Flag

An official website of the United States government

Hotuba ya Balozi Donald Wright katika Ufunguzi wa Kituo cha Uendeshaji Huduma za
Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar
7 MINUTE READ
Mei 19, 2021

Habari za Asubuhi,

Waziri wa Afya Mazrui,

Mkurugenzi Mkuu,

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani, (WHO) Dr. Andemichael

Mwakilishi wa taasisi ya Global Fund- Bw. Nelson Msuya

Ndugu Wanahabari

Na weheshimiwa wafanyakazi wenzetu wa Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar.

Nimefurahi sana kuungana nanyi hivi leo katika ufunguzi rasmi wa Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii.

Janga la COVID-19 limetuthibitishia kuwa tishio la ugonjwa mahali fulani, ni tishio la ugonjwa kila mahali. Kama alivyosema Samia Suluhu Hassan, “hakuna nchi yoyote iliyo kisiwa.” Sisi sote ni sehemu ya dunia iliyoungana, hivyo sote tupo katika hatari ya maradhi yanayosambaa ndani na hata nje ya mipaka yetu. Madhara makubwa ya janga la COVID-19 katika mwaka uliopita, yametudhihirishia wazi jambo hili. Aidha, yametudhihirishia umuhimu wa kuwa na nguvu kazi iliyoelimishwa vizuri na kuwa na vyombo na mifumo yenye ufanisi inayoweza kutambua kwa haraka hatari zozote zinazojitokeza na kuchukua hatua za haraka kuzikabili. Leo, tupo hapa tukizindua Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar (Zanzibar Public Health Emergency Operations Center) – kituo cha uratibu kinachosaidia sana kulinda afya na ustawi wa watu wa Zanzibar – na wengine duniani kote.

Uwezo wa kuthibitisha iwapo kweli tukio linaloleta kitisho kwa afya ya umma linatokea ama la ni wa muhimu sana. Kupitia shughuli zake za ukusanyaji wa haraka wa taarifa, uthibitishaji wa haraka (verification) wa taarifa hizo na usambazaji wake kwa wakati mwafaka, kituo hiki kinasaidia sana kuhakikisha kuwa wakati wote Zanzibar inakuwa tayari kuchukua hatua dhidi ya vitisho kwa afya ya umma. Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar ni kitovu cha usimamizi ambapo uratibu wa mawasiliano yote, ufuatiliaji na operesheni za kukabiliana na maradhi makubwa zinafanyika. Nina fahari kwamba miaka miwili iliyopita, Serikali ya Marekani kupitia Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Maradhi (CDC), ilisaidia uanzishwaji wa kituo hiki kwa kutoa miundombinu ya kimenejimenti, vifaa muhimu, programu za kompyuta (software) za kuhakikisha kuwa kituo kinafanya shughuli zake sawa sawa pamoja na mafunzo kwa watendaji muhimu kupitia mpango mahsusi wa mafunzo wa CDC uitwao Public Health Emergency Management Fellowship. Mafanikio ya kituo hiki kwa sehemu fulani ni matokeo ya uongozi mahiri, weledi na kujitoa kwa dhati kwa Dk. Haji kwa kituo.  Toka kilipoanza shughuli zake, kituo kimekuwa kitovu cha jitihada za kujiweka tayari kukabiliana na dharura (Emergency Preparedness) pamoja na uratibu wa hatua za kukabiliana na dharura hiyo zinazochulikiwa na sekta mbalimbali. CDC na Taasisi ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani ya Kupunguza Vitisho (U.S. Defense Threat Reduction Agency) wamesaidia kwa kutoa mafunzo kwa wanaepidemiolojia wanaosimamia timu za wataalamu wanaotumwa kwa haraka maeneo ya matukio (rapid response teams) ili kuweza kuwapeleka mahali popote na wakati wowote wanapohitajika.

Kutokana na jengo hili lililokarabatiwa upya tunalolizindua leo, kituo hiki kitakuwa na ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake muhimu, ambayo umuhimu wake umeongezeka zaidi kutokana na janga la COVID-19. Toka janga hili lilipozuka, Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii kimekuwa nyenzo muhimu sana katika ukusanyaji wa rasilimali, kutathmini hatari na kujenga uwezo wa ufuatiliaji wa watu wanaotoka na kuingia visiwani. Aidha, kituo hiki kimekuwa nyenzo muhimu katika ufutiliaji wa maradhi zaidi ya COVID-19 kikiweka kipaumbele katika kuhakikisha hali njema ya kiafya kwa Wazanzibari – na hii ikijumuisha kuwafanya wakazi na wageni wanaotembelea visiwa hivi kuwa salama ili biashara na utalii uweze kuendelea.

Janga la COVID-19 limetuonyesha jinsi hali yetu ya kawaida inayoweza kubadilika ghafla – na ni kwa kiwango gani sisi sote tunategemeana (watu walio ndani na nje ya mipaka yetu) katika kulinda na kuboresha maisha yetu na kuendeleza shughuli zinazotupa riziki yetu. Janga hili limetuonyesha pia jinsi tunavyoweza kuwa dhaifu kwa kitu ambacho hata hatuwezi kukiona kwa macho – ambacho ni kusambaa kimya kimya kwa maradhi ya kuambukiza. Kwa uwekezaji unaoendelea kutoka kwa wafadhili na Serikali ya Zanzibar, tunaweza kufanya kazi ili kuhakikisha kuwa maradhi yanazuiliwa, yanatambuliwa kwa haraka na kushughulikiwa kikamilifu na kwa ufanisi. Sasa tunafahamu kuwa hatari kubwa inayoweza kutukabili. Hata hivyo, nimetiwa moyo sana kuona kituo hiki na watu walio nyuma yake, wamejiandaa kikamilifu wakiwa na ari kubwa ya kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza.

Kudhibiti janga maana yake ni kufuatilia kwa karibu (surveillance), kubaini na kuzuia kuenea kwa maambukizi. Lakini pia kunamaanisha kuwatibu wale ambao tayari wameambukizwa kwa kuwapatia huduma bora zaidi kwa kadri inavyowezekana. Kwa msingi huo, leo hii, ninafurahi kutangaza kuwa Serikali ya Marekani, kupitia USAID na CDC imetenga zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 1.2 ili kusaidia jitihada za Wizara ya Afya ya Zanzibar za kukabiliana na mlipuko wa maradhi.  Fedha hizi ni sehemu ya uwekezaji muhimu katika usalama wa afya unaofanywa na Serikali ya Marekani katika miaka ya hivi karibuni.

Pasiwe na shaka yoyote, kwamba Marekani ipo bega kwa bega na Wizara, wahudumu wa afya na watu wa Zanzibar katika mapambano dhidi ya COVID-19.

Mapendekezo yaliyotolewa Jumatatu na Kamati Maalumu ya wataalamu wa afya iliyoundwa na Rais Samia ya kutathmini ugonjwa wa COVID-19 ni hatua kubwa na muhimu katika mapambano dhidi ya janga hili. Wataalamu wamependekeza kuongeza utoaji na uchangiaji taarifa/data juu ya ugonjwa huu, kuchukuliwa kwa hatua madhubuti za kinga na tiba kuudhibiti ugonjwa huu (mitigation measures), na kuhakikisha upatikanaji wa chanjo zilizothibitishwa kitaalamu kua salama na zenye ufanisi kwa wote watakaozihitaji, hususan wale walio katika makundi hatari zaidi ya kuambukizwa. Aidha, wamependekeza kuimarishwa kwa uwezo wa kiuchunguzi ili kubaini kwa ufanisi zaidi milipuko ya maradhi ya kuambukiza pamoja huduma za maabara ili kupanua uwezo wa upimaji, jitihada ambazo ZPHEOC inaweza kuchukua dhima kubwa ya kuongoza. Ninaamini kuwa – iwapo yatafuatwa – mapendekezo haya yataiweka Tanzania ( Zanzibar na Bara) katika mwelekeo sahihi wa kuishinda COVID-19. Ni matumaini yangu kuwa Rai Samia atayazingatia kwa kina.

Kwa kumalizia, ninapenda kuishukuru timu ya Wizara ya Afya ya Zanzibar kwa kazi kubwa inayofanya ya kuzuia, kubaini na kushughulikia vitisho vyote kwa afya ya umma. Ninathamini sana ushirikiano kati ya Serikali ya Zanzibar, Serikali ya Marekani, Shirika la Afya Duniani (WHO) na taasisi ya Global Fund. Ni matumaini yangu kuwa tutaendeleza ushirikiano huu wenye tija ili kuifanya Zanzibar salama, yenye afya na ustawi.