Kaimu Balozi Dk. Inmi Patterson azuru Moshi na Arusha

Kuanzia tarehe 28 Februari hadi 2 Machi, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk. Inmi Patterson alifanya ziara huko Moshi, Monduli na Arusha nchini Tanzania kutembelea na kukuza uelewa wa wananchi kuhusu jitihada zinazofanywa na Marekani katika kujenga uwezo wa wanafunzi wa Kitanzania, kuboresha huduma za afya na kulinda maliasili na wanyamapori.

Akiwa katika Shule ya Orkeeswa inayohudumia jamii wa Wamaasai huko Monduli, Kaimu Balozi Patterson alikabidhi mipira 24 iliyotolewa na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike kama zawadi kwa vijana wa Kitanzania. “Michezo inatufundisha umuhimu wa kutenda haki (fair play) na kuheshimiana.  Mafunzo tunayoyapata katika michezo tunaweza kuyatumia moja kwa moja katika mahusiano katika jamii tunazoishi na kwingineko,” alisema Dk. Patterson alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo.

Katika ziara yake katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, Dk. Patterson aliweza pia kukutana na wanafunzi wanaoshiriki katika programu maalumu ya mafunzo ya Kiingereza inayofadhiliwa na Ubalozi wa Marekani iitwayo  English language ACCESS Micro-scholarship program, viongozi waandamizi wa hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Center (KCMC) ikiwa ni pamoja mtaalamu wa Kimarekani anayefanya kazi hospitalini hapo chini ya mpango wa Fulbright unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani. Aidha, katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Wanyamapori, Kaimu Balozi, akiwa katika jiji la Arusha, alishiriki katika onyesho maalumu la filamu yenye matukio halisia iitwayo The Ivory Game inayoangazia jitihada za kukabiliana na ujangili zinazofanywa nchini Tanzania na duniani kote. Onyesho hilo lilihudhuriwa na wanafunzi na wahitimu wa programu mbalimbali za mafunzo na mabadilishano zinazofadhiliwa na serikali ya Marekani wapatao 120.

Picha za ziara hiyo zinazoweza kutumiwa na vyombo vya habari, kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam, zinapatikana katika tovuti: https://flic.kr/s/aHskxhADsf

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe:  DPO@state.gov