Marekani Kuendelea Kusaidia Watu Wa Tanzania Kukabiliana Na VVU/Ukimwi

Dar es Salaam, TANZANIA.  Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR), umeidhinisha mpango wa kutoa Dola za Kimarekani Milioni 526 katika kipindi cha mwaka mmoja ujao kwa ajili ya kukabiliana na VVU/UKIMWI nchini Tanzania. Msaada huu utaongeza idadi ya Watanzania wanaopatiwa matibabu ya kufubaza VVU kufikia milioni 1.2 na utaimarisha mapambano dhidi ya VVU kupitia huduma za upimaji, matibabu, kufubaza (viral suppression) na kuzuia maambukizi ili hatimaye kufikia lengo la kuutokomeza kabisa UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Fedha hizo zitafadhili miradi mbalimbali inayotekelezwa chini Mpango wa Utekelezaji wa  PEPFAR Nchini utakaoanza kutekelezwa Mwezi Oktoba 2017 hadi Septemba 2018, na ni ongezeko la asilimia 12.3 ya bajeti ya mwaka jana.  Chini ya mpango huu mpya, PEPFAR itafanya kazi na Serikali ya Tanzania na wabia wake kadhaa kutoa huduma ya upimaji wa VVU kwa Watanzania milioni 8.6 na kutoa matibabu ya kufubaza VVU kwa watu 360,000 watakaobainika kuwa wameambukizwa virusi hivyo kufanya idadi ya Watanzania watakaokuwa wakipata matibabu hayo kufikia milioni 1.2.  Bajeti iliyotengwa inajumuisha pia utoaji wa huduma na matibabu kwa watoto yatima na wale walio katika mazingira hatarishi pamoja na kukabiliana na ukatili wa kijinsia.  Hali kadhalika, katika kuimarisha jitihada za kuzuia maambukizi mapya ya VVU, PEPFAR itasaidia mpango wa tohara ya hiari kwa wanaume (VMMC) ambapo wanaume 890,000 watapatiwa huduma hiyo.

Mpango huu unaendeleza ubia wa muda mrefu kati ya Marekani na Tanzania katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na muongo mmoja wa ushirikiano uliowezesha kudhibiti kwa mafanikio makubwa maambukizi ya VVU na kufanyakazi tukilenga katika kuwa na Kizazi kisicho na UKIMWI. Akitoa maoni yake kuhusu mpango huu ulioidhinishwa, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Virginia Blaser alisema “Kwa niaba ya Watu wa Marekani tuna furaha kubwa kuendelea kuwasaidia watu wa Tanzania na kuendeleza ubia uliopo baina yetu. Kwa pamoja tunafanya kazi ili hatimaye kuwa na Kizazi Kisicho na UKIMWI Tanzania – ambacho hakuna hata mtu mmoja anayeachwa nyuma.”

Wadau na wabia wa PEPFAR walioshiriki katika uandaaji wa mpango huu na watakaoshiriki katika utekelezaji wake ni pamoja na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Programu ya Pamoja ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti VVU/UKIMWI (UNAIDS), Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na Kifua Kikuu, UKIMWI na Malaria (GFTAM), Shirika la Afya Duniani (WHO), Taasisi ya Bill na Melinda Gates, Taasisi ya Benjamin Mkapa ya kukabiliana na VVU/UKIMWI (BMAF) na Mtandao wa Kitaifa wa Wanawake wanaoishi na VVU/UKIMWI (NETWO+).

Kwa taarifa zaidi kuhusu PEPFAR nchini Tanzania tafadhali tembelea tovuti ya Ubalozi wa Marekani https://tz.usembassy.gov/our-relationship/pepfar/.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.