Dar es Salaam, TANZANIA. Hivi karibuni, Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Michael Battle, na Kamanda wa Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani, Jenerali Michael Langley, waliongoza hafla ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa pamoja wa ujenzi katika Chuo cha Intelijensia ya Kijeshi cha Tanzania jijini Dar es Salaam. Jiwe hili la msingi liliweka katika eneo la ujenzi wa mradi wa pamoja kati ya Marekani na Tanzania wenye thamani ya Shilingi bilioni 3.8 ukilenga kujenga makazi kwa ajili ya wakufunzi na wanafunzi wa chuo cha hicho cha intelijensia. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na makamanda wa Chuo cha Ulinzi na Intelijensia cha Tanzania, Meja Jenerali Wilbert Ibuge na Brigedia Jeneral Furahisha Ntahena.
Wakati Tanzania ikiendelea kuwa mbia wa kimkakati wa Marekani na washirika wake wa kikanda, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kung’aa kama mlinzi wa amani na usalama katika kanda. Ikisaidia ulinzi wa amani katika Jamhuri wa Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ushiriki unaoongezeka wa Tanzania katika ulinzi wa amani unahitaji kada ya inteligensia ya kijeshi yenye weledi na uwezo mkubwa. Chuo cha Intelijensia ya Kijeshi Tanzania ni shule intelijensia ya kimkakati yenye hadhi ya juu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Chuo hiki kimekuwa kikipata msaada wa kiulinzi wa Marekani toka kilipoanzishwa mwaka 2014.
Mbali na kusaidia ujenzi wa jengo kuu la utawala na ukumbi wa mihadhara, Jeshi la Marekani, Kikosi Kazi za Kusini mwa Ulaya – Afrika, litasaidia pia miradi ya mafunzo na ya kujenga uwezo wa kitaasisi itakayogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 3.1 katika miaka miwili ijayo, hivyo kufanya uwekezaji wa Marekani katika chuo hicho kufika takriban Shilingi bilioni 16.3. Hafla hii ni kielelezo cha kuendelea kwa ushirikiano rasmi wa kijeshi baina ya nchi hizi, ikiwa ni nyongeza katika zaidi ya shilingi bilioni 7.5 zinazotolewa kila mwaka kwa ajili ya mafunzo, vifaa na misaada mingine. Ujenzi kamili wa majengo hayo unatarajiwa kuanza mwaka 2024.