Flag

An official website of the United States government

MCC yazichagua Cabo Verde, Philippines na Tanzania kwa Ubia Mpya
5 MINUTE READ
Disemba 15, 2023

WASHINGTON (14 Disemba 2023) — Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) iliyoketi tarehe 13 Disemba katika kikao chake cha robo mwaka, imeichagua Cabo Verde kama nchi iliyokidhi vigezo vya kupata msaada kutoka shirika hilo, kupitia programu ya ruzuku ya miaka mitano (MCC compact) kwa lengo la kukuza utangamano wa kiuchumi wa kikanda. Aidha, Bodi hiyo imezichagua Tanzania na Philippines kuandaa programu za awali (threshold programs), ambazo ni ruzuku ndogo zaidi zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji uchumi.

“Hatua ya Bodi kuzichagua Cabo Verde, Philippines, na Tanzania ni ya kufurahisha na inayoziunganisha siku zilizopita za MCC na siku zijazo,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa MCC Alice Albright. “Nchi zote tatu zimeonyesha dhamira ya dhati ya kuzingatia utawala wa kidemokrasia, zikiwekeza katika watu wake na uhuru wa kiuchumi. Tuna shauku kubwa ya kuendeleza ubia wetu wa awali na kufanya kazi bega kwa bega na kila nchi miongoni mwa nchi hizi katika kuendeleza ustawi wa watu wake.”

Bodi ya MCC iliichagua Cabo Verde ambayo hapo awali ilikuwa mshirika wake, kwa ajili ya kuisaidia katika shughuli za utengamano wa uchumi kikanda kwa kutambua jitihada zake za dhati na za wazi za kuimarisha utawala wa kidemokrasia na changamoto zake kubwa za maendeleo na kupunguza umasikini. Katika ubia huu mpya, MCC itaisaidia Cabo Verde kukuza uchumi wake kwa kuiunganisha kikamilifu na kanda ya Afrika Magharibi.

Philippines na Tanzania ambazo zimekidhi vigezo kwa ajili ya miradi ya awali nazo pia zilikuwa washirika wa hapo awali wa MCC. Nchi hizi zimeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali za maendeleo. Katika miaka ya karibuni, Philippines na Tanzania zimeonyesha dhamira mpya ya kusukuma mbele mageuzi muhimu ya kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kulinda haki za binadamu na kupambana na rushwa. Katika kutambua jitihada hizi, Bodi ya MCC imezichagua Philippines na Tanzania kama wabia wake katika kuandaa programu za awali (threshold programs) zitakazolenga katika mageuzi ya kisera na kitaasisi ambazo nchi hizi zinaweza kuyafanya ili kupunguza umasikini na kuchochea ukuaji uchumi.

Kama sehemu ya majadiliano yake ya kila mwaka, Bodi ya MCC ilifanya pia mapitio ya utendaji wa nchi zilizochanguliwa hapo awali. Katika mapitio hayo, Bodi ya MCC ilizichagua tena Côte d’Ivoire na Senegal kuendelea kuandaa Mikataba ya Maendeleo ya Kikanda (regional compact development); Gambia, Togo, na Zambia kuendelea na mikataba ya maendeleo; na Mauritania kuendelea kuandaa programu ya miradi ya awali. Hali kadhalika, Bodi ilithibitisha kuunga kwake mkono kuendelea kwa ushirikiano wa MCC na nchi ya Belize. Pia Bodi iliichagua tena Sierra Leone kama nchi iliyokidhi vigezo vya kuendelea kupokea msaada wa MCC kwa kutambua maendeleo yaliyofikiwa katika mchakato wake wa majadiliano ya kitaifa, kuanza utekelezaji wa Makubaliano ya Umoja wa Kitaifa na kuanzisha kamati ya kitaifa ya kupitia sheria za uchaguzi. Hatua hizi ni mwanzo muhimu wa mchakato jumuishi wa kuimarisha taasisi za Kidemokrasia na za uchaguzi za Sierra Leone kufuatia uchaguzi wa Juni 2023. Katika kufikia uamuzi wake wa kuichagua tena Sierra Leone Bodi ilisisitizia matarajio yake ya kuendelea kupigwa hatua katika kuleta mageuzi ya kweli katika sheria na mifumo ya uchaguzi, kama yalivyoainishwa katika Makubaliano ya Umoja wa Kitaifa kabla ya kuidhinishwa kwa mkataba unaopendekezwa.

Mwisho, Bodi ya MCC ilipokea taarifa kuhusu maendeleo ya Kisiasa nchini Niger na hatua zilizofikiwa na MCC katika kufunga shughuli zake nchini humu kufuatia uamuzi wa kusitishwa ushirikiano. Aidha, Bodi ilipokea taarifa za hali ya utekelezaji wa miradi ya Barabara na Madaraja na Kuimarisha uthabiti wa maeneo ya Pwani ya Msumbiji dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi (Connectivity and Coastal Resilience Compact) kufuatia wasiwasi uliojitokeza kufuatia dosari zilizojitokeza katika chaguzi za serikali za mitaa za Oktoba 2023.

Pata maelezo zaidi kuhusu mchakato unaofuatwa na MCC kuchagua nchi za kupatiwa ruzuku kupitia tovuti yetu ya Who We Select.

Shirika la Changamoto za Millenia ni shirika huru la serikali ya Marekani linalojielekeza katika jitihada za kupunguza umaskini duniani kupitia ukuaji wa kiuchumi. Shirika hili lililoanzishwa mwaka 2004, hutoa ruzuku na msaada wa muda maalum kwa nchi zinazokidhi viwango na vigezo thabiti vya utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na kuheshimu haki za kidemokrasia.