Leo, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) limesherehekea mwaka mmoja wa mafanikio ya Mradi wa Feed the Future Tanzania Kilimo Tija katika hafla iliyofanyika Chuo cha Kilimo (MATI) – Ilonga, wilayani Kilosa, Morogoro.
Hafla hii iliangazia mafanikio ya mradi na kusisitizia ubia na MATI Ilonga, ubia ulioanza mwezi Mei 2023. Ushirikiano huu umechangia pakubwa katika kuanzishwa kwa kituo cha mafunzo ya kilimo cha mbogamboga na matunda (horticulture training center – PTC) na kutoa mafunzo ya teknolojia zenye kuongeza tija katika uzalishaji kwa maafisa ughani wa serikali, wanafunzi wa MATI – Ilonga, na Vijana wanaoshiriki katika Mradi Kilimo wa Kujenga Kesho iliyo Njema (BBT/YIA).
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Mratibu wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Maendeleo ya Kilimo wa Wizara ya Kilimo, Bi. Dainess Mtei. Katika hafla hii, aliungana na maafisa wa USAID, maafisa wa serikali, wawakilishi wa sekta binafsi, wakulima na waandishi wa habari. Tukio hili halikutoa tu fursa kwa wadau kusherehekea mwaka mmoja wa mafanikio ta mradi wa Kilimo Tija, lakini pia lilikuwa ni jukwaa la kujadili jinsi sekta ya kilimo cha mbogamboga na matunda nchini Tanzania inavyoweza kufanyiwa mageuzi na kuwa kinara wa uzalishaji katika kanda nzima.
Katika hotuba yake, Naibu Mkurugenzi wa USAID/Tanzania Ofisi ya Ukuaji wa Uchumi Plato Hieronimus alisisitiza umuhimu wa ubia kati ya Tanzania, Marekani na sekta binafsi katika kutengeneza fursa za maendeleo kwa vijana na kutengeneza fursa za ajira.
“Bila mchango mkubwa wa sekta binafsi na msaada mkubwa kutoka serikali ya Tanzania, mradi huu wa USAID usingewezekana. Kutokana na ubia huu, biashara ndogo ndogo na zile za kati za Kitanzania zipatazo 2,500 zitapata msaada zinazouhitaji ili kuwekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 20 katika ukuaji na kuzalisha nafasi mpya za ajira zipatazo 7,400.” Aidha, katika kipindi cha utekelezaji wake (2022-2027), mradi unakusudia kuongeza kiwango cha ukuaji wa mapato ya biashara hadi kufikia ukuaji wa asilimia 15 kwa mwaka na mauzo ya zaidi ya dola za Kimarekani 100,000 kwa bidhaa zinazozalishwa na wakulima wadogo.
Katika awamu yake ya kwanza, kituo cha mafunzo ya kilimo cha mbogamboga na matunda (PTC) kilitoa mafunzo kwa vitendo kwa zaidi ya walengwa 420, wakiwemo wahadhiri na wanafunzi wa Chuo cha Kilimo, maafisa ughani, wakulima na vijana 84 wanaoshiriki mradi wa BBT-YIA ambao walipatiwa kwa vitendo ujuzi na stadi za uzalishaji wa mbogamboga na matunda.
Ushirikiano huu wenye matokeo makubwa kati ya timu za USAID Kilimo Tija na MATI-Ilonga katika mradi wa kituo cha mafunzo ya kilimo cha mbogamboga umewezesha uwekezaji wa zaidi ya Shilingi milioni 124.8 katika Shamba Darasa la MATI Ilonga la ekari 5 likiwa na teknolojia za kisasa za kilimo. Shamba darasa hili litaendelea kuwapatia maafisa ughani ujuzi na stadi zinazohitajika kuwasaidia wakulima wadogo mkoani.
Ukiilenga mikoa inayohudumiwa na Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania “SAGCOT” ya Iringa, Mbeya, Morogoro na Njombe pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, lengo kuu la mradi wa USAID wa Kilimo Tija wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 37.9 ni kuongeza kwa njia endelevu fursa za kiuchumi katika mifumo ya masoko ya mazao ya mbogomboga na matunda, huku msisitizo maalumu ukiwekwa kwa vijana. Mradi unafanya kazi na taasisi za sekta za umma na sekta binafsi, taasisi za vijana na wanawake na mamlaka za kitaifa na serikali za mitaa ili kuimarisha mifumo mifumo ya masoko ya mbogamboga na matunda na kufungua fursa za kiuchumi, hususan kwa vijana.