakaowawezesha kukamata na kuzitumia kikamilifu fursa zitakazojitokeza.
Ni kwa sababu hii, sehemu kubwa ya msaada wa maendeleo wa Marekani kwa Tanzania unaelekezwa katika programu za kusaidia afya na elimu kwa vijana. Tunafanya hivi kwa sababu tunafahamu mafanikio huanza katika umri mdogo.
Ni mwezi uliopita tu, tumetangaza kuzinduliwa kwa mradi wa Afya Yangu wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 250 utakaotekelezwa kupitia USAID kwa kusaidia afya ya mama na mtoto na kuboresha utoaji huduma za afya, hususan katika maeneo ya vijijini.
Aidha, Marekani inaisaidia Tanzania kushinda vita dhidi ya UVIKO-19. Siku chache zilizopita, niliungana na Waziri wa Afya Mwalimu kuzindua mpango wa Kimataifa ya Upatikanaji Chanjo ya UVIKO-19 (Global Vax initiative) mradi wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 25 kusaidia kuongeza kasi ya jitihada za Tanzania za utoaji chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa sababu, – kama ambavyo miaka hii miwili ilivyotufundisha – hakuna aliye lindwa kikamilifu kabisa mpaka sote tumekuwa salama na kulindwa.
Katika sekta ya elimu, Marekani inafanya uwekezaji mkubwa kuhakikisha kuwa vijana wa Tanzania wanapata msingi wa elimu bora toka wakiwa wadogo kabisa. Katika miaka mitano iliyopita pekee, tumechangia zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 65 kusaidia mfumo wa elimu ya msingi wa Tanzania hususan kupitia programu ya kusoma, kuandika na kuhesabu kwa madarasa ya 1-4.
Iwapo vijana wa Tanzania watakuwa wana afya njema na wameelimika vyema, wataweza kuchangamkia fursa zitakazojitokeza katika siku zijazo. Hapa ndipo pananipeleka katika nguzo ya pili ya uhusiano kati ya Marekani na Tanzania, ambayo ni uchumi, biashara na uwekezaji.
Ninapozunguka katika nchi hii na kuongea na watu, kila ninaekutana nae – iwe ni Waziri au muuza madafu mtaani – huniambia Watanzania wanataka biashara na si misaada. Ninakubaliana nao kwa asilimia 100.
Kuongezeka kwa biashara na uwekezaji kati ya Marekani na Tanzania kutazinufaisha nchi zetu zote. Nilipata bahati ya kuambatana na Rais Samia alipotembelea Marekani mwezi Aprili na nina furaha kuwaambia kwamba makampuni ya Kimarekani yamesikia ujumbe wa Rais kwamba Tanzania ipo tayari kwa biashara na wana hamasa kubwa ya kuazisha biashara zao katika nchi hii.
Makampuni ya Kimarekani hayaleti tu mitaji lakini pia yanaleta mbinu za kufanya biashara zilizo endelevu, zenye uwazi na zinazosukumwa na kuongozwa na maadili.
Tunataka kutengeneza nafasi za ajira katika jamii kwa manufaa ya jamii hizo. Tunaunga mkono hatua za kukabiliana na rushwa na kuongeza uwazi, ili viongozi na raia waweze kutathmini iwapo mikataba inayoingiwa kwa niaba yao, kweli ni yenye manufaa kwao. Aidha, tunataka kuwalinda wafanyakazi na kuyalinda mazingira.
Sehemu ya jambo hili inahusu kuwekeza katika nishati ya siku zijazo. Kwa kadri tatizo la mabadiliko ya tabia nchi linavyoongezeka, tutajielekeza zaidi katika vyanzo vya nishati jadidifu. Tanzania ina fursa kubwa sana katika kufanikisha azma hii.
Hapa Jirani katika mkoa wa Singida, Kampuni ya Kimarekani iitwayo Upepo inapanga kuwekeza mamia ya mamilioni ya dola katika mradi wa kuzalishaji umeme kutuma jua na upepo. Kampuni hii inafanya kazi kwa karibu na TANESCO na Wizara ya Nishati ili kukamilisha makubaliano, ambayo tunaamini yatasainiwa hivi karibuni ili kuanza ujenzi na hatimaye kuwapatia Watanzania umeme wa uhakika zaidi.
Nguzo nyingine ya uhusiano kati ya Marekani na Tanzania ni ushirikiano wa kiusalama. Inapokuja suala la kukuza amani na utulivu katika kanda, Tanzania, kwa miongo kadhaa, imekuwa mstari wa mbele kabisa. Iwe ni kwa kutumia diplomasia na kusuluhisha migogoro miongoni mwa majirani zake au kwa kutoa askari wake kushiriki katika oparesheni za kulinda amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, Tanzania imekuwa, kwa kunukuu maneno ya Rais Bill Clinton, “sababu na mhimili wa amani na ushirikiano katika kanda.”
Kwa Bahati mbaya, tunashuhudia kuongezeka kwa hali ya kukosekana utulivu na usalama barani Afrika – hata katika nchi zilizo karibu kabisa na Tanzania. Kushughulikia vitisho hivi itakuwa mojawapo kati ya changamoto muhimu ambazo Tanzania itakabiliana nazo katika miaka ijayo, na Marekani ipo tayari kutoa msaada wowote utakaoweza kuutoa. Sehemu ya utekelezaji wa jambo hii ni kuongeza ushirikiano kati ya majeshi yetu ya ulinzi. Ninafurahi kuwaeleza kwamba, kufuatia ziara ya mwaka jana ya Kamanda Mkuu wa Kamandi Maalumu ya Afrika ya Jeshi la Marekani (AFRICOM) Jenerali Townsend, ushirikiano wetu wa kiusalama umekuwa wa karibu na imara zaidi kuliko ilivyokuwa wakati mwingine wowote. Ni matarajio yetu kuwa uhusiano huo utaendelea kutanuka na kuimarika katika miaka ijayo.
Nguzo ya mwisho ya uhusiano kati ya Marekani na Tanzania ni ile inayogusa nyanja nyingine zote: kuheshimu utawala wa sheria, utawala wa kidemokrasia na kuheshimu haki za binadamu. Hizi ni nguzo ambazo kwayo maendeleo endelevu hujengwa. Historia inatuonyesha kuwa nchi zinazoheshimu maadili ya kidemokrasia, kwa kipindi kurefu huwa zina amani, utulivu na ustawi zaidi. Ili Tanzania iweze kunufaika kutokana na fursa za wakati ujao ni lazima watu wake wawe huru kutoa maoni yao na kushiriki kwa uhuru katika maisha ya kisiasa ya nchi yao.
Katika suala hili, ninafikiri hatua zilizochukuliwa hadi hivi sasa na Rais Samia ili kuongeza majadiliano ya kisiasa na kuvifungulia vyombo vya habari, ni hatua njema kabisa. Ni matumaini yetu kuwa huu ndiyo mwelekeo ambao nchi hii itaendelea kuufuata.
Mabibi na mabwana,
Tupo hapa leo kuzungumza kuhusu siku za baadae na ninapoiangalia hadhira hii na sura zote hizi za vijana, ninakumbushwa kwamba vijana wa leo ndio viongozi wa kesho. Jambo hili linanipa matumaini makubwa kuhusu wapi nchi hii inaelekea.
Nikiwa Balozi, nimepata Bahati ya kukutana na vijana wengi wa Kitanzania, hususan, vijana wanaoshiriki katika programu zetu mabadilishano ya kielimu kama ile ya Young African Leaders Initiative (YALI) – na wakati wote wameniacha nikiwa nimepigwa na bumbuwazi kutokana na matumaini hamasa na ari kubwa waliokuwa nayo.
Kazi ilipo mbele yetu wakati tukiangalia miaka 60 ijayo na zaidi ya hapo, ni kutumia kikamilifu ari, nguvu na matumaini ya vijana hao ili kujenga Tanzania ya baadaye ambayo vijana wanaitaka na kuistahili.
Tunapoanza jitihada hizi, tambueni kwamba watu na Serikali ya Marekani itakuwa nanyi bega kwa bega, kama ilivyokuwa katika miaka 60 iliyopita.
Tulikuwa pamoja, tupo pamoja, na tutakuwa pamoja.
Kwa mara nyingine, asanteni sana ninawatakia kongamano jema na lenye mafanikio.