Flag

An official website of the United States government

Marekani, Tanzania zashirikiana kukuza taaluma kupitia mpango wa kutoa chakula shuleni
4 MINUTE READ
Novemba 3, 2022

DAR ES SALAAM, TANZANIA – Serikali za Tanzania na Marekani leo zimezindua mradi wa elimu na lishe uitwao “Pamoja Tuwalishe” unaotarajiwa kuwanufaisha zaidi ya Watanzania 355,000 wakiwemo wanafunzi, wanafamilia, walimu, wakulima na wanajamii kwa kuboresha taaluma kupitia utoaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni.

Mradi huu ulizinduliwa katika hafla maalumu iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde na Prof Bonaventure Rutinwa ambaye in Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyewakilisha Wizara ya Elimu. Serikali ya Marekani iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Kilimo Jewel Bronaugh na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Robert Raines.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri Bronaugh alisema programu hii itainua ufaulu wa wanafunzi watakaoshiriki na hivyo kufungua zaidi fursa zao katika siku za usoni.

“Umuhimu na thamani Programu ya Kimataifa ya Lishe Shuleni ya McGovern-Dole inayoendeshwa nchini Tanzania na ari ya Wizara ya Kilimo ya Marekani kuusaidia ni kubwa sana. Wizara ya Kilimo ya Marekani imekuwa ikitoa msaada wa kiufundi, kifedha na kimawazo kwa programu za chakula shuleni na elimu toka mwaka 2010. Tunafurahi kutoa misaada hii inayotolewa wakati sahihi na kuendelea na ushirikiano huu muhimu.” Alisema Naibu Waziri Bronaugh.

Mradi wa Pamoja Tuwalishe utatekelezwa na taasisi iitwayo Global Communities, ambayo hapo awali ilijulikana kama Project Concern International (PCI), kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania. Mpango huu ni sehemu ya Programu ya Kimataifa ya Elimu na Lishe kwa Watoto ya Wizara ya Kilimo ya Marekani iitwayo USDA McGovern-Dole International Food for Education and Child Nutrition Program.   

Programu ya Kimataifa ya Elimu na Lishe ya Wizara ya Kilimo ya Marekani (McGovern-Dole International Food for Education and Child Nutrition project) nchini Tanzania ni programu ya kutoa chakula shuleni inayofadhiliwa na Wizara ya Kilimo ya Marekani (USDA) na kutekelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali ya Tanzania na jamii nyingi Mkoani Mara. Toka mwaka 2010, Wizara ya Kilimo ya Marekani imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 67 kwa shule mkoani Mara ili kuboresha lishe kwa wanafunzi, kuinua taaluma, usafi wa mazingira na mahudhurio shuleni. Mradi huu umewanufaisha zaidi ya wanafunzi 200,000 kutoka katika shule za msingi 231 kupitia shughuli mbalimbali zinazolenga kuongeza uwezo wa wanafunzi kujifunza shuleni na hivyo kuboresha ufaulu wao kwa kuboresha afya na lishe yao. Kwa taarifa zaidi kuhusu Programu hii: https://fas.usda.gov/programs/mcgovern-dole-food-education-program.