Marekani Yatoa Dola 9M kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani ili kusaidia kulisha Wakimbizi nchini Tanzania
[Translation → English] |
DAR ES SALAAM – Leo, Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), inatoa karibu dola za Marekani milioni 9 kama msaada muhimu wa chakula ili kuleta unafuu wa haraka kwa watu waishio katika mazingira magumu. Msaada huu mpya utawezesha ushirikiano kati ya USAID na Shirika la Umoja wa Mataifa wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kutoa msaada wa chakula ili kuokoa maisha ya wakimbizi 204,000 waliohifadhiwa kwenye kambi zilizopo kaskazini-magharibi mwa Tanzania.
“Tunashukuru kwa usaidizi huu unaoendelea na unaotolewa kwa wakati kutoka Marekani,” asema Sarah Gordon-Gibson, Mkurugenzi Mkazi na Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania. “Mchango huu ni muhimu sio tu kwa sababu ya thamani ya chakula kwenda kwa wakimbizi lakini pia kwa sababu ya matokeo chanya yatakayotokana na ununuzi wa chakula ndani ya nchi.
WFP imekabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha tangu mwaka 2020 uliopelekea kupunguzwa kwa mgao hadi asilimia 68 chini ya mahitaji. Kupunguzwa kwa mgao kwa muda mrefu huhatarisha ulaji wa chakula, lishe na afya ya wakimbizi. Licha ya ufadhili huu mpya, WFP bado haiwezi kutoa mgao kamili kwa wakimbizi kutokana na uhaba wa fedha unaohusiana na kiwango na idadi ya majanga ya kibinadamu duniani kote.
USAID ndiye mfadhili mkubwa zaidi wa operesheni ya WFP ya wakimbizi ya nchini Tanzania, ikitoa takriban theluthi moja ya bajeti yao kila mwaka. Tangazo la leo la dola za Marekani milioni 9 – ambazo ni nyongeza ya dola za Marekani milioni 4 zilizotolewa na USAID kwa WFP mwezi Februari 2022 – zitatumika kununua zaidi ya tani 12,000 za unga wa mahindi na kuingizwa kwenye kikapu cha mgao wa chakula kinachosaidia wakimbizi wanaoishi katika kambi mbili za wakimbizi nchini Tanzania.
Katika hotuba yake kwenye hafla hiyo, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Donald J. Wright ameitaka serikali ya Tanzania kuhakikisha mahitaji ya kibinadamu ya wahamiaji wote wanaoishi katika mazingira magumu nchini yanafikiwa. Balozi Wright aliendelea, “Matatizo haya – ukosefu wa fursa za kujikimu, huduma duni za afya na elimu, na utapiamlo – yanachangiwa na kuyumba na kupanda kwa bei kutokana na uvamizi usio wa haki wa Urusi dhidi ya Ukraine, ambao unasumbua ugavi wa chakula duniani, na kuongezeka kwa bei ya mafuta, na hivyo kufanya maisha ya Watanzania – na wakimbizi wanaoishi Tanzania – kuwa ghali na magumu zaidi.”
WFP inampa kila mkimbizi kikapu chenye chakula kila mwezi kilicho na unga wa mahindi, kunde, mafuta ya mboga na chumvi. Aidha, WFP inatoa msaada wa lishe kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha , na watoto chini ya umri wa miaka mitano.