Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini Andy Karas azuru miradi mkoani in Iringa

Dar es Salaam, Tanzania. Kuanzia tarehe 13 hadi 17 Novemba, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimarekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) nchini Tanzania Andy Karas alifanya ziara mkoani Iringa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani. Miradi hiyo ni pamoja na ile iliyo katika sekta za kilimo, usimamizi wa maliasili, uhifadhi, ukuaji wa uchumi, afya, ulemavu na elimu.

Katika ziara hiyo ujumbe wa USAID uliweza pia kujionea jinsi masuala ya usawa wa kijinsia na kuwajengea uwezo vijana yanavyojumuishwa katika programu zote za USAID mkoani humo. Hali kadhalika ujumbe huo ulijionea jitihada za kuwasaidia wakulima vijana chini ya mradi wa Mboga na Matunda; ushirikishwaji wa wanawake na vijana wa Kitanzania katika usimamizi wa matumizi bora ya maji chini ya mradi wa uitwao WARIDI (Water Resources Integration Development Initiative); shughuli za kudhibiti maambukizi ya VVU na kuwajengea uwezo vijana wa kike walio katika mazingira hatarishi chini ya mradi wa Sauti; na kuinua uwezo wa watoto kusoma chini ya mradi wa Tusome Pamoja.

Toka mwaka 2014, USAID imekuwa ikitekeleza miradi yake yote ya maendeleo mkoani Iringa kwa kuzingatia mbinu shirikishi na michakato jumuishi (integrated approach) ambapo shughuli zake na zile za wabia wake, kwa msaada wa karibu na serikali za mitaa, hutekelezwa kwa pamoja zikichangia rasilimali ili kupata matokeo makubwa zaidi badala ya kila mradi kutekelezwa kivyake. Jambo hili limeufanya mkoa huu kuwa kitovu muhimu cha misaada ya maendeleo inayotolewa na Serikali ya Marekani na kuwezesha huduma nyingi zilizo katika sekta mbalimbali kuwafikia wakazi wa Iringa.

Kwa taarifa zaidi kuhusu programu jumuishi za USAID mkoani Iringa, tembelea: https://goo.gl/iQtyuG

Picha za ziara hiyo zinazoweza kutumiwa na vyombo vya habari kwa hisani ya USAID zinaweza kupatikana kupitia:  https://flic.kr/s/aHsm9ZyarR

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.