Hotuba ya Kaimu Balozi Dk. Inmi Patterson – Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari

Ukumbi: Morena Hotel – Dodoma
3 Mei 2019

Ningependa kuungana na wenzangu hapa leo kutoa salamu zangu za rambirambi kwa familia na marafiki wa Marehemu Dr. Reginald Mengi. Katika tulivyosema jana kwenye mitandao ya kijamii, wajibu wa Dr. Mengi katika kuendeleza ukuaji na maendeleo ya Tanzania haupimiki, pia kama ulivyo mchango wake kwa vyombo vya habari vya Tanzania kama muasisi wa IPP Media. Maombi na sala zetu ziende kwa wanafamilia wake katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Waziri Mwakyembe, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Mahenge na wageni waalikwa watendaji wa vyombo vya habari, kuhusu umuhimu wa vyombo vya habari, ningependa kuanza kwa kumnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Antonio Guterres. Nchi zetu mbili. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani, zote ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na zenye msimamo mzuri. Hivyo tunaweza kudhani kwamba serikali yangu na serikali yenu; watu wa Marekani na watu wa Tanzania, wanakubaliana na anachosema Katibu wao wa Umoja Mataifa.

Bw. Guterres anasema:  “Hakuna demokrasia iliyokamilika bila upatikanaji wa habari za wazi na za kuaminika. Ni nguzo ya kujenga taasisi za haki na zisizo na upendeleo, kwa kuwawajibisha viongozi kwa kusema ukweli madarakani.”  Naomba nirudie nukuu hii, kwasababu maneno ya Katibu Mkuu wetu yanahitaji usikivu wetu kamilifu.

Tutarudi tena baadaye kwenye alichosema Katibu Mkuu, lakini kwanza ninataka kuwapeleka safarini. Tusafiri pamoja, sote, kwa sekundi moja, hadi mwaka 1971 – kupitia angani hadi Marekani – nchi ambayo ninaiwakilisha.

Mwaka huo, mtu mmoja jasiri alivujisha nyaraka za siri nyeti kwenye gazeti muhimu nchini Marekani. Nyaraka hizo zilionesha kwamba serikali ya Marekani iliwadanganya wananchi wake kuhusu sababu zilizoifanya Marekani kupigana vita katika nchi nyingine; huko Vietnam; na pia kuhusu mahali na jinsi vita hiyo ilivyokuwa ikipiganwa. Nyaraka hizo zinajulikana kama “Nyaraka za Pentagon” na nina hakika wengi wenu mnazikumbuka.

Kama alivyoandika mmoja wa majaji wa Mahakama Kuu, Jaji Black, wakati huo: “Ni vyombo vya habari huru na visivyo na vizuizi pekee ndivyo vitakavyoweza kwa ufanisi kufichua udanganyifu serikalini.”

Unaweza kuona kutoka alichoandika Jaji Black kwanini watu wa Marekani na hasa wapinzani wa kisiasa wa vitendo au sera za serikali wangependa kuona vyombo vya habari huru na visivyo na vizuizi vinavyoweza kufichua kila kitu serikali inachokosea. Lakini kwanini serikali nayo ingetaka vyombo vya habari huru na visivyo na vizuizi?

Ingawa nyaraka zile zilitajwa na serikali ya Marekani kama “siri nyeti”, gazeti liliamua kwa maslahi ya umma nyaraka zile zichapishwe. Na ilizichapisha kwenye ukurasa wake wa mbele.

Kama unavyoweza kuona, serikali, yaani serikali yangu, haikupenda kabisa. Gazeti liliiweka hadharani taarifa ya siri kuhusu vita ambayo ilikuwa bado inapiganwa. Lakini haikulifungia gazeti. Kwanini? Kwababu haikuwa na mamlaka ya kisheria kufanya hivyo. Sasa, unaweza kuuliza: Kwanini wakati huo serikali haikupitisha sheria itakayoipa mamlaka ya kuyafungia magazeti yatayochapisha makala inazoziona kama ni kinyume cha sheria? Kwasababu haiwezi. Mabadiliko ya kwanza ya katiba ya Marekani, ambayo ni sheria yetu mama, kama ilivyo katiba yenu ya Tanzania, inalizuia bunge letu kutunga sheria yoyote itakayominya uhuru wa habari.

Seneta wa Marekani, Birch Bayh, alisema wakati huo mvutano huu kati ya serikali ya Marekani na vyombo vya habari ulikuwa ukiendelea, kwamba wakati serikali ilikuwa ikisema jambo moja na wananchi wanajua kitu tofauti kutokana na uzoefu wao, “pengo la uaminifu” hujitokeza. Kwa maneno mengine, wananchi huacha kuiamini serikali inachowaambia, hata kama ni cha kweli! Na hivyo kuifanya kazi ya serikali kuwa ngumu zaidi kwenye maeneo mengi.

Kwa kuwa serikali yangu haikuweza kulifungia gazeti lile, hata pale ilipochapicha nyaraka za siri nyeti, ikajaribu kufanya kitu kingine bora. Iliiomba mahakama, mahakama zetu kutoa hukumu kwamba gazeti lile halikuwa na haki ya kuchapisha nyaraka zile za siri nyeti. Kesi hiyo ya serikali baadaye ilikatiwa rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Marekani. Na mahakama iliamua kwamba haki ya vyombo huru vya habari na haki ya wananchi kupata ambacho Katibu wa Umoja wa Mataifa alikiita “habari ya wazi na ya kuaminika”, ilikuwa muhimu zaidi kuliko kulinda siri za serikali. Kwa maneno mengine, Haki ya kupata habari ya watu wa Marekani ilikuwa muhimu sana, na wajibu wa vyombo vya habari kuwapatia habari ilibidi kulindwa.

Naomba nirudi kwa ufupi kwenye mojawapo ya vitu alivyosema Katibu Mkuu wetu. Aliita habari za kuaminika kwamba ni “nguzo ya kujenga taasisi za haki na zisizo na upendeleo.” Hii ni kauli yenye nguvu sana. Anasema kwamba huwezi kuwa na bunge linalofanya kazi, biashara zinazofanya kazi, shule zinazofanya kazi, mahakama zinazofanya kazi, bila kuwepo taarifa za kuaminika. Ukimwajiri mfanyakazi mwenye shahada ya chuo kikuu, na baadaye ukagundua kwamba kumbe hajui kusoma wala kuandika, haraka sana utapoteza imani na mfumo wa chuo kikuu au taasisi inayothibitisha shahada za chuo kikuu.

Ni lazima tutambue kwamba jukumu la kuhakikisha taarifa zetu zinabaki kuwa za kuaminika ni la kila mtu, kuelewa kwamba uhuru wa vyombo vya habari unapimwa kwenye uwezo wa vyombo vya habari katika kukusanya na kuripoti taarifa hizo za kuaminika na si kwa idadi ya machapisho ambayo huenda yanadai kuwa hivyo.

Vyombo vya habari huru ni mapigo ya moyo ya jamii yoyote iliyo hai. Yanasukuma damu ambayo ndio habari, kupitia mwili, ambao ni watu, wanaoitumia katika kufanya maamuzi ya jinsi ya kuishi maisha yao.