Hotuba ya Kaimu Balozi Dk. Inmi Patterson – Uzinduzi wa Majadiliano ya Kibiashara kati ya Tanzania na Marekani

Ukumbi: Hyatt Regency Hotel
Juni 17, 2019

Nakushukuru Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Angela Kairuki, kwa kuanzisha mazungumzo haya na Chama cha Wafanya Biashara wa Marekani nchini Tanzania kwa ushiriki mzuri na mchango wake katika kufanikisha tukio hili.

Nimefurahi kuwa hapa pamoja nanyi leo kuzungumzia vigezo muhimu katika kuwezesha mahusiano ya kibiashara na uwekezaji yenye manufaa kwa pande zote mbili kati ya Marekani na Tanzania. Wakati Waziri Kairuki alipopendekeza wazo la mazungumzo haya, Ubalozi wa Marekani ulikubali haraka kuwa mwenyeji wa tukio hili leo, kwasababu ya umuhimu tunaouweka kwenye ushiriki wetu kiuchumi na Tanzania.

Kwa kweli, kuendeleza mahusiano ya kibiashara na nchi za Afrika ili kuongeza ustawi wa Marekani na Afrika ni kipaumbele cha kwanza cha Mkakati wa Marekani kwa Afrika. Uwekezaji wa nje na sekta binafsi inayokua vizuri ni jambo la lazima kama serikali ya Tanzania itataka kufikia malengo yake ya kuwa nchi inayojitegemea ya uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

Aidha, mazungumzo ya leo yanaendana na uzinduzi wa kesho nchini Msumbiji kuhusu Mkakati wa Rais wa Marekani unaofahamika kama “Prosper Africa” (Stawisha Africa) – ni mkakati wa serikali nzima unaolenga kuongeza maradufu biashara na uwekezaji kati ya Marekani na Africa. “Prosper Africa” itawakutanisha wataalamu wa kiufundi na kisheria na pia mashirika kutoka sekta binafsi na serikali, wote wakifanya kazi kwa pamoja kuongeza upatikanaji wa nishati barani Africa.

Marekani haiangalii kufanya biashara tu nchini Tanzania, bali inaangalia ushirikiano na wabia wa Tanzania. Biashara inapaswa kuwa huru, ya haki, ya pande mbili, inayozingatia sheria za kimataifa za biashara na kutoa fursa zaidi za uwekezaji. Hii inahusu kutengeneza ajira kwa wote wamarekani na watanzania. Tunaunga mkono marekebisho ya sera yanayoongeza uwazi na ushindani nchini Tanzania na tunafanya kazi kuelekea mafanikio makubwa na viwango bora vya maisha. Katika shughuli za kiuchumi nchini Marekani tunasisitiza wa usawa pande zote mbili na kamwe si kujishusha chini.

Vitendo vina nguvu zaidi kuliko maneno. Ili kuwavutia na kuwabakisha wawekezaji, wakiwemo wawekezaji wa kimarekani, serikali ya Tanzania inabidi isonge mbele zaidi ya mazungumzo na kuchukua hatua madhubuti kuhimiza uwekezaji.

Tathimini ya awali ya bajeti ya mwaka 2019/2020 (Mwaka elfu mbili na kumi na tisa, elfu mbili na ishirini) iliyotolewa wiki iliyopita imebainisha vivutio vipya kwa wawekezaji, kwa mfano punguzo la kodi ya mapato kwa wazalishaji wa ndani wa taulo za kike, punguzo au kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vifaa vinavyotengeneza bidhaa za kilimo na mbogamboga, sabuni na nepi. Vivutio hivi ni mwanzo tu, lakini vinatoa ishara ya maana kwamba sasa Tanzania “iko tayari kufanya kazi”. Wakati tuko hapa leo, wawekezaji kwenye ukumbi huu wanayo fursa ya kupendekeza vivutio muhimu zaidi ambavyo serikali inaweza kuvitoa ili kuchochea uwekezaji mpya.

Masuala Yaliyokwama Ya Muda mrefu
Tunasisitiza utekelezaji wa dhana ya kuheshimu mikataba, wakati Tanzania ikitarajia kuvutia mapato zaidi ya uwekezaji wa moja kwa moja. Kimsingi Makampuni ya Kimarekani yanaangalia sera zinazotabirika, urahisi katika utawala wa kufanya biashara na kuzingatia utawala wa sheria yanapofikiria uwekezaji.

Mjasiriamali yeyote aliyefanikiwa atakuambia kwamba ili apate mafaniko zaidi ni lazima apange malengo ya muda mrefu. Ili kufanya kazi kwa mafanikio na kudumu, biashara inahitaji mfumo wa sheria, mamlaka ya uthibiti na kodi ambao ni endelevu na wa wazi. Wanahitaji mazingira ambayo sheria za utendaji kazi haziwezi kubadilika ghafla katikati. Kuna makampuni ya Kimarekani Tanzania, mengi yako hapa ukumbini na wako makini katika kufanya biashara hapa, lakini wanatafuta ufumbuzi wa masuala yaliyokwama muda mrefu, kwa mfano urefu wa muda unaochukua katika kupata vibali, kulipa kodi na taratibu na ada zinazobadilika mara kwa mara. Kwa mfano, licha ya kuwasilisha TRA na kaguzi zinazofanywa na idara mbalimbali za serikali, makampuni yanadai mamilioni ya dola kwa ajili ya marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi zingine. Wengine hutumia muda wao wa thamani kufuatilia kwenye ofisi kadhaa juu ya suala moja la kiutawala bila kupata ufumbuzi wa suala hilo.

Umuhimu wa Sekta Binafsi
Ni sekta binafsi pekee inayoweza kuzalisha idadi ya ajira zinazotakiwa kukuza uchumi Tanzania. Mabadiliko ya sera zinazosaidia sekta binafsi yanasaidia kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na kuimarisha sekta binafsi na ukuaji wa ajira.

Sekta binafsi ni muhimu katika maendeleo ya uchumi na lazima iangaliwe, ithaminiwe na ichukuliwe kama mshirika anayeheshimiwa. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, serikali ya Tanzania imepoteza uaminifu kwa sekta binafsi. Kuna pengo la uaminifu kati ya kinachoelezwa kuwa ni uungwaji mkono wa serikali na hatua madhubuti zinazochukuliwa kuimarisha mazingira ya biashara za ndani na nje. Hili limejidhihirisha wazi kwa ukweli kwamba Tanzania imeshuka nafasi 12 (Kumi na mbili) ndani ya miaka mitatu kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ya nafasi ya Urahisi wa Kufanya Biashara”, na uwekezaji wa moja kwa moja wa nje umeshuka kutoka asilimia 3.9 (Tatu nukta tisa) ya pato la taifa kwa mwaka 2016 (Elfu mbili na kumi na sita) hadi asilimia 2.3 (Mbili nukta tatu) mwaka 2017(Elfu mbili na kumi na saba.

Tunaelewa kwamba serikali ya Tanzania inataka kuvutia na kukuza uwekezaji, lakini ili kufanikiwa na kuendelea kuwekeza, ni lazima itengeneze mazingira ya biashara ya kujenga uaminifu kwa pande zote kati ya serikali na sekta binafsi.

Kuongeza Thamani Kwa Biashara za Kimarekani.
Biashara za kimarekani zina sifa ya kipekee ya kuleta ubunifu mpya na teknolojia katika biashara zao. Utamaduni wetu wa biashara unajivunia katika kujenga wafanyakazi wa ndani waliofundishwa vizuri na kuimarisha jamii kupitia jukumu la kusaidia jamii. Tunaunga mkono mazingira ya biashara yenye kiwango cha juu cha maadili yanayozuia rushwa kisheria. Utamaduni huu wa biashara unahimiza uwazi na kutengeneza fursa kubwa za kibiashara kwa wote.

Serikali ya Marekani ambayo ni mfadhili mkubwa wa maendeleo wa Tanzania, inaunga mkono ushirikishwaji wa sekta binafsi Tanzania kupitia ushirikiano wa sekta binafsi na za umma ambao unachochea mazingira imara na ubunifu. Watu wa Tanzania wananufaika kutokana na sekta binafsi imara ambayo inahimizwa kuwekeza kwenye nguvukazi.

Nitaishia hapa, kwa kuwa tuko hapa katika majadiliano, nanyi hamko hapa leo kunisikiliza mimi tu. Mjadala huu leo wa na serikali ya Tanzania ni mwanzo wa kile tunachotumaini kuwa ushirikishwaji zaidi. Na muhimu zaidi tunataka mazungumzo ya leo yalete matokeo muhimu ya kudumu. Tunatazamia kuendelea na ushirikiano na serikali ya Tanzania katika kutekeleza mabadiliko ya msingi ili yaweze kusaidia biashara za kimarekani na pia kutatua changamoto zao.

Asanteni kwa kunisikiliza.