Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) yapongeza mageuzi yaliyofanywa na Tanzania lakini yaelezea wasiwasi wake kuhusu rushwa

MCC Logo

DAR ES SALAAM, TANZANIA – Katika mkutano wake wa robo mwaka uliofanyika tarehe 17 Septemba 2015, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) linalomilikiwa na Serikali ya Marekani lilijadili pendekezo la mkataba mpya na serikali ya Tanzania wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 472.8 unaolenga kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, uimarishaji wa taasisi zinazohusika na usambazaji wa nishati hiyo na usimamizi wake, kusaidia utekelezaji wa mipango ya mageuzi katika sekta ya nishati na kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi.

Baada ya mkutano huo Bodi ya MCC ilitoa taarifa rasmi ikieleza kuwa Serikali ya Tanzania imefanya mageuzi muhimu kama sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wenye ufanisi la mkataba huu. Pamoja na kutambua mageuzi hayo, Bodi iliendelea kuelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania na kukubaliana kwamba ni lazima kwanza Tanzania ifaulu kufikia kigezo cha udhibiti wa Rushwa (Control of Corruption indicator) katika  tathmini ya mwaka 2016 ya jinsi nchi husika zinavyokidhi vigezo vya kusaidiwa na MCC (MCC’s fiscal year 2016 scorecard).

Kufuatia taarifa hiyo, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mark Childress alisema kuwa “tunafurahishwa na jitihada za Tanzania katika miezi kadhaa iliyopita za kufanya  mageuzi ya kimuundo na kitaasisi ili kuinua ufanisi, tija na uwazi katika sekta ya nishati. Hata hivyo, kama ambavyo Bodi ya MCC imebainisha, pamoja na jitihada kadhaa zilizochukuliwa kukabiliana na rushwa, bado tatizo hili limeendelea kuwa kubwa likiathiri nyanja zote za maendeleo na ufanisi katika utendaji wa serikali.”

Katika taarifa yake, Bodi ya MCC imeeleza pia matumaini yake kwamba uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika hapo Oktoba 25 utakuwa huru na wa haki, hasa ikizingatiwa umuhimu mkubwa ambao MCC inauweka katika haki za kidemokrasia.  Balozi Childress aliongeza kuwa “tunatambua rekodi ya Tanzania katika maendeleo ya demokrasia na tunaunga mkono na kusaidia jitihada endelevu za Tanzania katika kuimarisha taasisi zake za kidemokrasia. Tunatarajia kuona uchaguzi ulio huru, wa haki, wa amani na ambao utawasilisha matakwa ya watu wa Tanzania.”

Tamko kamili la mkutano huo wa Bodi ya Wakurugenzi ya MCC wa tarehe 17 Septemba 2015 inapatikana katika tovuti ya MCC kwa anuani ifuatayo: https://www.mcc.gov/news-and-events/release/mcc-statement-on-board-of-directors-discussion-of-tanzania-091715

Shirika la Changamoto za Milenia ni taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi zinazoendelea. Shughuli za MCC zinajengwa katika msingi kwamba msaada utaleta ufanisi na matokeo makubwa zaidi pale tu unapoimarisha utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu ambao unakuza uchumi na kuondoa umasikini.