Flag

An official website of the United States government

Marekani Yazindua Mpango Mpya wa Kukuza Sekta ya Mazao ya Bustani “Horticulture” Zanzibar
4 MINUTE READ
Juni 16, 2023

Leo, Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezindua Mpango Mpya wenye lengo la kuimarisha mifumo ya soko na kilimo cha mazao ya bustani Zanzibar ili kukuza maendeleo ya kiuchumi. Mradi wa Feed the Future Tanzania Kilimo Tija Visiwani Unguja na Pemba utaongeza fursa za kiuchumi katika kilimo cha mazao ya bustani, na kuwawezesha vijana. Mradi huo unafanya kazi na sekta za umma na binafsi, taasisi zinazolenga vijana na wanawake, serikali kuu na za mitaa ili kuimarisha mifumo ya huduma, uzalishaji na soko la mazao ya bustani, na kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana.

Uzinduzi huo umeongozwa na Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Zuberi Ali Maulid pamoja na Mawaziri, na maafisa kutoka USAID. Uzinduzi wa mradi wa Feed the Future Tanzania Kilimo Tija visiwani Zanzibar unadhihirisha dhamira ya USAID katika kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya mazao ya bustani katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika hotuba yake Mratibu wa Mpango wa Feed the Future kutoka USAID Tanzania Dkt. Tor Edwards alisisitiza juu ya ukuaji wa ushirikiano kati ya serikali ya Marekani na Tanzania, ambao unadhihirishwa na mafanikio ya sekta ya kilimo cha mazao ya bustani katika kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye lishe bora na kuinua wa uchumi wa Zanzibar.

“Muongo mmoja uliopita, Zanzibar ilikuwa ikiagiza mazao mengi ya bustani kutoka bara na vyanzo vingine, lakini sasa takribani asilimia 80 ya mazao ya bustani yanazalishwa Zanzibar,” alisema Dkt. Edwards. “Kilimo cha bustani Zanzibar kinashamiri na wakulima wanauza baadhi ya bidhaa katika hoteli za kitalii.”

Hafla hiyo ya uzinduzi pia ilihusisha makabidhiano ya pikipiki na vifaa vya kupima udongo kwa Maafisa Ugani wanaofanya kazi chini ya Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar. Mradi wa Kilimo Tija umetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.3 ili kusaidia sekta ya kilimo cha mazao ya bustani Zanzibar kwa mwaka 2023/2024, nakuchochea maendeleo ya uchumi endelevu.Mpango huu unatarajiwa kunufaisha takribani wafanyabiashara wadogo na wa kati 500 na wakulima 8,000 visiwani humo.

Ukilenga kukuza kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, na Njombe, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba (Zanzibar), mradi wa USAID Kilimo Tija utaongeza fursa za uchumi endelevu na kuimarisha mifumo ya huduma za sekta ya mazao ya bustani hususani ukilenga zaidi vijana na wanawake. Mradi huo unafanya kazi na sekta ya umma, binafsi, taasisi zinazolenga vijana na wanawake, na serikali kuu na za mitaa ili kuimarisha mifumo ya huduma na soko katika sekta ya kilimo cha mazao ya bustani na kufungua fursa za kiuchumi hasa kwa vijana.

Katika kipindi cha mradi (Septemba 2022 – Septemba 2027), mradi unatarajia kusaidia biashara ndogo na za kati 2,500 na maelfu ya wakulima wadogo hasa vijana. Mpango huo pia unalenga kufikia ukuaji wa asilimia 15 wa mapato ya kila mwaka kwa makampuni yatakayoshiriki, zaidi ya dola 100,000 katika mauzo ya mazao ya wakulima wadogo, zaidi ya dola milioni 20 katika uwekezaji na kutengeneza ajira mpya 7,400.