Flag

An official website of the United States government

Marekani na Tanzania zaadhimisha miaka 20 ya PEPFAR na mafanikio ya katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI
5 MINUTE READ
Febuari 3, 2023

Dar es Salaam – Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya mafanikio katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI yaliyowezeshwa na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI, au PEPFAR.

Nchini Tanzania, toka mwaka 2003, PEPFAR imesaidia kupunguza vifo vinavyotokana na UKIMWI kwa takriban asilimia 80 na kupunguza maambukizi mapya kwa karibu asilimia 60. Wakati programu hii ilipokuwa ikianza, pungufu ya watu 1,000 nchini Tanzania walikuwa wakipata dawa za kufubaza VVU. Leo hii, zaidi ya Watanzania milioni 1.5 wanapokea matibabu haya yanayookoa maisha.

Toka kuanzishwa kwa PEPFAR hapo mwaka 2003, chini ya utawala wa Rais George W. Bush, serikali ya Marekani imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 100 katika kupambana na VVU/UKIMWI duniani kote, ikijumuisha takriban Dola za Kimarekani bilioni 7 zilizotolewa kwa Tanzania. Kiwango hiki cha uwekezaji ni kikubwa zaidi kuwahi kufanywa na nchi yoyote katika kukabiliana na ugonjwa wa aina moja katika historia ya mwanadamu.

Katika hotuba yake, Naibu Balozi wa Ubalozi wa Marekani nchini, Robert Raines alisema hafla hii ilikuwa ni fursa ya kusherehekea ushirikiano imara kati ya Marekani na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

“Leo, tuna fursa adhimu ya kuadhimisha miaka 20 ya kujitoa kwa dhati kwa PEPFAR katika kukabiliana na athari za VVU na safari muhimu iliyotufikisha hapa hivi leo. Mafanikio yetu yasingewezekana bila ushirikiano imara na wa karibu na serikali ya Tanzania.”

Wageni wengine waliohudhuria hafla hiyo walikuwa ni pamoja na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel, Mwakilishi wa Kiongozi wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA) Agnes Nyoni na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko. Aidha, hafla hii ilihudhuriwa pia na viongozi wa taasisi nne za Kimarekani zinazotekeleza miradi ya PEPFAR nchini Tanzania. Taasisi hizo ni Shirika la Marekani la Ushirikiano wa Kimataifa (USAID), Kituo cha Marekani cha Udhibiti wa Maradhi (CDC), Taasisi ya Utafiti wa Kijeshi ya Walter Reed na Shirika la Wafanyakazi wa Kujitolea la Peace Corps. Kwa ujumla zaidi ya wageni 300 kutoka sekta ya afya walihudhuria hafla hii.

Ili kuonyesha matokeo ya programu za PEPFAR katika maisha ya watu, hafla hii iliambatana na tamasha la filamu fupi kadhaa zilizoandaliwa na kuongozwa na watengeneza filamu wa Kitanzania.

Japokuwa hafla hii ililenga kuadhimisha mafanikio ya programu ya PEPFAR, washiriki walitoa wito kwa jumuiya ya watoa huduma za afya kutokulegeza kamba kutokana na mafanikio haya.

“Bado kuna kazi kubwa mbele yetu ya kukamilisha ngwe ya kulidhibiti kabisa janga hili nchini Tanzania.  Jitihada zaidi zielekezwe katika kupunguza pengo la usawa lililopo katika utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wasichana, wanawake vijana, Watoto na makundi ya jamii yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa VVU,” aliasa Mkurugenzi Mkazi wa PEPFAR nchini Tanzania Jessica Greene.