Mkurugenzi Mkazi Andy Karas Azuru Progamu za USAID Mkoani Morogoro

Dar es Salaam, Tanzania: Toka tarehe  17 hadi 20 Oktoba, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Andy Karas alifanya ziara mkoani Morogoro ili kujionea matokeo ya programu mbalimbali zinazoendeshwa na USAID mkoani humo pamoja na kufanya mazungumzo na wabia na walengwa wa programu hizo. Ziara hii inaakisi wigo mpana wa miradi inayofadhiliwa na Marekani nchini Tanzania, ikijumuisha sekta za kilimo, lishe, elimu, afya, wanawake na vijana na utawala bora.

Kwa muda mrefu, mkoa wa Morogoro umekuwa mlengwa wa msaada wa maendeleo wa Serikali ya Marekani kutokana na fursa yake kubwa ya kilimo, taasisi za kielimu na kuwa katika eneo zuri la kimkakati lililo karibu na miundombinu ya usafirishaji. Mkoani humo ndipo ilipo mojawapo ya programu za kwanza kabisa kufadhiliwa na USAID nchini Tanzania – ambayo ni uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.  Akiwa chuoni hapo, Mkurugenzi Mkazi Karas alitembelea maabara mpya ya TEHAMA iliyofadhiliwa na USAID  na kukutana na wanafunzi wa Shahada ya Uzamili walionufaika kutokana na mradi wa utafiti wa kilimo ujulikanao kama Innovative Agricultural Research Initiative -iAGRI, uliokuwa ukifadhiliwa na USAID.

Ziara hiyo iliangazia msaada unaotolewa na USAID kwa shule, vituo vya afya, mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Dakawa na ushirika wa wakulima 950 wanaonufaika nao. Hali kadhalika, ziara ilihusisha miradi ya kijamii ya lishe na ile ya kuboresha utoaji huduma katika sekta ya umma na mamlaka za serikali za mitaa.  Aidha, Mkurugenzi Mkazi Karas alikutana na viongozi wa serikali mkoani humo pamoja na washiriki wa programu nyingine zinazofadhiliwa na Serikali ya Marekani ikiwa ni pamoja na Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps na wahitimu wa mpango wa kuwaendeleza vijana wa Kiafrika katika uongozi uitwao Young African Leaders Initiative (YALI).

Mkurugenzi Mkazi Andy Karas alijiunga na USAID/Tanzania mwezi Agosti 2017. Amewahi kufanyakazi na USAID katika nchi za Rwanda, Afghanistan, Djibouti, Ghana na Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki jijini Nairobi.

Picha kuhusu ziara hizo kwa matumizi ya vyombo vya habari, kwa hisani ya USAID,  zinaweza kupatikana mtandaoni kwa kupitia anuani:  https://flic.kr/s/aHsm7A37YN

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.