Marekani na Tanzania waadhimisha miaka 15 ya ushirikiano katika kupambana na VVU/UKIMWI

KAMPENI YA #PEPFAR15

Dar es Salaam, TANZANIA. Jumatano, tarehe 30 Mei, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Inmi K. Patterson na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhesimiwa Kassim Majaliwa walizindua rasmi kampeni ya maadhimisho ya miaka 15 ya ubia kati ya Marekani na Tanzania katika kupambana na janga la VVU/UKIMWI chini ya Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR).  Katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Kaimu Balozi alitangaza pia kuwa hivi karibuni PEPFAR imevuka lengo muhimu katika utoaji huduma hapa nchini ambapo hivi sasa inatoa matibabu yanayookoa maisha kwa zaidi ya Watanzania milioni moja wanaoishi na VVU. Toka kuzinduliwa kwa PEPFAR na Rais George W. Bush hapo mwaka 2003, Serikali ya Marekani imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 4.5 (takriban Shilingi trillion 10.26) katika kudhibiti maambukizi ya VVU/UKIMWI nchini Tanzania.

Kampeni mpya ya #PEPFAR15 itaendelea kwa mwaka wote wa 2018 ili kuadhimisha mafanikio yaliyofikiwa na nchi zetu mbili katika mapambano dhidi ya VVU na kuendelea kuchukua hatua stahili za kudhibiti kuenea kwa VVU nchini Tanzania.  Ili kudhibiti janga hili, ni muhimu sana kwa Watanzania wote wanaoishi na VVU kupima na kujua hali za afya zao na kisha kuanza matibabu yatakayookoa maisha yao.  Katika kufikia azma hiyo, kampeni ya #PEPFAR15 inalenga kupunguza unyanyapaa, kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma zitolewazo za kukabiliana na VVU. Kila mtu atakayepimwa na kugundulika kuwa na maambukizi ya VVU ataanzishiwa matibabu mara moja. Watu wengi walio katika matibabu haya huwa na kiasi kidogo sana cha virusi hivi kiasi kwamba ni vigumu kwao kuwaambukiza wengine, ikiwemo wenza na watoto wao.

“Wakati wa kampeni hii, tutafanya kazi nanyi nyote, pamoja na watu wanaoishi na VVU nchini kote Tanzania ili kusimulia hadithi na habari nzuri (positive stories): habari za watu wanaoishi na VVU ambao wakati mmoja walikuwa dhaifu na wagonjwa lakini sasa wakiwa wenye nguvu na afya, habari za watu waliopima mapema na kuanza matibabu hata kabla hawajaanza kuumwa, habari za watu wanaoishi na VVU walioanza matibabu ya kuokoa maisha ili pia kuwalinda wenza wao na habari za akina mama wanaoishi na VVU wanaopata matibabu ili kuwalinda watoto wao,” alisema Kaimu Balozi Inmi Patterson.

Kwa taarifa zaidi kuhusu PEPFAR nchini Tanzania, tafadhali tembelea tovuti ya Ubalozi wa Marekani: https://tz.usembassy.gov/our-relationship/pepfar/.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe:  DPO@state.gov.

 

Taarifa kuhusu Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) nchini Tanzania

Muhtasari: PEPFAR ni mpango maalumu wa Serikali ya Marekani wa kusaidia kuokoa maisha ya watu wanaoishi na VVU/UKIMWI duniani kote.  Mpango huu wa kihistoria ni mkubwa zaidi ya mpango wowote uliowahi kuendeshwa na nchi yoyote duniani katika kukabili ugonjwa mmoja kimataifa.  Mpango wa PEPFAR huongozwa na kuendeshwa na majukumu ya pamoja kati ya nchi wafadhili na nchi wabia na wadau wengine katika kuokoa maisha.

Kupitia PEPFAR, Marekani imesaidia dunia kuwa salama zaidi kwa kupunguza vitisho vya magonjwa ya kuambukiza.  Awali mpango huu ulibuniwa ili kutoa huduma za kuokoa maisha katika nchi zilizokuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU/UKIMWI, hata hivyo hivi sasa PEPFAR inalenga kudhibiti kuenea kwa VVU/UKIMWI duniani kote.  Mpango huu unajumuisha miradi ya Serikali ya Marekani inayolenga afya, maendeleo, usalama na diplomasia ukiwa na uwezo mkubwa wa kufikia malengo na matokeo yaliyo wazi, yanayopimika na yanayobadilisha maisha.

Taarifa na takwimu muhimu kuhusu matokeo ya mpango huu:

  • Katika mwaka wa fedha 2017 pekee, PEPFAR iliwezesha upimaji wa VVU kwa Watanzania milioni 9.
  • PEPFAR iliwezesha Watanzania 950,000 kupata matibabu ya kufubaza VVU (antiretroviral treatment); Lengo : Kuwawezesha Watanzania milioni 1 kupata matibabu hayo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2018
  • Katika mwaka wa fedha 2017, PEPFAR ilitoa matibabu ya kuokoa maisha kwa akina mama wajawazito wapatao 56,000 ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

 

Miaka 15 toka kuanzishwa kwa PEPFAR hapo mwaka 2003:

  • Vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 70, kutoka vifo 110,000 mwaka 2003 hadi 33,000 mwaka 2016
  • Kiwango cha maambukizi mapya kwa mwaka kimeshuka kwa zaidi ya nusu, kutoka maambukizi mapya 100,000 mwaka 2003 hadi 55,000 mwaka 2016
  • Programu za kudhibiti VVU nchini Tanzania zimezuia maambukizi mapya milioni 1.1 na vifo 690,000

 

Mchango wa PEPFAR wa miaka 15 kwa Watanzania unaakisi uhusiano wetu imara na wa muda mrefu na Watu wa Tanzania:

  • Kupitia PEPFAR, Serikali ya Marekani imetumia takriban Shilingi bilioni 9 (Dola za Kimarekani bilioni 4)
  • Fedha zilizotengwa kwa ajili yam waka wa fedha 2018 ni zaidi ya Shilingi trilioni 1 (Dola za Kimarekani milioni 512)
  • Hivi sasa PEPFAR inatoa asilimia 80.0 ya fedha zote zinazogharamia programu za kukabiliana na VVU nchini Tanzania.
  • PEPFAR inatoa asilimia 68.0 ya fedha za kugharimia ARVs na asilimia 81.3 vipimo vya kupimia VVU ( rapid test kits.)