Flag

An official website of the United States government

Taarifa ya Balozi Wright katika kuipatia Tanzania zaidi ya dozi milioni moja za chanjo dhidi ya COVID-19.
3 MINUTE READ
Julai 24, 2021

Marekani ina furaha kuchangia na Watu wa Tanzania zaidi ya dozi milioni moja za chanjo dhidi ya Covid-19. Marekani inasaidia kuiongoza dunia katika kulitokomeza janga hili, kujenga dunia iliyo salama zaidi na iliyokingwa zaidi dhidi ya kitisho cha maradhi ya kuambukiza.  Nchi zote, bila kujali hali zao za kiuchumi, zinahitaji chanjo zinazokidhi viwango vya juu kabisa vya ubora wa kiusalama na utendaji kazi wake.

Toka janga la COVID-19 lilipoanza nchini Tanzania mwaka jana, Serikali ya Marekani imetoa zaidi ya Dola milioni 26 kama msaada wa moja kwa moja katika kukabiliana na janga hilo.  Marekani imedhamiria kwa dhati kuongoza mapambano ya kimataifa dhidi ya janga la COVID-19 na kuongeza kasi ya usambazaji wa chanjo duniani ikiwa mfadhili mkubwa zaidi wa Mpango wa Kimataifa wa Usambazaji Chanjo (COVAX).

Tunachangia chanjo hizi ili kuokoa maisha na kuiongoza dunia katika kulitokomeza janga hili. Aidha, kuchangia kwetu chanjo hizi ni kielelezo cha uimara wa ubia wetu wa miaka 60 na dhamira yetu ya dhati kwa Tanzania. Kwa miongo kadhaa, Serikali ya Marekani kupitia taasisi zake kama USAID na Taasisi ya Kudhibiti Maradhi (CDC) imewekeza katika kuimarisha mifumo na taasisi za kiafya nchini Tanzania ili ziweze kushughulikia kwa haraka mahitaji ya kidharura kama janga hili.

Kama alivyosema Rais Biden:  “Marekani imedhamiria kulishughulikia suala la upatikanaji wa chanjo kimataifa kwa umuhimu, uzito na udharura uleule ulioonyeshwa katika kulishughulikia suala hilo nyumbani.”

Kwa werevu na umahiri wa wanasayansi wa Kimarekani na ustahimilivu na kujitoa kwa dhati kwa watu wa Marekani, leo hii tupo mahali ambapo tunaweza kuwasaidia wengine. Tutaendelea kufanya kila liwezekanalo kujenga dunia iliyo salama na iliyokingwa zaidi dhidi ya kitisho cha maradhi ya kuambukiza.

###