Marekani na Tanzania Waadhimisha miaka 20 ya Taasisi ya Utafiti wa Walter Reed nchini Tanzania

Dar es Salaam, TANZANIA. Ijumaa, tarehe 6 Desemba, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Inmi Patterson na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bw. Juma Homera, waliadhimisha miaka 20 ya kuwepo kwa Taasisi ya Utafiti ya Jeshi la Marekani ya (WRAIR) nchini Tanzania katika hafla maalumu iliyofanyika mjini Mpanda, mkoa wa Katavi, ijumaa tarehe 6 Desemba. Kama sehemu ya maadhimisho hayo, Kaimu Balozi Patterson alizindua maabara iliyofadhiliwa na Serikali ya Marekani itakayoimarisha uwezo wa mfumo wa afya Mkoani Katavi kuchunguza maradhi.

“Wakati Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR na Serikali ya Tanzania walipoanza kufanya kazi pamoja, Watanzania wapatao 110,000 walikuwa wakipoteza Maisha kila mwaka kutokana na janga la UKIMWI. Mwaka 2004 pungufu ya Watanzania 1000 wanaoishi na VVU walikuwa wakipokea matibabu yanayookoa maisha kwa  kufubaza VVU. “Bila juhudi zetu hizi za pamoja, janga la UKIMWI lingekuwa linaendelea kumaliza watu mijini, vijijini na katika familia nchini kote. Lakini leo, Serikali ya Marekani inawasaidia zaidi ya watu milioni 1.2 wanaoishi na VVU kupata matibabu ya kufubaza virusi hivyo na hivyo kuokoa maisha yao,” alisema Kaimu Balozi Patterson.

Ikiwa sehemu ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI, taasisi ya Walter Reed husimamia na kuendesha programu ya kina ya kuzuia maambukizi ya VVU pamoja na matibabu na matunzo (prevention, care and treatment) kupitia mfumo uliopo wa utoaji huduma za afya katika mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini, na katika hospitali na vituo vya afya vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Taasisi ya Walter Reed inatoa matibabu ya kufubaza VVU kwa zaidi ya Watanzania 235,000, hali kadhalika inajihusisha na utafiti wa kimatibabu wa maradhi ya UKIMWI, Ebola, Malaria, Mafua na Kifua Kikuu ili kuokoa maisha ya Watanzania.