Flag

An official website of the United States government

Hotuba – Balozi Dkt. Donald J. Wright katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani 2022
10 MINUTE READ
Disemba 1, 2022

1 Desemba 2022, Lindi, Tanzania

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack
Mheshimiwa Godwin Mollel, Naibu Waziri wa Afya
Waheshimiwa Makatibu Wakuu,
Dkt. Leonard Maboko, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS,
Bi. Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS
Zlatan Milicic, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini,
Watu wanaoishi na VVU,
Wabia wanaotekeleza miradi mbalimbali,
Mabibi na Mabwana, Itifaki imezingatiwa.

Ni furaha kubwa kwangu kwa mara nyingine kuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hapa Tanzania. Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na Uongozi wa Mkoa, ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Zainab Telack kwa kuandaa tukio hili muhimu hapa Lindi.

Awali ya yote, kwa niaba ya serikali ya Marekani, napenda kukushukuru wewe Mheshimiwa Rais, kwa dhamira yako ya dhati katika kupambana na VVU hapa Tanzania, kama inavyodhihirishwa na ushiriki wako katika tukio hili muhimu. Toka ulipoingia madarakani, umefanya afya ya watu wako kuwa jambo la kipaumbele. Hongera sana Mheshimiwa Rais kwani Tanzania imeweza kutoa chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa zaidi ya asilimia 85 ya watu wake wanaotakiwa kuchanjwa. Kujitoa kwako kwa dhati na mchango wako mkubwa katika suala hili na katika kusaidia mapambano ya kitaifa dhidi ya VVU unaonekana wazi na unathaminiwa sana. Uongozi wako kupitia Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI na TACAIDS umekuwa imara na thabiti na umeendelea kuiweka Tanzania katika njia sahihi kuelekea udhibiti wa janga la VVU.

Aidha, ninafuraha kumkaribisha tena Bi. Winnie Byanyima nchini Tanzania. Bi. Byanyima, nina fahari kuchangia pamoja nawe jukwaa hili hivi leo. Jitihada zako ukiwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti UKIMWI (UNAIDS) za kuhakikisha kuwa suala la VVU/UKIMWI haliondoki katika orodha yetu ya vipaumbele tunaposhughulikia majanga, ni muhimu sana katika siku na zama za leo wakati Dunia inapambana na UVIKO-19.

Leo, tunapoadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani, tuna fursa ya kutafakari kuhusu hatua tulizopiga katika kukabiliana na VVU, Kuwakumbuka na kuwaenzi mamilioni ya watu duniani kote waliopoteza maisha kutokana na maradhi yanayohusiana na UKIMWI na kukumbushana kuhusu kazi iliyo bado mbele yetu. Tupo hapa kukumbuka ni wapo kazi hii ilianzia na hatua tulizopiga hadi sasa. Tupo hapa pia kushirikiana kuweka dhamira ya dhati kukamilisha ngwe ya mwisho katika safari ya kudhibiti janga hili nchini Tanzania – lengo ambalo kwa hakika tunaweza kulifikia.

Nikiwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania, suala la afya, hususan jitihada za kutokomeza VVU, ni miongoni mwa vipaumbele vyangu. Ninaona fahari kwa kazi kubwa iliyofanyika kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI– (PEPFAR). Ukiwa ni ufadhili mkubwa zaidi duniani uliowahi kutolewa na nchi yoyote kwa ajili kupambana na ugonjwa wa aina moja. PEPFAR, toka mwaka 2003 imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 6 kusaidia jitihada za Tanzania za kupambana na VVU. Kauli mbiu ya Siku ya UKIMWI Duniani ya 2022 ya Serikali ya Marekani ni “Tujiweke kwenye jaribio la Kufikia Usawa Kutokomeza VVU (“Putting Ourselves to the Test: Achieving Equity to End HIV”), kaulimbiu inayohimiza uwajibikaji na kuchukua hatua. Kaulimbiu hii inaakisi dhamira ya dhati ya serikali ya Marekani ya kutokomeza VVU/UKIMWI kama kitisho kwa afya ya jamii kupitia PEPFAR kwa kushughulikia tofauti za kiafya zilizopo katika jamii, tofauti zilizokuwepo hata kabla hatujakumbwa na janga la UVIKO-19, Homa ya nyani (monkeypox) na milipuko mingine ya maradhi. Aidha, kauli mbiu hii inakwenda sambamba kabisa na kaulimbiu ya Siku ya UKIMWI Duniani ya UNAIDS’: Imarisha Usawa (Equalize). Kutokomeza janga la VVU kutawezekana tu pale ambapo makundi yote katika jamii, watoto, wasichana, vijana wa kike na makundi maalumu wataweza kufikia malengo ya 95-95-95.

Wakati ambapo Serikali ya Marekani inajiandaa kuadhimisha miaka 20 ya PEPFAR hapo mwezi ujao, tunatafakari mafanikio yote tuliyoyafikia hadi hivi leo hapa Tanzania. Mathalan, miaka 20 iliyopita, kulikuwa na watu 1,000 tu waliokuwa wakipatiwa Dawa za Kufubaza VVU (ARV) hapa. Hii inamaanisha kuwa kuambukizwa VVU ilikuwa sawa na kupata hukumu ya kifo. Leo kuna zaidi ya Watanzania milioni 1.5 wanaopatiwa matibabu haya ya ARV yanayookoa maisha yao. Kwa matunzo na matibabu sahihi, watu wanaoishi na VVU wanaweza sasa kuishi maisha yenye afya na kufikia malengo yao ya kimaisha.

Tunapongeza uongozi wa Serikali ya Tanzania chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Afya kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP). Mmehakikisha kuwa Tanzania inatekeleza sera sahihi na afua bora kuhakikisha watu wanaoishi na VVU wanaweza kufikia huduma za upimaji wa VVU, wanapata dawa bora, wanadumu katika matibabu na wanaendelea kupata huduma za matunzo. Ninaipongeza pia OR-TAMISEMI ambao wameweza kwenda na mabadiliko katika mapambano dhidi ya VVU kupitia usimamizi wa kimkakati wa utoaji wa huduma katika ngazi za mikoa na wilaya. Kwa hakika mafanikio ya Tanzania ni kazi ya Serikali nzima.

Mpango wa Tanzania wa kupambana na janga la VVU umekuwa na mafanikio makubwa. Toka kufanyika kwa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania uliofanyika mwaka 2016-2017, pamefanyika jitihada kubwa kushughulikia mapungufu katika kubaini wanaoishi na VVU wapya na kusaidia zaidi maeneo ya kijiografia ambako kuna pengo kubwa la matibabu ya ARV. Hivi sasa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2022-2023 unaendelea. Matokeo ya utafiti huu unategemewa kutoa mwongozo wa kutufikisha kwenye maili ya mwisho ya kudhibiti janga hili.

Japokuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika jitihada zake za kudhibiti janga hili, bado kuna maeneo ambayo tunahitaji kuyashughulikia zaidi ili kutokomeza VVU nchini Tanzania. Ni lazima tutegemee sayansi na kulenga kutekeleza afua zenye matokeo makubwa. Ni lazima tuhakikishe kuwa huduma ya kutumia dawa kinga za kuzuia maambukizi ya UKIMWI (PrEP) inapatikana kwa wingi zaidi ili kuzuia maambukizi mapya kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi. Ni lazima tuwatambue watu wazima, vijana na watoto ambao hawajui hali zao za maambukizi – hususan, wale waliopo katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi – kuhakikisha wanapata matibabu na kuwa virusi walivyonavyo vinafubazwa. Ni lazima tuendelee kufanya kazi pamoja kuhakikisha kuwa huduma za kukabiliana na VVU ni zile zinazomlenga na kumjali mpokea huduma na zinaandaliwa maalumu kwa makundi yanayoathiriwa zaidi na VVU.

Mwisho, wakati tunasherehekea hatua tuliyofikia, hatuna budi kutambua kuwa kazi ya kufikia udhibiti wa VVU inafanywa kuwa ngumu zaidi kwa kuwepo kwa unyanyapaa, ubaguzi, sera, na desturi ambazo zinafanya iwe vigumu kwa baadhi ya watu walio katika hatari zaidi ya maambukizi ya VVU kupata huduma za VVU na msaada wa jamii wanaohitaji. Mbali na uwekezaji katika huduma za kuzuia na kutibu VVU, tunapaswa pia kuweka kipaumbele katika juhudi kuelekea demokrasia jumuishi. Demokrasia ya kweli na ushiriki mpana wa raia inachangia moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa afya ya jamii. Tunafurahishwa na vikosi kazi vya Rais Hassan na Rais Mwinyi vinavyojumuisha vyama vya siasa, viongozi wa dini, na asasi za kiraia kushughulikia mapungufu ya utawala na kutoa mapendekezo ya kushughulikia mapungufu hayo.

Tumeshuhudia mipango ikiibuliwa kulenga athari za VVU zisizo na uwiano miongoni mwa makundi tofauti ya jamii. Mkutano wa kikanda wa Umoja wa Mataifa ulioangazia kushughulikia viupaumbele vya wanawake na wasichana katika kupambana ya UKIMWI ulifanyika nchini Tanzania; ukichagiza mabadiliko ya kisera yanayozingatia uongozi na sauti za wanawake vijana na wasichana. Zaidi ya hayo, Tanzania ilitia saini kuwa mbia muhimu katika Umoja wa Kidunia wa Kutokomeza UKIMWI kwa Watoto (Global Alliance to End AIDS in children) ifikapo 2030, ubia uliotangazwa mwanzoni mwa mwaka huu. Kundi la watoto likiwa limeachwa nyuma ikilinganishwa na watu wazima katika safari ya kuelelea malengo ya 95-95-95, hakuna tena muda wa kupoteza katika kutatua changamoto hizi. Seikali ya Marekani kupitia program ya PEPFAR ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa watoto wote wanaoishi na VVU wanaweza kupata matibabu na kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Ili kuendeleza mafanikio ambayo Tanzania imeyapata, na kufikia lengo letu la pamoja la kuutokomeza kabisa UKIMWI ifikapo 2030, hatuwezi kuacha kujielekeza katika kuhakikisha afua dhidi ya UKIMWI ni endelevu. Programu ya Serikali ya Marekani ya PEPFAR, Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria, na mashirika ya Umoja wa Mataifa ndio yanayotoa sehemu kubwa ya msaada wa kiufundi na kifedha kusaidia jitihada za Tanzania za kukabiliana na UKIMWI. Kutokana na kupungua kwa bajeti na kuibuka kwa vipaumbele vingine vya afya ya jamii vinavyohitaji pia kushughulikiwa, msaada huu, kama unavyotolewa hivi sasa, hautaendelea kuwepo milele.

Tunatambua kuwa ili kuhakikisha utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI ni endelevu kwa muda mrefu ni lazima kufanya mabadiliko makubwa katika namna mfumo mzima wa mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI unavyoendeshwa. Ninaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuchukua hatua muhimu ya awali kwa kuanzisha kikosi kazi maalumu cha kiufundi kitakacho tathmini vipengele vyote vya programu ya kupambana na VVU endelevu. Hii ni kuanzia kuhamasisha utafutaji wa fedha kutoka vyanzo vya humu humu nchini hadi kuhakikisha kuwa kuna rasilimali watu ya kutosha katika sekta ya afya na ufuatiliaji thabiti na mifumo ya kukabiliana na magonjwa. Uendelevu haupimwi na kiasi cha dola au shilingi bali hupimwa kwa uongozi wa kisiasa.

Serikali ya Marekani inaihimiza Serikali ya Tanzania kuongeza zaidi jitihada zake za kuhakikisha uendelevu wa mapambano dhidi ya VVU katika nguzo zote tatu za uendelevu ambazo ni kisiasa, kiprogramu na kifedha – ili kuweza kuongoza, kusimamia na kufuatilia shughuli za kupambana na VVU na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya VVU kwa uwazi, ufanisi, usawa na kwa namna endelevu.

Tukirejea kwenye kaulimbiu ya siku ya UKIMWI Duniani ya mwaka huu, “Imarisha Usawa.” Huu ni wito wa kuchukua hatua madhubuti za kutambua na kushughulikia hali ya kukosekana usawa kwa watu wote katika upatikanaji wa huduma muhimu za VVU na UKIMWI hususan vijana wa kike, wanaojidunga dawa za kulevya na makundi mengine waliokatika hatari zaidi ya maambukizi ya VVU. Kaulimbiu hii ituhamasishe sisi sote tuchukue hatua kwa pamoja, kama wabia, pamoja na serikali ya Tanzania, kulitokomeza janga la VVU/UKIMWI duniani kote.

Kwa kumalizia, ni vyema tujikumbushe kuwa hali ya kukosekana usawa duniani inatuathiri sote, bila kujali wewe ni nani au unatoka wapi. Ni lazima tuhakikishe kuwa kila mmoja, kila mahali, anaweza kuzifikia kwa usawa huduma za kinga dhidi ya VVU, upimaji, matibabu na matunzo. Ni lazima huduma za afya ziandaliwe na kutolewa ili kuyafikia na kukidhi mahitaji ya makundi ya jamii yaliyo katika hatari na yanayoathiriwa zaidi, na hii inajumuisha kutekeleza sera ya kutovumilia kabisa unyanyapaa na ubaguzi wa aina yoyote katika utoaji wa huduma zote za afya. Kwa pamoja, tutaendelea kupiga hatua ya kuboresha afya za Watanzania. Ninaona kwamba sote tuliokutanika hapa leo tupo tayari kuhuisha tena ahadi yetu ya kupambana na ubaguzi au hali ya kutokuwepo usawa na kutokomeza VVU.

Asanteni sana