Kongamano la Maziwa Makuu hadi Maziwa Makuu lazinduliwa

Kongamano la Maziwa Makuu hadi Maziwa Makuu lazinduliwa
Kongamano la Maziwa Makuu hadi Maziwa Makuu lazinduliwa

Mwakilishi Maalumu wa Marekani kwa Nchi za Maziwa Makuu na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Russel Feingold kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uendelezaji Ziwa Tanganyika, wiki hii amezindua kongamano maalumu linalowakutanisha wataalamu kutoka eneo la Maziwa Makuu ya Amerika ya Kaskazini na wale wa Maziwa Makuu ya Afrika ili kujadili suala la usimamizi endelevu wa maeneo ya maji yanayochangiwa na nchi kadhaa (transboundary waters). Kwa pamoja maeneo ya maziwa makuu ya Amerika Kaskazini na yale ya Afrika yanajumuisha zaidi ya nusu ya rasilimali ya maji yasiyo na chumvi duniani.

Kwa siku tatu wakiwa mjini Kigoma katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, wanasayansi, wasomi na watunga sera kutoka Marekani na Canada watakuwa na majadiliano ya kina na wenzao kutoka katika nchi za ukanda wa maziwa makuu, hususan zile zinazozunguka ziwa Tanganyika ikiwa ni pamoja na Burundi, DRC, Rwanda, Tanzania, and Zambia. ‎

Kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa katika kongamano hili na majadiliano yatakayotokana na mada hizo, washiriki wataangazia changamoto zinazokabili usimamizi wa maziwa makuu ya Amerika Kaskazini na maziwa makuu ya Afrika ambazo ni pamoja na:

  • vitisho kwa shughuli za uvuvi‎;
  • mwani wenye sumu na magugu maji haribifu;
  • kuingia kwa aina ya wanyama na mimea haribifu na isiyo ya asili katika mito na maziwa; na
  • Mabadiliko ya tabia nchi.

Mwakilishi Maalumu Feingold alisema kuwa, “Kongamono hili adhimu ni mojawapo ya mifano ya manufaa makubwa yanayotokana na kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya nchi za ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika. Hali kadhalika ni fursa adimu na ya kipekee ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu mbinu zetu za kushughulikia masuala kuhusu mazingira.”

Kwa pamoja washiriki wa kongamano hili walibainisha maeneo ya kupewa kipaumbele katika ushirikiano baina ya pande hizi mbili katika siku zijazo. Inatarajiwa kuwa makongamano yajayo  ya “Maziwa Makuu hadi Maziwa Makuu “ yataangazia maeneo hayo pamoja na maziwa mengine makuu ya Afrika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano, Meneja wa Maziwa Makuu katika Idara ya Uhifadhi wa Mazingira ya Marekani, Susan Hedman, alibainisha ukubwa wa changamoto za usimamizi wa rasilimali katika maziwa makuu ya Amerika ya Kaskazini na yale ya  Afrika ambayo yanabeba karibu nusu ya rasilimali yote ya maji matamu (yasiyo na chumvi) ya dunia.

Hapo mwanzoni mwa mwaka 2012 nchi za Burundi, DRC, Rwanda, Tanzania, na Zambia zilipitisha mkakati na mpango wa utekelezaji wa pamoja wa kulinda bayoanuai na uendelezaji endelevu wa maliasili katika bonde la Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika ndio ziwa kubwa Zaidi miongoni mwa maziwa yaliyo katika ukanda huu wa Afrika.  Baadaye mwaka huo huo, Marekani na Canada ziliboresha makubaliano yao kuhusu Ubora wa Maji katika Maziwa Makuu. Makubaliano hayo ndiyo yamekuwa yakiongoza usimamizi wa pamoja wa Maziwa Makuu ya Amerika ya Kaskazini toka mwaka 1972.‎

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji Ziwa Tanganyika, Jean-Marie Nibirantije alisisitizia umuhimu wa kukabiliana kikamilifu na vitisho vyovyote dhidi ya bayoanuai na matumizi endelevu ya maliasili na rasilimali za ziwa: “Majadiliano na wataalamu kutoka Maziwa Makuu ya Amerika ya Kaskazini yametuwezesha kuelewa kuwa mengi ya matatizo tunayokabiliana nayo yanafanana. Kongamano hili limetupa tumaini jipya la kuwa na ushirikiano endelevu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.”