Kaimu Balozi Inmi Patterson Atembelea Kigoma

Dar es Salaam, TANZANIA. Kutoka tarehe 4 hadi 6 Disemba Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Inmi Patterson alifanya ziara Mkoani Kigoma, Tanzania ambapo aliungana na ujumbe wa Kimataifa ulioongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Idadi ya Watu, Wakimbizi na Uhamiaji Mark Storella na ujumbe wa serikali ya Tanzania kuzindua rasmi kituo kipya kitakachotumika kuwashughulikia wakimbizi watakaokuwa katika mpango wa kupelekwa nchi ya tatu.

“Ninafahari kwa kile ambacho nchi yangu imefanya katika kuwasaidia watu wanaokimbia migogoro na machafuko katika eneo la Afrika Mashariki,” alisema Naibu Waziri Storella Wakati wa sherehe za kukata utepe kuzindua kituo hicho.  “Katika miaka mitano iliyopita Marekani imewachukua zaidi ya wakimbizi 40,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikiwa ni pamoja na wakimbizi 11,000 waliokuwa wakitokea Tanzania.  Jitihada hizi zimemewawezesha maelfu ya wakimbizi kuwa na mwanzo na fursa mpya.”

Ikiwa ni nchi inayoongoza duniani kwa kupokea wakimbizi duniani, Marekani imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 4.5 katika kituo cha kisasa kabisa cha kuwashughulikia wakimbizi katika kijiji cha Makere, mkoani Kigoma ambacho kitashughulikia taratibu zote zinazotakiwa kuwawezesha wakimbizi kutoka Kongo wanaokidhi matakwa ya kuhamishiwa nchi nyingine (resettlement) kupata uhamisho huo pamoja na kushughulikia masuala ya ulinzi na matibabu kwa wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu.  Marekani inazihamasisha nchi nyingine ambazo zipo tayari kuwapokea wakimbizi hawa kukitumia kituo hiki kupanua programu zao za kupokea wakimbizi kutoka kanda hii.  Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) ndilo litakalosimamia kituo cha Makere ambapo wabia mbalimbali kwa miaka kadhaa ijayo wanaweza kuendesha shughuli za kuwahudumia wakimbizi wanaotarajiwa kuhamishiwa katika nchi nyingine kwa ufanisi mkubwa na gharama nafuu zaidi.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe:  DPO@state.gov.