Mfuko Wa Balozi Wa Marekani Wa Kupambana Na VVU/UKIMWI Watoa Fursa Kwa Asasi Za Kiraia Kuchangia Katika Kudhibiti UKIMWI Kitaifa

Dar es Salaam, Tanzania. Katika hafla iliyofanyika American Corner katika Maktaba ya Taifa Dar es Salaam Oktoba 1. 2019, Kaimu Balozi wa ubalozi wa Marekani Dr. Inmi Patterson kwa kupitia mfuko wa Balozi wa kupambana na VVU/UKIMWI alitunuku fedha kwa asasi za kiraia 11 zilizosajiliwa , zisizojiendesha kibiashara na za kidini kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania ili kutekeleza miradi ya UKIMWI Tanzania.

Watunukiwa waliomba ruzuku hizo ambazo zinatoka katika mfuko wa dharura, wa Raisi wa Marekani kwa ajili ya kupambana na UKIMWI yaani PEPFAR kwa kutuma maandiko yanayolenga kutekeleza afua za kupambana na UKIMWI katika jamii zao. Miradi iliyopendekezwa inalenga kuongeza uelewa kuhusu VVU na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa watu wanaoishi na VVU, yatima na watoto waishio katika mazingira hatarishi, makundi maalum yaliyo katika hatari ya kupata na kuambukiza UKIMWI, wanaume na vijana balehe; na wasichana balehe na wanawake vijana.

Miradi hiyo inalenga vipaumbele vya kimkakati ambavyo ni pamoja na kuboresha elimu ya matibabu ya dawa za kufubaza VVU, kupunguza unyanyapaa na ubaguzi, ubunifu katika kuzuia unyanyasaji wa kijinsia (GBV), upatikanji wa huduma kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia; pamoja na kuhamasisha wanaume kupima VVU na kuwaunganisha kwenye huduma za matibabu.

Mfuko wa Balozi wa kupambana na VVU/UKIMWI ulianzishwa mwaka 2009 na umeshatoa ruzuku kwa zaidi ya Asasi za kiraia 130, zisizojiendesha kibaishara nchini Tanzania. Serikali ya Marekani ina jivunia kuendeleza utamaduni wa kushirikiana na asasi hizi katika kufikia malengo ya Tanzania katika kudhibiti VVU/UKIMWI.

 

Watunukiwa wa ruzuku za Mfuko wa Balozi Kupambana na VVU/UKIMWI 2019 ni:

 1. BAKWATA National HIV/AIDS Program watatoa Mafunzo kwa viongozi 150 wa dini ya kiislamu, mashehe, Ma-Imamu, Waalimu wa madrasa, viongozi wa kike wa kiislamu, viongozi vijana wa kiislamu na watu waishio na VVU katika jamii za kiislamu zilizochaguliwa.
 1. Chimaba Sanaa wataongeza idadi ya wanaume na vijana wa kiume katika upimaji wa hiari na kuwaunganisha katika huduma ya tiba na matunzo wilayani Mbarali, Mkoani Mbeya.
 1. Tanzania Data lab itajenga uwezo wa washawishi wa mitandao ya kijamii kuongeza ushiriki wa vijana wa kiume katika masuala ya upimaji wa VVU/UKIMWI na kujenga jamii isiyokuwa na unyanyapaa.
 1. Foundation for Development (FODEO) kwa kutumia vikundi rika watahamasisha wasichana balehe na wanawake vijana kujua hali yao ya maambukizi ya VVU na kuwaunganisha na watoa ushauri nasaha na upimaji wa hiari na waathirika watapewa ushauri wa kujiunga kwenye kliniki zinazotoa dawa za kufubaza makali ya UKIMWI . Wasichana balehe na wanawake vijana watapewa elimu ya kujikinga dhidi ya VVU kupitia watoa huduma ngazi ya jamii watakapotembelewa majumbani.
 1. Jitambue Lembuka Tanzania (JLT) itapunguza unyanyasaji dhidi ya wasichana katika shule za msingi, madarasa ya chini ya sekondari pamoja na wale wasioshuleni. Wasichana walioathirika na VVU watapewa kipaumbele katika programu za kuwajengea uwezo.
 1. Jumuiya ya Kuelimisha Athari ya Dawa za Kulevya, UKIMWI na Mimba Katika Umri Mdogo (JUKAMKUM) kwa kutembelea watu majumbani, watatoa ushauri nasaha ili kupunguza unyanyapaa na kutumia viongozi wa kidini na wa kijamii kupunguza unyanyapaa na ubaguzi katika jamii.
 1. Kigoma Alliance for Community Needs (KACON) itatumia elimu kwa mbinu ya mawasiliano ya kubadilisha tabia kuhamasisha wanaume na vijana wadogo kupima VVU/UKIMWI, kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za kufubaza VVU (ART), na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi.
 1. Muungano wa Vikundi vya Maendeleo ya Wanawake Kamachumu (MUVIMAWAKA) itatumia semina na huduma mkoba kuwafikia wanawake walio katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU/UKIMWI ili kuboresha uwezo wao kujikinga na VVU, kupima pamoja na kuendelea na matibabu; na kuongeza upatikanaji wa msaada kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia.
 1. Njombe Southern Highland Association (NSHDA) itatoa elimu kwa wanachama 1500 katika kikundi chao cha kilimo cha mbogamboga na jamii yao katika kata mbili ili waweze kupata huduma za afya kwa ajili ya upimaji wa VVU, kuanza matibabu ya dawa za kufubaza makali ya VVU na elimu ya namna ya kubaki kwenye matumizi sahihi ya dawa kwa watu waishio na VVU,  kushughulikia masuala ya unyanyapaa na ubaguzi, kuhamasisha wanaume na vijana wadogo kupima VVU na kuelimisha juu ya athari za unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.
 1. Parakuiyo Pastoralists Indigenous Community Development Organisation (PAICODEO) itaongeza elimu ya uelewa wa matibabu ya VVU/UKIMWI na kupunguza unyanyapaa katika jamii za wafugaji kupitia mbinu za mawasiliano ya kubadilisha tabia.
 1. Tanzania Network of Women Living with HIV and AIDS (TNW+) itafanyakazi na watu waishio na VVU katika wilaya ya Kiteto, eneo ambalo ni gumu kulifikia hasa katika kipindi cha mvua. Wanajamii katika eneo hili wana Imani kali za kimila ambazo zinaathiri matumizi sahihi ya dawa zinazofubaza makali ya VVU na kusababisha waliokatika tiba kuacha kuhudhuria kliniki.

Kujua Zaidi juu ya mfuko wa Balozi wa kupambana na VVU/UKIMWI tafadhali tembelea tovuti ya PEPFAR Tanzania (https://tz.usembassy.gov/our-relationship/pepfar/) au wasiliana na mratibu wa PEPFAR wa asasi za kijamii PEPFARGrantsDar@state.gov.