Mradi Mpya Wa Vyombo Vya Habari Na Asasi Za Kiraia Kuinua Fursa Ya Kupata Habari Na Kuimarisha Uandaaji Na Upashaji Habari

Dar es Salaam, TANZANIA.  Tarehe 17 Januari, Serikali ya Marekani kwa kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), imezindua mradi  wa kuimarisha asasi za kiraia na vyombo vya habari  uitwao Boresha Habari Katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Ukiendeshwa chini ya uratibu wa mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Internews na FHI 360, mradi wa Boresha Habari utashirikiana na wabia wa Kitanzania, ikiwa ni pamoja na: Baraza la Habari Tanzania, Tanzania Bora Initiative, na Jamii Media; ili kuboresha weledi miongoni mwa waandishi wa habari na kusaidia kuweka mazingira yaliyo wazi kwa vyombo vya habari. Shabaha kuu ya jitihada hizi itakuwa ni kushirikisha na kujenga uwezo wa wanawake na vijana ili kuinua sauti, usemi na masuala yao katika nyanja mbalimbali za jamii wakiwa ni wazalishaji na watumiaji wa habari.

“Serikali ya Marekani imedhamiria kwa dhati kusaidia kuinua ujuzi na weledi wa vyombo vya habari na asasi zisizo za kiserikali za Kitanzania – hususan katika kuwawezesha wanawake na vijana – kupaza sauti zao na kueleza dukuduku zao kwa ufanisi,”  alisema Mkurugenzi Mkazi wa USAID Andy Karas Wakati wa hafla hii.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, mradi wa Boresha Habari  unalenga kufanya kazi na wadau wa vyombo vya habari katika mikoa ya  Dar es Salaam, Zanzibar, Iringa, Mbeya, Morogoro, Arusha, Manyara, Dodoma, Tanga, Mtwara, Mwanza na Kigoma. Aidha, mradi wa Boresha Habari utatoa mafunzo na msaada wa kitaalamu kwa vyombo vya habari vya humu nchini ukivisaidia kuanza kutumia teknolojia za kidijitali na kuimarisha uwezo wao wa kiusimamizi na kifedha. Hali kadhalika, mradi huu utatoa mafunzo kwa asasi za kiraia ili ziweze kushirikiana vyema na vyombo vya habari katika kusukuma mbele jitihada zao. Kwa kuzingatia umuhimu wa redio za jamii kama vyanzo maarufu vya habari za maeneo husika, mradi wa Boresha Habari utafanya kazi na vituo mbalimbali vya redio nchini kote ili kuboresha uwezo wao wa kitaalamu na uendelevu katika masuala ya kifedha.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe:  DPO@state.gov.