Marekani na Tanzania zazindua Programu ya Mbwa Maalumu Kubaini Dawa za Kulevya na Pembe za Ndovu

L to R: US Customs and Border Protection (CBP) Attaché Michael Lata, Acting Director General of Ports Authority Aloyce Matei, US Embassy Dar Chargé d’ Affaires, a.i. Virginia Blaser, Tourism Minister Lazaro Nyalandu and CBP Commissioner Gil Kerlikowske

dog_program_600pxaHapo tarehe 5 Mei  2015 katika Bandari ya Dar es Salaam, Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Maliasili na Utalii za Tanzania walitangaza kuzinduliwa kwa programu mpya ya kutumia mbwa kubaini dawa za kulevya na pembe za ndovu uitwao “Canine Detection Program.”  Kupitia programu hii, polisi wa Tanzania wakiwa na mbwa waliopatiwa mafunzo maalumu watawekwa katika Bandari na uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kusaidia kubaini dawa za kulevya nAdd a translation in Englisha pembe za ndovu.

Bandarini hapo, Kamishna wa Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani R. Gil Kerlikowske aliungana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Aloyce Matei pamoja na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Bi. Virginia Blaser katika kuizindua na kuielezea programu hii mpya na ya kibunifu ya ushirikano baina ya nchi hizi mbili. Katika miezi kadhaa ijayo, maafisa wa polisi wa Kitanzania watapatiwa mafunzo maalumu katika vyuo vya Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka huko Marekani. Watarejea nchini wakiwa na mbwa waliopatiwa mafunzo maalumu ya kubaini dawa za kulevya na pembe za ndovu zilizofichwa na wasafirishaji haramu wa bidhaa hizo. Maafisa hao na mbwa wao watapangiwa kufanya kazi bandarini na katika uwanja wa ndege wakiwa sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya wasafirishaji haramu wa dawa za kulevya na bidhaa zitokanazo na wanyamapori.

cbp_600px“Programu za kutumia mbwa hawa maalum, huongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa bandari na viwanja vya ndege kubaini bidhaa haramu zinazoingizwa au kutolewa nchini,” alisema Kamishna R. Gil Kerlikowske. Aliongeza kuwa “Tunafurahi kufanya kazi na wabia wetu nchini Tanzania na kuchangia nao ujuzi wetu wa kutumia mbwa maalum katika kuongeza uwezo wao kutambua bidhaa haramu, na kwa mara ya kwanza katika historia ya Idara yetu kuwezesha matumizi ya mbwa hawa katika kubaini pembe za ndovu.”

Naye Kaimu Balozi wa Marekani nchini Bi. Virginia Blaser alisema kuwa  “Programu hii tunayoizindua leo ni mfano mzuri wa mafanikio tunayoweza kuyapata pale ambapo wahusika wote tutafanya kazi pamoja kupitia mchakato unaoijumuisha serikali yote kwa ujumla wake (a whole-of-government approach) katika kukabiliana na biashara haramu za dawa za kulevya na ujangili.  Taasisi moja, wakala mmoja, wizara moja au hata nchi moja pekee haiwezi kufanikiwa katika jitihada hizi. Ili kuwakamata na kuwadhibiti majangili na wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni lazima sote tufanye kazi kwa pamoja.”

Mbali na mafunzo ya awali kwa maafisa wa polisi na kutoa mbwa hao, Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani itasaidia pia utekelezaji wa vipengele vingine vya programu hii. Vipengele hivyo ni pamoja na uandaaji wa mfumo wenye ufanisi wa usimamizi, mafunzo endelevu ya ziada na programu ya afya kwa mbwa.   Ushirikiano huu mpya unajengwa katika ubia imara na wa muda mrefu kati ya Tanzania na Marekani katika oparesheni za usalama na utekelezaji wa sheria.  Mathalan, Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani imetoa mafunzo kwa zaidi ya polisi na watendaji wa idara ya wanyamapori 200 kupitia kitengo chake cha doria za mipaka iliyo katika maeneo ya vijijini (Regional Rural Border Patrol Unit). Hali kadhalika, mwaka huu Watanzania wapatao kumi watashiriki katika programu ya mafunzo kwa wakufunzi itakayowawezesha kutoa mafunzo kwa kutumia mtaala wa doria za mipaka katika maeneo ya vijijini (Regional Rural Border Patrol curriculum).

Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani ni idara iliyo chini ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani yenye jukumu la kusimamia, kudhibiti na kulinda mipaka ya marekani na katika maeneo yote rasmi ya kuingilia nchini humo.

Kwa taarifa Zaidi, tafadhali wasiliana na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani.