Flag

An official website of the United States government

Ofisi Ya Rais – Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa Yazindua Mfuko Ulioboreshwa Wa Afya Ya Jamii (ICHF)
4 MINUTE READ
Febuari 11, 2021

Dodoma: Jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Suleiman Jafo, alizindua mpango mpya wa kusambaza kadi za Mfuko wa Afya ya Jamii zilizoboreshwa (iCHF) / improved Tiba kwa Kadi (iTIKA) kwa kaya zilizo katika mazingira hatarishi. Kufikia kaya hizi, OR-TAMISEMI imeshirikiana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), kupitia mradi wao wa Kizazi Kipya, ambao unasaidia yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi.

Kadi za bima ya afya za iCHF / iTIKA zinagharamia huduma za jumla za afya, pamoja na huduma za afya ya watoto. Mradi wa USAID Kizazi Kipya umefadhili mwaka wa kwanza wa malipo yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 4.7 za Kitanzania. Ili kuhakikisha kuwa watu hawa walio katika mazingira hatarishi wanaweza kulipia malipo ya kawaida katika miaka inayofuata, USAID Kizazi Kipya husaidia kaya hizi kuongeza mapato yao kwa kuzisaidia kuanzisha biashara ndogo ndogo na kushiriki na vikundi vya kuweka akiba na kukopa.

USAID Kizazi Kipya itatumia mitandao yake iliyopo kutoa kadi za iCHF / iTIKA kwa kaya takriban 93,000 zilizo katika mazingira hatarishi na kwa jumla ya watu zaidi ya 360,000. Kaya zinazofadhiliwa zinatoka katika halmashauri 85 katika mikoa 25 nchini Tanzania. Wanufaika wakuu wa huduma hii ni pamoja na wale walio na watoto wanaoishi na VVU, kaya zinazoongozwa na watoto, kaya zilizo na wazee na walezi waliougua kwa muda mrefu, na kaya masikini sana ambazo haziwezi kukidhi mahitaji ya kimsingi ya familia zao.

Katika maoni yake, Waziri alitoa shukrani zake kwa Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR / USAID kwa msaada huu na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na washirika kuhakikisha makundi yaliyosahaulika yanapata huduma bora za afya popote na muda wanapozihitaji.

Akizungumzia hafla hio, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Andy Karas, alihimiza Serikali ya Tanzania kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya ili kuboresha huduma za afya kwa watu waliosahaulika. “Kuwekeza katika huduma za afya ni uamuzi wa kimkakati wa kukuza ukuaji jumuishi wa uchumi. Watu wapatapo huduma bora za afya na elimu, wanaishi maisha yenye afya na tija.” alisema. Mkurugenzi Mkazi pia alitoa maoni juu ya ushirikiano wa PEPFAR na Tanzania katika juhudi zao za kufikia udhibiti wa janga la VVU. “Kwa udhibiti kamili wa janga la VVU, tutaendelea kuimarisha ushirikiano wetu na Serikali ya Tanzania na asasi za kiraia ili kuendeleza suluhisho endelevu, ndani ya nchi ili kuhakikisha kuwa Watanzania walio katika mazingira hatarishi zaidi wanaweza kupata huduma bora za afya.”