Marekani na Tanzania Zashirikiana kukabiliana na Ujangili na Usafirishaji Haramu wa Wanyamapori

Dar es Salaam: Tarehe 4 Aprili 2018, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk. Inmi Patterson alikabidhi rasmi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) magari matatu aina ya  Toyota Land Cruiser kama sehemu ya programu ya Serikali ya Marekani ya Mafunzo na Kujenga Uwezo wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Usafirishaji Wanyamapori.

Kukabidhiwa kwa magari haya TAWA kunaongeza uwezo wa askari wake wa wanyamapori kufanya doria za kuzuia ujangili katika mapori ya akiba ya Rungwa/Kizigo/Muhesi na kuthibitisha ushirikiano endelevu na imara kati ya Marekani na Tanzania. Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Kaimu Balozi Patterson alisema kuwa, “kwa ushirikiano wa dhati kati ya serikali, raia wake, wabia wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi, tunaweza kulikabili na kulitokomeza janga hili la ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori.”

Serikali ya Marekani ni mbia mwenye fahari katika jitihada za Tanzania za kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori, ambapo imekuwa ikitoa mafunzo, vifaa na kufadhili shughuli za kujenga uwezo (capacity building) ili kuongeza uwezo wa askari wanyamapori kudhibiti ujangili katika mapori ya akiba ya Rungwa,Kizigo naMuhesi.  Miradi inayofadhiliwa hivi sasa na serikali ya Marekani ni pamoja na ule wa kuweka mfumo wa Mawasiliano ya simu, ukarabati wa vituo viwili vya askari wanyamapori na kuweka daraja maalumu la kamba kuwezesha kuvuka mto katika kipindi chote cha mwaka kuelekea mashariki mwa hifadhi.  “Mafanikio yaliyopatikana hivi karibuni yanatupa matumaini,” alisema Kaimu Balozi Patterson, “hata hivyo bado vita dhidi ya ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori haijamalizika. Serikali ya Marekani ina fahari kusimama pamoja nanyi katika vita hii.”

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe:  DPO@state.gov.

Jitihada za Serikali ya Marekani za Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Usafirishaji Haramu wa Wanyamapori:

Mwezi Oktoba 2016, Rais Mstaafu Barack Obama alisaini Mswada wa Sheria ya Kutokomeza, na Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Wanyamapori kuwa sheria kamili. Sheria hii ilipitishwa bila kupingwa na wajumbe kutoka vyama vyote kwa kuwa inaielekeza Serikali ya Marekani kuendelea kutoa misaada ya kiusalama kusaidia jitihada za kukabiliana na usafirishaji haramu na kuhakikisha pana uratibu mzuri kati ya taasisi mbalimbali za Serikali ya Marekani na balozi za Marekani katika nchi mbalimbali katika kushughulikia suala hili.

Kupitia ushirikiano wake na TAWA, Ubalozi wa Marekani unalenga kusaidia uhifadhi wa wanyamapori na maeneo yao kupitia shughuli mbalimbali zilizoratibiwa. Kwa miaka mitatu sasa, ushirikiano huu rasmi umejielekeza katika kushirikiana na askari wanyamapori katika kupanga na kutekeleza doria mahsusi, zinazowapo walinzi wa Kitanzania wa wanyamapori taarifa zinazowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu. Kazi hii inahitaji vifaa na serikali ya Marekani inachangia kwa kuwapa askari wanyamapori ramani, Mifumo ya utambuzi wa maeneo ya GPS, matrekta na matela yake pamoja na kukarabati vituo vya askari hao (ranger posts).