Mifumo Mipya ya Taarifa za Serikali ya Tanzania kwaajili ya Kuboresha Utoaji wa Huduma za Umma

Dodoma (Septemba 5) – Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa leo katika hafla mkoani Dodoma alitangaza uzinduzi wa Mfumo wa kuandaa Mipango, Bajeti na Taarifa (PlanRep) na Mfumo wa Uhasibu na Utoaji Taarifa kwenye Vituo vya Kutolea Huduma (FFARS). Katika hafla hii pia alishiriki Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Inmi Patterson na viongozi wa juu wa Serikali na Mawaziri kuonesha matarajio makubwa ya PlanRep na FFARS katika sekta na taasisi za serikali nchini Tanzania.

Kwa ushirikiano wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa (USAID) mifumo hii ya usimamizi wa taarifa kwa kutumia TEHAMA itachangia katika kuboresha uandaaji wa mipango, bajeti na usimamizi wa kifedha kwa kila ngazi ya serikali. Hasa, mifumo hii itahakikisha inaimarisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji wa matumizi ya fedha kati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na vituo vya kutolea huduma, kuelekea katika kuboresha huduma za umma kwa wananchi.

Ikiwa imezinduliwa zaidi ya miaka kumi iliyopita kama chombo cha uaandaaji mipango, kutoa taarifa, na bajeti kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, maboresho ya mfumo wa PlanRep yanaonesha mabadiliko zaidi kuliko ile ya awali. Ingawa toleo la mwanzo halikupatikana kwenye mtandao na watumiaji wa serikali walitegemea matoleo tofauti ya programu, mfumo huu mpya, una muundo wenye mfanano na una patikana katika mtandao wakati wowote, popote. Zaidi ya hayo, toleo jipya la mifumo linaruhusu PlanRep kutoa na kupokea taarifa na nyaraka kwenye mifumo mingine ya taarifa za serikali na kuepusha mchakato wa muda mrefu wa uandaaji wa mipango na bajeti uliochangia makosa mengi katika kuhifadhi taarifa na nyaraka. Kwa watumiaji zaidi ya 1,500 waliohitimu mafunzo ya kutumia mfumo mpya, PlanRep itatumika katika sekta zote za umma na kuimarisha mfumo wa ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za umma kwa wananchi.

Wakati Mfumo wa PlanRep inasaidia katika mipango, bajeti na utoaji wa taarifa katika ngazi mbalimbali za serikali, Mfumo wa FFARS utatumika kama mfumo wa uhasibu na utoaji wa taarifa kwa vituo kama vile shule na vituo vya afya, ambapo fedha kwa ajili ya huduma za umma zinasimamiwa. FFARS husaidia watoa huduma kuandaa taarifa za kifedha na nyaraka rahisi kwa kurekodi upatikanaji na chanzo cha fedha zao kwa huduma za msingi katika kila kituo. FFARS pia inasaidia kufuatilia jinsi fedha zinavyotumika na kuhakikisha taratibu na sheria za manunuzi na mahitaji ya kutoa taarifa yanazingatia matumizi ya fedha za kutolea huduma. Kwa taarifa hii, Serikali ya Tanzania itaendeleza mfumo imara wa usimamizi wa fedha za umma ambao utaongeza uwazi ili watoa huduma wawe wawajibikaji kwa jamii na mashirika wanayoyatumikia.

“Marekani inajivunia kushirikiana na Tanzania, mnapofanya kazi kwa malengo ya kuwa na serikali yenye uwazi, maendeleo endelevu na ustawi wa pamoja” alisema Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Inmi Patterson  wakati wa hafla hiyo. “Kwa Pamoja, mifumo hii miwili itaongeza ufanisi na kuboresha usimamizi wa fedha, na kuwezesha Serikali ya Tanzania kutoa fedha kwa malengo yaliyokusudiwa na mahitaji ya wananchi kwa ufasaha.

Msaada wa Serikali ya Marekani kwa PlanRep na FFARS uko chini ya mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3). Iliyoundwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, PS3 inafanya kazi katika mikoa 13 na Halmashauri 93 kuimarisha huduma za umma kwa njia ya utawala bora, fedha, rasilimali watu, na mifumo ya taarifa. Pamoja na uundwaji na uendelezaji wa PlanRep na FFARS, PS3 hivi karibuni ilisaidia uundwaji, utengenezaji na uzinduzi wa tovuti kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kote mapema mwezi Machi mwaka huu.

Kuomba taarifa zaidi, tafadhali piga simu Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam Ofisi Habari huko Simu: +255 22 229-4000 au barua pepe: DPO@state.gov, au Wasiliana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Simu: +255262320024 au barua pepe: dict.staff@tamisemi.go.tz