Kaimu Balozi Inmi Patterson Afanya Ziara Mkoani Mbeya

Dar es Salaam, TANZANIA. Kutoka tarehe 17 hadi 19 Oktoba, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk. Inmi Patterson alifanya ziara mkoani Mbeya kwa lengo la kukuza uelewa wa wananchi kuhusu jitihada zinazofanywa na Marekani katika kujenga uwezo wa Watanzania katika kujenga jamii zenye afya na elimu, kukuza uchumi wa jamii na mkoa na kusaidia usimamizi bora wa maliasili.

“Serikali ya Marekani ina fahari kufanya kazi na Watanzania, ikiunga mkono na kusaidia jitihada za wananchi wenyewe za kujenga Tanzania yenye amani, ustawi, usalama na afya,”alisema Kaimu Balozi Patterson akiwa ziarani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ambako programu kadhaa za kiafya zinazofadhiliwa na Serikali ya Marekani zinasaidia kupunguza janga la VVU/UKIMWI katika Nyanda za Juu za Tanzania. “Uhusiano wetu mkubwa unaakisiwa na ushirikiano wa kina baina ya nchi zetu mbili. Kwa zaidi ya nusu karne, tumefanya kazi pamoja kama marafiki, wabia, na washirika, na ninaimani kuwa safari yetu ya pamoja itaendelea.”

Ukiwa mkoa muhimu katika ushirikiano kati ya Serikali ya Marekani na Tanzania, Mbeya ni mwenyeji wa miradi kadhaa ya uwekezaji ya sekta binafsi ya Marekani pamoja na programu mbalimbali za mafunzo na misaada ya maendeleo zinazofadhiliwa na Serikali ya Marekani, hii ni pamoja na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI, Miradi inayoendeshwa na Shirika la Kimarekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) pamoja na Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps. Ushirikiano wa maendeleo na wabia wa Kitanzania ni sehemu ya uwekezaji mkubwa na ushirikiano kati ya serikali ya Marekani na watu wa Tanzania.

Picha kuhusu ziara hizo kwa matumizi ya vyombo vya habari, kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam,  zinaweza kupatikana mtandaoni kwa kupitia anuani: https://flic.kr/s/aHsm4QqxfY

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.