Kujenga uwezo wa usimamizi na kukabili mabadiliko ya Kimazingira na Maliasili katika Afrika Mashariki

Arusha, 2 Machi 2018: Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ushirikiano na Tume ya Bonde la Ziwa Viktoria (Lake Victoria Basin Commission – LVBC) na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), waliendesha kongamano la kikanda la mafunzo na mkutano uliowajumuisha wawekezaji na wafadhili wa usimamizi wa mazingira na maliasili uliokuwa na mada isemayo: Kujenga Uwezo wa Kukabiliana na Kuhimili Mabadiliko katika Afrika Mashariki: Kuziba pengo lililopo kati ya Sera na Utendaji.  (Building Resilience in East Africa: Bridging the Gaps in Policy & Practice.

Matukio haya yaliipa fursa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuonyesha miradi yake ya kipaumbele katika usimamizi wa mazingira na maliasili ikiwa ni pamoja na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi; uhifadhi wa bayoanuai; maji, usafi wa mazingira, na usimamizi wa pamoja wa nchi za EAC wa rasilimali maji. Mafunzo na kongamano hili liliwakutanisha watendaji wa kikanda na kitaifa katika sekta husika, watengeneza sera, watafiti, wawakilishi wa asasi zisizo za kiserikali, mashirika ya kimataifa, mashirika ya kikanda, sekta binafsi na wabia wa maendeleo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki. Washiriki walijadili mada hizi kwa lengo kuchagiza kuchukuliwa kwa hatua mahsusi zitakazoweza kuleta mabadiliko chanya kwa ekolojia na jamii zilizo katika hatari zaidi ya kuathiriwa.

“Serikali ya Marekani, kwa kupitia USAID inalenga kusaidia usimamizi endelevu wa utajiri mkubwa wa maliasili zilizopo katika eneo hili kama nyenzo za kusukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi na hivyo kuleta maendeleo endelevu. Dhamira yetu ya pamoja ya kuhakikisha usimamizi mzuri wa maliasili ni muhimu sana,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mazingira ya USAID ya Kenya na Afrika Mashariki Brad Arsenault Wakati wa kongamano hili.

Kupitia programu mbalimbali za USAID kama ile ya kukabiliana na athari za tabia nchi kupitia sera, kujenga uweza wa kupokea mabadiliko, utafiti na kuinua maendeleo ya kiuchumi katika nchi za Afrika Mashariki (Planning for Resilience in East Africa through Policy, Adaptation, Research and Economic Development – PREPARED), serikali ya Marekani inalenga kuimarisha uwezo wa kuifundi wa taasisi za kikanda, kuimarisha uongozi wa kisera na utayari wa kuchukua hatua katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Aidha, programu hii inakusudia kuimarisha usimamizi endelevu wa ekolojia muhimu za kibaiolojia zinazohusisha nchi zaidi ya moja pamoja na usimamizi wa utoaji huduma za maji, majitaka na usafi wa mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria.

Kongamano lililenga pia kuunganisha jitihada zinazofanyika katika jamii na zile zinazofanyika katika ngazi za kitaifa na kikanda ili kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

##

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe:  DPO@state.gov.

USAID:
Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ni taasisi ya maendeleo ya kimataifa ya Serikali ya Marekani inayofanya kazi kwa ushirikiano na serikali, mashirika na hata sekta binafsi katika nchi za Afrika Mashariki ili kuondoa umasikini uliokithiri, kujenga jamii imara na za kidemokrasia huku tukiendeleza malengo ya pamoja ya kuimarisha usalama na ustawi.

PREPARED (ambayo kirefu chake ni Planning for Resilience in East Africa through Policy, Adaptation, Research and Economic Development),  ni programu ya miaka mitano inayotekelezwa na taasisi mbalimbali ikiwa na  malengo ya kuimarisha uwezo wa nchi za kanda katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kukuza maendeleo endelevu ya kiuchumi, kusimamia ekolojia zinazovuka mipaka ya kitaifa  (trans-boundary ecosystems) na kuimarisha jamii.

KUHUSU PROGRAMU YA PREPARED:
Programu ya PREPARED inatekeleza na wabia sita wa kikanda, ikiwa ni pamoja na  Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Tume ya Bonde la Ziwa Viktoria (LVBC) Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Pembe ya Afrika (IGAD), Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha Kimataifa (ICPAC), Mtandao wa kimataifa wa kutoa mapema tahadhari kuhusu majanga ya ukame na njaa (Famine Early Warning Systems Network – FEWSNET), Kituo cha Kikanda cha Uainishaji Rasilimali kwa Maendeleo (Regional Centre for Mapping of Resources for Development – RCMRD) na taasisi ya ushauri wa kisayansi katika masuala ya Mazingira ya Tetra Tech ARD. Programu hii inalenga pia kuingiza masuala yanayohusu uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi katika uandaaji wa mipango ya maendeleo na utekelezaji wake na katika ajenda za maendeleo za kikanda na kitaifa.

###