Mfuko Wa Balozi Wa Marekani Wa Kusaidia Mapambano Dhidi Ya VVU/Ukimwi Unasaidia Makundi Ya Kijamii Na Watu Waishio Na Virusi Vya Ukimwi Kushughulikia

Dar es Salaam, TANZANIA.  Katika sherehe zilizofanyika American Corner pale Maktaba Kuu ya Taifa, Dar es Salaam, tarehe 21 Septemba, 2018, Kaimu Balozi wa Marekani, Dkt. Inmi Patterson alitoa msaada kutoka kwenye Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya VVU/UKIMWI kwenda kwa makundi kumi na tisa (19) ya kijamii na mashirika yasiyo jiendesha kibiashara kutoka maeneo yote Tanzania yanayotoa msaada kwa waathirika wa Virusi vya UKIMWI.

Wapokeaji wa misaada hiyo walituma maombi kupata fedha hiyo – inayotoka kwenye Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) – ikiwa ni muitikio wa maombi ya kuwasilisha maandiko ya miradi inayolenga katika kusaidia kuzuia maambukizi ya VVU katika maeneo yao. Miradi iliyopendekezwa inalenga masuala yanayowakumba watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, wajane, wasimamizi wa familia, na watu waishio kwenye mazingira hatarishi kama yatima, wasichana balehe na wanawake vijana.

Miradi mingi (orodha imewekwa chini) itakuza shughuli za kuingiza kipato kama kukamua mafuta na ufugaji wa kuku- ili kutengeneza ajira na kupata fedha za ziada kwa ajili ya makundi yaliyo kwenye mazingira hatarishi katika jamii. Miradi mingine itaboresha mazingira kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuwezesha upatikanaji wa matenki/mapipa ya kuhifadhi maji, umeme wa jua, na vifaa kama vitanda vya wagonjwa ikiwa ni pamoja na vitanda vya kujifungulia.

Miradi hii yote inatumia mbinu ya kutumia jamii husika hutambua changamoto katika maeneo yao na kupendekeza ufumbuzi. Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya VVU/UKIMWI ulianza Mwaka elfu mbili na tisa na umeshatoa misaada kwa makundi ya kijamii yapatayo mia moja na kumi na moja nchini Tanzania. Marekani inajivunia kuendeleza utamaduni huu imara wa kushirikiana na mashirika haya ya kijamii.

Washindi wa Msaada wa Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya VVU/UKIMWI:

 1. African Women AIDS Working Group (AFRIWAG) watapanua biashara yao ya kutengeneza matofali ili kuwasaidia watu waishio na Virusi vya UUKIMWI na UKIMWI katika Wilaya ya Tanga, mkoani Tanga.
 2. Agro-Livestock and Welfare Advancement Rural Environment watajenga matenki sita ya kuvuna maji ya mvua katika Zahanati wilayani Kilosa na Dakawa wilayani Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro. Katika wilaya ya Kilosa, matenki haya yatakuwa katika zahanati za Magomeni, Tindiga, na Chanzuru. Katika Wilaya ya Morogoro vijijini, matenki yatakuwa kwenye zahanati za Magari, Tunuguo na Bondwa.
 3. Alliance for Women, Children and Youths Survivors (AWCYS) watanunua mashine tatu za kusaga unga na kuanzisha biashara ya kusaga mahindi na mihogo ili kuwasaidia watu waishio na VVU kupata kipato. Mradi huu utafanyikia Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
 4. Anglican Church of Tanzania – Diocese of Lake Rukwa (ACT-DLR)- Kanisa la Anglikana Tanzania- Dayosisi ya Ziwa Rukwa watakuza mradi wao wa ufugaji wa kuku kwa kununua mashine tano za kutotolesha vifaranga kwa makundi matano ya watu waishio na Virusi vya UKIMWI ambao wanawatunza watoto mia tano (500) ambao ni yatima na waishio kwenye mazingira hatarishi.
 5. The Communication and Information Sharing Group in Wash Emergencies (CIGRO-WASH) watanunua na kufunga mashine ya kukamulia mafuta ya mbegu za alizeti kwaajili ya vikundi viwili vilivyosajiliwa, vyenye watu hamsini (50) waishio na VVU/UKIMWI, wilaya ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa, ili kuwasadia kupata kipato.
 6. Conservation of Nature for Survival (CONASU) watafunga vifaa vya kutengeneza umeme wa jua na mfumo wa kuvuna na kuhifadhi maji katika zahanati za Kumbulu na Chanjale, zote katika Kata ya Chajale, wilaya ya Gairo mkoani Morogoro.
 7. Health Promotion Tanzania (HDT) watajenga mifumo ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua katika zahanati tano katika wilaya ya Geita, mkoani Geita. Zahanati hizi ni: Zahanati ya Kasang’hwa, Zahanati ya Kishinda, Zahanati ya Mwamitilwa, Zahanati ya Nyalwanzaja na Zahanati ya Nyamwilolelwa.
 8. Kijogoo Group for Community Development (KGCD) watafunga tenki la maji na mashine ya kutotolesha vifaranga vya kuku katika kituo cha watoto yatima cha Mgolole, kilichopo wilaya ya Morogoro Mjini, mkoani Morogoro.
 9. Mavuno Village watanunua greenhouse au banda kitalu na kuendeleza miradi yake ya kuhifadhi nyuki ili kupata kipato kitakachosaidia kazi wanazozifanya kusaidia watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira hatarishi, katika wilaya ya Magu, mkoani Mwanza.
 1. Neema Village watanunua mashine za kuchemshia maji zinazotumia umeme wa jua kwa ajili ya matumizi ya nyumba wanapowalea watoto waliotelekezwa au walio hatarini kupata magonjwa mfano wale walio na lishe duni au hali dhaifu ya kimwili. Neema Village wanafanya kazi Wilaya ya Arusha, mkoani Arusha.
 2. Rural Islands Community Health Initiative (RICHI) iko Wilaya ya Buchosa, mkoani Mwanza na itatoa elimu ya afya katika vijiji vilivyopo kwenye visiwa vya Ziwa Victoria. Elimu hii itaweka mkazo kwenye unyonyeshaji wa maziwa ya mama ya mwanzo, na kuzuia utapiamlo na magonjwa, na yatalenga wamama wanaonyonyesha waishio na VVU/UKIMWI na watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira hatarishi walio na umri chini ya miaka mitano.
 3. Support Women and Orphans in Need (SWONE) watakuza mradi wao wa kuwapa wanawake wenye kipato cha chini, na watu wanaoishi na VVU, mafunzo ya ushonaji, kudarizi na ujasiriamali. Shirika litanunua mashine tano za cherehani, mashine moja ya kudarizi na mashine moja ya Overlock kwaajili ya kituo chake cha mafunzo kilichopo Wilaya ya Arusha, mkoani Arusha.
 4. Tanzania Data Lab (dLab) watawajengea uwezo watendaji washirika wa PEPFAR na wadau katika kutumia na kuunganisha takwimu na itatengeneza dashboard ili kuoanisha seti za takwimu kutoka katika vyanzo mbalimbali vya takwimu. Huu mradi utafanyikia Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
 5. Tanzania League of the Blind watanunua na kupeleka vitanda vitatu vya kujifungulia na vitanda kumi vya wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Sumve, iliyoko wilayani Kwimba, mkoani Mwanza.
 6. The Olive Branch for Children watajenga vyoo vinne vyenye mfumo wa kugeuza kinyesi kuwa mbolea na matenki mawili ya maji pale “The Peace Home”, ambapo wanalea watoto walio kwenye mazingira hatarishi na vyoo vinne katika kituo cha kijiji cha Mwashota, karibu na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Pia watanunua misumeno na cherehani ili kupanua mtaala na utendaji wa Kituo cha Kubini, ambacho kinatoa mafunzo ya kuanzisha biashara kwa vijana walio kwenye mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na vijana waishio na VVU.
 7. Thubutu Africa Initiatives (TAI) watakarabati na kujenga vyoo nane vya wasichana katika shule ya Sekondari ya Pandagichiza, shule ya Sekondari Old Shinyanga na shule ya sekondari Kizumbi, zote zikiwa kwenye Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, mkoani Shinyanga. Pia, TAI itatoa mafunzo kwa wanafunzi juu ya kusimamia usafi na elimu ya afya ya uzazi.
 8. Tongwa Lishe Group watanunua mashine ya kutengeneza siagi ya karanga, kuchuja mafuta, na mashine ya kumenyea karanga ili kuendeleza biashara ya utayarishaji wa siagi ya karanga, ambayo itainua kipato cha wanakikundi vijana wadogo arobaini na nane (48), ambapo kati yao kumi na tisa (19) wanaishi na VVU na ishirini (20) ni walezi wa watoto yatima hamsini na tatu (53) walioko wilaya ya Mpanda, Mkoani Katavi.
 9. Women Pro Development Group (WODEG) watanunua mashine nane za kufyatulia matofali kwaajili ya vikundi vidogo nane vya wajasiriamali walioko vijijini, vinavyoundwa na wajane na watu wanaoishi na VVU katika wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, ili kuwasaidia kupata kipato.
 10. Youth Volunteers Against Risky Behaviors (YOVARIBE) watanunua vifaa vya kuoshea magari kwaajili ya watu wanaopata nafuu kutoka kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na taulo za kike zinazoweza kutumika zaidi ya mara moja kwa ajili ya wanawake wanaotumia madawa ya kulevya. Kundi hili linatoa ushauri nasaha, upimaji wa Virusi vya UKIMWI, rufaa ya tiba kwa wanaoishi na VVU na rufaa kwenda kwenye vituo vyenye tiba ya Methadone ili kusaidia watu kupata nafuu kutoka kwenye uraibu au ulevi wa madawa.

 

Kupata taarifa zaidi kuhusu Mfuko wa Balozi wa Mapambano dhidi ya UKIMWI, Tafadhali tembelea Tovuti ya PEPFAR PEPFAR Tanzania website (https://tz.usembassy.gov/our-relationship/pepfar/) au wasiliana na Mratibu wa PEPFAR wa Asasi za Kijamii kupitia anuani hii PEPFARGrantsDar@state.gov