Marekani na Serikali ya Tanzania wazindua Baraza la Taifa la Ushauri la Maendeleo ya Vijana

Iringa, Tanzania – Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk. Inmi Patterson, na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mheshimiwa Anthony Mavunde, leo wamezindua Baraza la Taifa la Ushauri la Maendeleo ya Vijana ambacho ni chombo cha ushauri kinachoongozwa na vijana wenyewe kilichoanzishwa na Kitengo cha Kuwaendeleza Vijana cha Mpango wa Feed the Future Tanzania. Mpango huu unafadhiliwa na Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

Ukitekelezwa katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Zanzibar, mpango huu umebuniwa ili kuwahimiza vijana wa vijijini kujihusisha katika sekta ya kilimo ya Tanzania na kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana wa kuanzia umri wa miaka 15 -35 huku ukiwahimiza vijana hao kufuata mifumo ya maisha itakayowawezesha kuwa na afya nje.

Katika hotuba yake, Kaimu Balozi Patterson alisema kuwa vijana wanaoshiriki katika mpango huu “tayari wametambua faida kubwa ambazo vijana wanaweza kuzipata kwa kuanzisha biashara zao wenyewe zinayohusiana na kilimo, kuanzisha bidhaa mpya na za kibunifu au kutatua changamoto zinazokabili jamii zao.”

Baraza hili la Kitaifa litakuwa ndio mshauri mkuu wa mpango wa Feed the Future Tanzania wa Maendeleo ya Vijana – ukiuhabarisha na kuushauri mpango huu kuhakikisha kuwa shughuli zake zote zinazingatia mahitaji na kukidhi maslahi ya vijana na kwamba zinatatua changamoto halisi zinazowakabili vijana wa vijijini nchini Tanzania.