Mfuko Wa Balozi Wa Marekani Wa Kupambana Na VVU/UKIMWI Kuzijengea Uwezo Asasi Zisizo Za Kiserikali Za Ndani

Dar es Salaam, TANZANIA.  Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania,  Inmi Patterson   amekabidhi fedha za msaada kutoka Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kupambana na VVU/UKIMWI, (AFHR), kwa vikundi vya kijamii na Asasi Zisizo za Kiserikali 18, ambazo hufanya kazi kusaidia watu walioathirika na UKIMWI. Sherehe ya makabidhiano hayo imefanyika ubalozini leo tarehe 6 Septemba, 2017.

Vikundi vilivyopokea mafungu hayo ya fedha viliomba kutoka Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI  (PEPFAR) – kwa kuandika miradi ambayo itasaidia jamii kuthibiti janga la magonjwa hatari kwenye jamii zao wakijikita zaidi katika watu wanaoishi na VVU, wajane, wasimamizi wa familia, makundi maalum yaliyo katika mazingira hatarishi, wakiwamo yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wasichana balehe na wanawake vijana.

Miradi mingi kati ya iliyoorodheshwa hapa chini inalenga kuimarisha upatikanaji wa maji safi, usafi wa afya na mazingira, umeme na mahitaji mengine muhimu katika shule na vituo vya afya. Miradi mingine ni ya shughuli za kuongeza kipato, kama usagaji nafaka na utengenezaji matofali, ikiwa ni njia ya kutengeneza ajira na kuongeza kipato  kwa ajili ya wanajamii walio katika hali ngumu. Kwa pamoja miradi hii itasaidia elimu, huduma za afya, na maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania.

Kila mradi unaonesha mfano katika njia ya kufikia wananchi kwa kutokea chini kwenda juu ambapo jamii husika hubainisha matatizo yao na kuja na suluhisho la matatizo hayo. Marekani inaona fahari kushirikiana na watanzania hawa wanaotatua matatizo.

Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kupambana na VVU/UKIMWI (AFHR) ulianza mwaka 2009 na umekwishatoa fedha kwa vikundi vya kijamii 93 hapa Tanzania. Mpango huu umeendelea kuwa utamaduni imara wa ushirikiano kati ya wananchi wa Marekani na  Tanzania.

Ili kupata taarifa zaidi, tafadhali piga simu Ubalozi wa Marekani, Ofisi ya Habari, simu: +255 22 229-4000 au wasiliana kwa barua pepe kupitia anuani hii: DPO@state.gov.


Orosha ya Asasi Zilizokabidhiwa Msaada wa Fedha kutoka Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kupambana na VVU/UKIMWI (AFHR) kwa mwaka 2017:

 1. Amenity Nonprofit Charity Organization (ANCO) itajenga tangi la maji katika shule ya msingi Nyansha wilayani Kasulu, mkoa wa Kigoma.
 1. Association of Rare Blood Donor (ARBD) watanunua na kufunga vitanda 50 vya hospitali na magodoro, vitanda 25 vya kujifungulia kina mama wazazi, na makabati 25 ya kando ya vitanda ili kuimarisha huduma za kujifungua katika wodi za wazazi za vituo 10 vya afya katika wilaya za Kalambo, Nkasi na  Sumbawanga mkoani Rukwa.
 1. Charity Organization itaimarisha mradi uliopo wa maeneo ya kando ya maji unaowasaidia watu wanaoishi na VVU huko Kigangama, wilayani Magu, mkoani Mwanza.
 1. Community Development Mission of Tanzania (CDMT) utajenga vyoo vya shimo vyenye matundu matano katika shule tatu za msingi za Seuta, Msomela na Masatu, huko Chanika, wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga.
 1. Ebeneza Group (Kikundi cha Ebeneza) kitanunua zana na mashine za kutumia katika mafunzo ya ufundi seremala kwa vijana wakiwemo watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi na watu wanaoishi na VVU mkoani Shinyanga.
 1. Health Promotion Tanzania (HDT) iliona baadhi ya akina mama wajawazito wakifika kwenye kliniki ili kujifungua wakiondolewa kutokana na vituo husika kukosa vifaa bora vya kutupa kondo la nyuma la mtoto na vyoo, hivyo akina mama hao kulazimika kutafuta huduma katika vituo vya mbali. Ili kutatua tatizo hilo, Health Promotion Tanzania (HDT) itajenga eneo la kutupa makondo ya nyuma ya watoto na mfumo wa kuvuna maji ya mvua katika zahanati za Kirushya na Murubanga, katika wilaya ya Ngara mkoani Kagera. HDT pia itajenga vyoo vya shimo vyenye matundu manne katika zahanati ya Kirushya.
 1. Hope Community Development itanunua paneli za nishati ya jua katika kliniki ya Amani na shule ya sekondari ya Dr. John Chacha na Taasisi ya Uongozi wilayani Tarime mkoa wa Mara.
 1. Kagera Women Environmental Society (KAWESO) itanunua na kufunga mashine ya kufyatulia matofali itakayowanufaisha mamia ya watu wasio na makazi, wakiwemo wanaoishi na VVU, wajane na familia zao huko Muleba, mkoani Kagera.
 1. KIEMA Group itajenga mashimo kumi na manne ya vyoo katika Shule ya Msingi Rubihizi iliyoko Kitahana, wilayani Kibondo mkoa wa Kigoma.
 1. Kimwani Women Empowerment and Social Development (KIMWESO) watajenga mashimo na vyoo kumi kati shule za msingi za Mbanju na Njenga zilizopo wilayani Masasi mkoani Mtwara.
 1. Kwetu Faraja itanunua na kufunga mashine za kukoboa mpunga na kukamua mafuta ili kuongeza kipato kwa ajili ya kituo cha watoto yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
 1. Linda Children’s Foundation itajenga vyoo vyenye matundu sita katika shule yake ya mchepuo wa Kiingereza iliyoko Kifaru katika wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro.
 1. Sustainable Hub for Policy Initiatives (SHPI) itanunua na kufunga mshine nne za kusaga mahindi ambazo zitawasaidia moja kwa moja watu wanaoishi na VVU, wajane na watoto yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi huko Kiabakari wilaya ya Butiama mkoani Mara.
 1. Tanzania HIV/AIDS Dunia Elimu Yangu (THADEY) itanunua vyerehani na vifaa vyake vinavyohitajika katika mafunzo ya ushonaji ili kuwanufaisha wasichana, wanawake vijana, wajane na watu wanaoishi na VVU katika eneo la Picha ya Ndege, Kibaha mkoa wa Pwani.
 1. Tanzania Youth Health and Development Organization (TAYOHADO) itajenga matangi sita ya kuvuna maji ya mvua ili kusaidia shule na watu walioathirika na VVU huko Sabasaba, Tarime mkoani Mara.
 1. Tumaini La Maisha Tanzania itaanzisha kanzidata ya wagonjwa watoto wa saratani wakiwemo wenye VVU. Kanzidata hiyo itakusanya na kuunganisha taarifa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya KCMC Moshi, Hospitali ya Sengerema, Hospitali ya Bugando , Hospitali ya rufaa ya Mbeya, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar. Tumaini La Maisha Tanzania ipo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
 1. WOCHIVI itajenga mfumo wa kuvuna maji ya mvua na vyoo sita vya shimo kwenye shule ya msingi Olkereyan katika wilaya ya Moshono, Arusha.
 1. Women of Vision (WOV) watajenga mashimo ya vyoo yenye matundu kumi katika shule mbili za msingi wilayani Mikindani, mkoani Mtwara.

Ili kufahamu zaidi kuhusu Mfuko wa Balozi wa Kupambana na VVU/UKIMWI, tafadhali tembelea tovuti  ya PERFAR Tanzania (https://tz.usembassy.gov/our-relationship/pepfar/) au wasiliana na Mratibu wa Mawasiliano Asasi za Kiraia wa  PEPFAR kwa anuani hii  PEPFARGrantsDar@state.gov.