Kituo Kipya Cha Kimarekani Katika Makutano Ya Elimu Na Ubunifu

Dar es Salaam (29 Septemba) – Kaimu Balozi katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam Dk. Inmi Patterson na Naibu Waziri wa Elimu na Sayansi naTeknolojia, Mhandisi Stella Manyanya wamezindua rasmi Kituo Kipya cha Kimarekani kilichoanzishwa kwa ubia na Maktaba Kuu jijini. Akiungana na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Maktaba nchini Dk. Alli Mcharazo, Kaimu Balozi Patterson alipongeza kuzinduliwa kwa kituo hiki akikielezea kuwa mfano wa ushirikiano wa maendeleo kati ya Marekani na Tanzania akibainisha kuwa programu mbalimbali zitafanyika kituoni hapo.

“Kituo kitakuwa kiunganishi cha kidijitali kati ya Tanzania na eneo la Silicon Valley (kitovu cha uvumbuzi na ubunifu wa teknolojia), TEHAMA, na ubunifu. Aidha, kituo kitakuwa daraja la kuzifikia taasisi za elimu ya juu za Kimarekani, taasisi za utafiti za Marekani na hata ufadhili wa masomo. Kituo kitashirikisha hulka ya ubunifu na ujasiriamali Watanzania ambao watabuni mstakabali mpya,” alisema Kaimu Balozi Patterson.

Vikiwa vimeanzishwa kwa ushirikiano na Serikali ya Marekani, vituo vya Kimarekani ni maeneo yaliyotengwa maalumu katika taasisi mbalimbali za humu nchini yanayolenga kukuza fikra yakinifu na mijadala ya kina kuhusu masuala mbalimbali kwa kuwapa wananchi haki ya kupata elimu na kuwapa taarifa bila vikwazo. Ni maeneo ambapo watu wanaweza kutafiti na kutiwa hamasa na mawazo, ujuzi na fursa mpya zenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya.

Kikiwa na huduma ya kuunganishwa na mtandao kupitia njia ya Wi-Fi, huduma za kompyuta, printa maalum ya 3-d na nyingi nyinginezo, Kituo cha Kimarekani katika Maktaba Kuu kipo wazi kutumiwa na wananchi wote bila malipo yoyote na kitakuwa wazi kwa umma kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni kwa siku za Jumatatu hadi Ijumaa na kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nane adhuhuri kwa siku za Jumamosi.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.