Flag

An official website of the United States government

Salaam za Kipindi cha Sikukuu
6 MINUTE READ
Disemba 21, 2023

Na. Balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael A. Battle Sr.

Disemba 21, 2023

 

Mke wangu Linda na mimi, tuliwasili Tanzania kwa furaha mwanzoni mwa mwaka 2023 ili kuanza ngwe yangu ya pili nikiwa na wadhifa wa balozi.  Toka wakati nilipokabidhi nyaraka zangu za utambulisho kwa Rais Samia Hassan, nimejitoa kwa dhati kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu rasmi ili kuimarisha amani, ustawi, usalama na afya kwa raia wote. Tunaadhimisha kipindi cha sikukuu pamoja na familia na wapendwa wetu, ningependa kuchukua fursa hii kurejea na kutafakari yale tuliyoweza kuyafanikisha pamoja, wakati tukijiandaa kwa kazi iliyo mbele yetu mwaka 2024.

Kuongeza biashara na uwekezaji kati ya Marekani na Tanzania ni mojawapo ya mambo ninayoyapa kipaumbele cha juu nikiwa Balozi. Kufuatia mkutano wa Kihistoria kati ya Rais Samia na Makamu wa Rais Kamala Harris mwanzoni mwa mwaka, tulijizatiti na kukamilisha Majadilino ya Kibiashara (Commercial Dialogue) na wenzetu Watanzania.  Majadilino ni ahadi na azma ya serikali zetu kuboresha biashara na uwekezaji wa pande zote mbili, kuboresha mazingira ya kufanya biashara kupitia teknolojia, uwazi na mageuzi ya kikanuni na kisheria. Majadiliano ya Kibiashara yatakwenda sambamba na mkakati wa kukuza uchumi wa USAID.  Ninaposafiri katika nchi hii nzuri kutoka Zanzibar hadi Kigoma au Arusha hadi Mbeya, ninakutana na wawakilishi wa serikali, viongozi wa asasi za kiraia, wahitimu na washiriki wa programu zetu mbalimbali na wawakilishi wa sekta binafsi nikilenga katika kukuza fursa za kibiashara kwa Wamarekani kufanya kazi na Watanzania.

Chukulia kwa mfano, kitengo cha Kilimo cha USAID, ambacho katika mwaka 2023 kilitenga zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 30 kwa maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa na serikali ya Tanzania.  Hii ni pamoja na kuweka msingi wa kujenga kitovu cha uzalishaji mbolea, kuongeza tija na uzalishaji wa kilimo, kukuza teknolojia za kilimo zinazozingatia mabadiliko ya tabia nchi na kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi katika kilimo.  Msaada huu umeandaliwa mahsusi kuongeza biashara na uwekezaji ukienda sambamba na malengo ya Mkutano wa Kilele wa Viongozi wa Marekani na Afrika.  Zaidi ya hayo, USAID imeboresha uhifadhi wa takriban hekta milioni mbili za ardhi huku ikiwasaidia watu 64,000 kuongeza kipato chao kupitia uhifadhi wa hazina kubwa ya maliasili za Tanzania.  Kukiwa na ongezeko kubwa la watalii na wanafunzi wa kigeni wanaokuja Tanzania, ninafahamu kwamba mambo mazuri bado yanakuja mbele yetu.

Usalama wa Afya kimataifa bado unaendelea kuwa eneo muhimu katika ushirikiano wetu, na uwekezaji mkubwa zaidi wa Marekani unalenga kusaidia afya ya raia wa Tanzania. Tangu mwaka 2003, PEPFAR imetoa Dola za Kimarekani bilioni 7 kwa ajili ya kusaidia kinga, huduma na matibabu ya VVU, na kuimarisha mfumo wa afya nchini Tanzania. Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, PEPFAR kwa sasa inawasaidia zaidi ya watu 1.4 milioni wanaoishi na VVU kwa kupata na kutumia dawa za kufubaza VVU. Katika Siku ya Ukimwi Duniani, nilifurahi kuona Waziri Mkuu Majaliwa akatangaza matokeo ya Utafiti wa Athari za VVU nchini Tanzania wa mwaka 2022 – 2023, ukionyesha kuwa Tanzania iko karibu kudhibiti janga la VVU. Waziri Mkuu alikuwa sahihi alipotoa wito kwa vijana na wanaume kwenda kupima VVU. Tanzania iko karibu sana kufikia malengo ya UNAIDS ya 95-95-95, na upimaji wa VVU ndio ufunguo wa kufikia lengo hilo.

Pale ugonjwa wa Marburg ulipogundulika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwezi Machi, sekta ya afya iliwasiliana na washirika wa kimataifa na kushughulikia changamoto hiyo kwa uwajibikaji na uwazi mkubwa. Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Maradhi cha Marekani (CDC) kwa Fahari kubwa kilishirikiana na Serikali ya Tanzania ili kusaidia katika ufuatiliaji, epidiemolojia, na usimamizi wa data ili kudhibiti mlipuko, ambao ulitangazwa rasmi kuwa umekwisha tarehe 2 Juni 2023.

Nikiwa Balozi, nimefurashishwa sana na falsafa ya Rais kuwa nguzo za demokrasia za vyama vingi nchini Tanzania kuwa ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Mpya, na ninawahimiza timu yetu ya ubalozi kufanya kazi kwa kuzingatia falsafa hii kuitia moyo Tanzania ichukue hatua muhimu, stahiki na zenye maana kuelekea mageuzi ya kweli ya kidemokrasia. Ili kujenga jamii salama, familia zenye afya, kufikia mustakabali bora kwa vijana wa Tanzania, ni muhimu kuendelea kupanua nafasi ya ushiriki wa wananchi. Wananchi wa Tanzania ndio hazina na rasilimali kubwa zaidi ya nchi hii, na tunajivunia kushirikiana nao kuunga mkono mageuzi makubwa ya Tanzania. Tunamaliza mwaka wa 2023 kwa furaha, kwani Shirika la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation – MCC) limeichagua Tanzania kupata ruzuku kwa ajili ya maandalizi ya  programu ya awali  (threshold program) itakayoisaidia Tanzania kufikia malengo ya kiuchumi na ya kimageuzi,  itakapokuwa ikijiandaa kwa  kwa uwekezaji mkubwa zaidi na uwezekano wa makubaliano kamili na MCC (MCC compact).

Ni nchi chache sana duniani zinaweka kipaumbele katika suala la amani na utulivu kama sehemu ya tunu zake kuu, kama wafanyavyo Watanzania. Tunashukuru kwa ushirikiano wetu wa kijeshi unaodhihirika kupitia Mafunzo ya Pamoja ya Kubadilishana ujuzi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kuanza kwa ujenzi wa kambi mpya katika Chuo cha Intelijensia cha Jeshi la Ulinzi la Tanzania.

Wema na ukarimu wa Tanzania unatugusa sisi sote hapa ubalozini na unatupa hamasa ya kutekeleza programu za kimkakati na zenye ufanisi ambazo zitaimarisha urafiki wa muda mrefu baina ya mataifa yetu kwa siku nyingi zijazo. Wakati msimu wa likizo na sikukuu unapoanza na tunapoutazamia mwaka mpya, sisi katika Ubalozi tunawatakia Watanzania wote amani na baraka tele, pamoja na afya njema na ustawi.