Marekani yaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 20 ya mashambulizi ya kigaidi katika balozi zake Afrika Mashariki na kuzindua makumbusho mapya kuwaenzi waath

Dar es Salaam, TANZANIA. Jumanne, tarehe 7 Agosti, Ubalozi wa Marekani na Makumbusho ya Taifa ya Tanzania walikuwa wenyeji wa hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya mashambulizi ya kigaidi katika balozi za Marekani jijini Dar es Salaam na Nairobi yaliyofanyika tarehe 7 Agosti 1998 na kuwaenzi waathiriwa wa mashambulizi hayo. Mwishoni mwa maadhimisho hayo, ndugu, jamaa na marafiki wa wale waliopoteza maisha na kujeruhiwa katika mashambulizi hayo waliungana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk. Inmi K. Patterson na Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Kangi Lugola katika kuweka mashada ya maua katika makumbusho mapya yaliyopewa jina “Tumaini baada ya Majonzi” katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa. Makumbusho haya maalumu ni matokeo ya ushirikiano wa kielimu na kitamaduni kati ya Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania.

Akizungumizia matukio hayo ya kusikitisha na kumbukumbu yake, Kaimu Balozi Patterson alisema, “Matukio haya ya kinyama yalikuwa ni jitihada zilizojaa woga za kuwafarakanisha Watanzania na Wamarekani, serikali ya Tanzania na serikali ya Marekani na hata kuwafarakanisha watu wa imani tofauti, lakini badala yake yalidhihirisha na kuimarisha umoja na mshikamano. Watu wa imani zote waliungana pamoja kulaani vitendo hivyo vya kinyama na kwa pamoja kuwaombea waathirika. Tunayazindua makumbusho haya kwa majonzi na kumbukizi ya wenzetu waliotangulia mbele ya haki, kwa kuelewa na kuwahurumia wale ambao maisha yao yamebadilika kabisa kutokana na mashambulizi hayo. Aidha kupitia kwayo, tunakumbuka vitendo vya kijasiri, kujitoa ili kuwasaidia wengine na ukarimu wa hali ya juu uliojidhihirisha wazi siku ya matukio haya na ambao umewaleta watu na mataifa yetu mawili karibu zaidi hata kuliko ilivyokuwa hapo awali.”

Mashambulizi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam yalisababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi wengine zaidi ya 100. Huko Nairobi watu 218 waliuawa na wengine zaidi ya 1,000 walijeruhiwa.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov