Pemba – Ubalozi wa Marekani una furaha kutangaza kufunguliwa tena kwa Kituo cha Kimarekani Pemba kilichopo ndani ya Maktaba Kuu Chake Chake, Kisiwani Pemba, Zanzibar. Kituo hiki hutoa huduma za kompyuta na Internet bila malipo. Huduma nyingine zinazotolewa ni pamoja na ushauri wa kielimu kwa wanaotaka kwenda kusoma elimu ya juu Marekani, Klabu za Kiingereza kwa wanafunzi wa shule za sekondari, kozi mbalimbali zinazotolewa kwa njia ya mtandao kwa walimu wa Kiingereza, taarifa kuhusu programu mbalimbali za mabadilishano za Marekani na huduma nyingine nyingi.
Vikiwa vimeanzishwa kwa ubia na Serikali ya Marekani, Vituo vya Kimarekani ni vituo vinavyoweka katika maeneo mbalimbali ya kijamii na kuendeshwa na watu wa nchi husika vikilenga kukuza fursa za kielimu, kukuza elimu ya lugha ya Kiingereza na kuhimiza tafakuri yakinifu na majadiliano ya kina kuhusu masuala mbalimbali kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa zisizoegemea upande wowote na internet. Haya ni maeneo ambapo watu wanaweza kujadili na kutiwa hamasa na mawazo, ujuzi na fursa mpya ambazo zina uwezo wa kuleta mabadiliko chanya.
Kikiwa na huduma ya internet ya Wi-Fi, kompyuta ambazo zinaweza kutumiwa na umma na huduma nyingine nyingi, kituo hakitozi malipo yoyote kwa watumiaji. Kituo cha Kimarekani Pemba ambacho kilikuwa kimefungwa kutokana na janga la UVIKO-19, hivi sasa kitakuwa wazi kuanzia siku za Jumatatu hadi Jumamosi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 8:30 adhuhuri. Tunawakumbusha wageni wote kuchukua tahadhari za kiafya wakati wote wanapokuwa kituoni ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono na kutokwenda kituoni wakiwa wagonjwa.